Na mwandishi wetu
Watoto zaidi ya 1,886,226 mkoani Mbeya wenye umri chini ya miaka mitano wanatarajia kupewa chanzo ya surua, homa ya kupooza (polio), matone ya vitamin ‘A’ na dawa ya minyoo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk.Seif Mhina, akizungumza na mwandishi wetu amesema kampeni ya kutoa chanjo hizo itaanza Novemba 12 hadi 15 mwaka huu katika Halmashauri zote za mkoa huu.
Alisema kampeni hii inalenga kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa hatari ya surua na homa ya kupooza na kuzuia mlipuko wa magonjwa hayo na kuimarisha kinga kwa watoto hao.
Dk.,Mhina alitoa mchanganuo kuwa watoto 453,127 watapewa chanjo ya surua,polio watoto 535,995, matone ya vitamin ‘A’ 477,770,na dawa za minyoo watoto 419,404.
Kwamujibu wa Dk.Mhina, chanjo ya Surua itatolewa kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi miaka mitano, polio wenye umri wa kuanzia siku moja hadi miaka mitano,matone ya vitamin ‘A’ wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miaka mitano wakati dawa ya minyoo watapewa watoto wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitano.
Alisema chanjo hizo zitatolewa kwa watoto wote bila kujali kama alishawahi kupata chanjo nyingine katika utaratibu wa kawaida unaojulikana kitaalam kama Routine Immunization.
Dk.Mhina alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao katika vituo vya kupatia chanzo vilivyopo katika maeneo yao kwa tarehe hiyo ili kuwezesha kufanikisha zoezi hilo ambalo ni muhimu sana.
0 comments:
Post a Comment