MTOTO AFARIKI BAADA YA KUSHAMBULIWA NA KUNDI LA NYUKI.

Kamanga na Matukio | 03:35 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbozi.
Mtoto Runi Fabi(5) mkazi wa Kitongoji cha Namleya,Ilembo,Kata ya Vwawa,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kung'atwa na kundi la nyuki.

Tukio hilo limetokea Mei 27 mwaka huu majira ya saa sita mchana,wakati akicheza na watoto wenzake nje kidogo ya nyumba yao.

Balozi wa mtaa huo Bwana Hanzi Wega, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha ya kwamba tukio hilo ni la pili kutokea mtaani kwake.

Ameongeza kuwa mwezi Mei mwaka jana mwanamke marehemu Namyugumbi Nzunda, aliuawa baada ya kuvamiwa na kundi la nyuki.

Hata hivyo Baba mzazi wa mtoto huyo Bwana Fabi Mjewa amesema alishangaa kuletewa mwanae akiwa amezirai lakini alipopelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, aliambiwa mwanae kashafariki na hivyo mazishi yake kufanyika Mei 28 mwaka huu katika mtaa wa Ilembo.

WATU WATATU WASHTAKIWA KWA KUJERUHI.

Kamanga na Matukio | 03:34 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watu watatu wakazi wa Tuduma Kati, Wilaya mpya ya Momba, Mkoani Mbeya wameshtakiwa kwa tuhuma za kujeruhi.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Martha Ndabila(30),Gibe Prosper(37) na Victor Haonga(37) ambapo wote kwa pamoja walifikishwa katika Mahakama ya mwanzo Tunduma Mei 29 mwaka huu.

Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Leonard Kazimzuri wa mahakama hiyo, wakidaiwa kumjeruhi Bwana Elias Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya Halmashauri ya mji mdogo wa Tunduma, Mei 28 mwaka huu majira ya saa 5:30 asubuhi.

Akisoma mashtaka mbele ya mahakama hiyo PP Nathani amesema kuwa watu hai wametenda kosa la jinai kifungu cha 241 sura ya 16 ya marekebisho ya sheria ya nchi ambapo kesi hiyo imesajiliwa kwa namba ya 236 ya mwaka 2012.

Baada ya kusomewa shtaka hilo watuhumiwa walikana kutenda kosa hilo na kesi hiyo kupigwa kalenda mpaka June 11 mwaka huu,na Hakimu kuweka bayana dhamana kwa washtakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja ambapo wote walidhaminiwa.

Aidha sababu za wananchi hao na kufikishwa mahakamani ni kutokana na kutokubaliana na taarifa ya mapato na matumizi iliyosomwa katika mkutano wa mtaa,ambapo wananchi hao hawakutaka kukubaliana na taarifa ya Mwenyekiti huyo wa halmashauri  wakidai si sahihi na kwamba amefuja pesa za wananchi zaidi ya shilingi milioni 2.5.

Kufuati hali hiyo walimtaka mwenyekiti huyo Bwana Cheyo kujiuzuru kwa kutia saini kwenye karatasi jambo ambalo kiongozi huyo alilikataa na kuuvunja mkutano majira ya saa 6:30 mchana na wananchi kutawanyika.

Sakata hilo halikuishia hapo majira ya saa 5:00 usiku, Jeshi la polisi liliwakamata watuhumiwa hao kwa mahojiano katika Kituo cha Polisi Tunduma, hali iliyowatia hasira wananchi hao na kusababisha taflani kituoni hapo  baada ya wananchi wengine kutaka kuvamia ili kuwatoa watuhumiwa.

Hata hivyo baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu Jeshi la Polisi Mei 29 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi, lililazimika kuandaa hati ya mashtaka kwa watuhumiwa na kuwafikisha mahakama ya mwanzo, hivyo kushusha hasira ya wananchi hao.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tunduma mheshimiwa Frank Mwakajoka Mwesa,ambaye alikuwa mmoja wa waalikwa kwenye mkutano huo amesema amesikitishwa na kitendo cha wananchi hao kushtakiwa mahakamani kwani hakuona kitendo chochote cha sambulio na kwamba hawezi kuingilia uhuru wa mahakama anaiachia itende haki.

Wakati kesi hiyo ikitajwa mahakamani hapo mlalamikaji  Bwana Cheyo,hakuwepo mahakamani na pia hakuwa tayari kuzungumzia lolote kuhusiana na kesi hiyo.

Kata hiyo imekuwa na migogoro ya mara kwa mara hivyo kufanya eneo hilo kuwa tete huku wanafunzi wakijazana katika vyumba vya madarasa na wengine wakisoma kwa kuchuchumaa madarasani.

WAUMINI WA EAGT KANDETE WAMTUHUMU MCHUNGAJI KWA USHIRIKINA.

Kamanga na Matukio | 05:34 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
 Waumini 45 wa kanisa la EAGT(Evangelical Asemblies of God), Kandete Mwakaleli, Wilaya ya Rungwe,Mkoani Mbeya wameamua kujitenga na kanisa hilo lililopo chini ya Mchungaji Jaremia Mwamwaja wa kanisa hilo kwa tuhuma za ushirikina.

Sakata hilo limetokea Mei 27 mwaka huu katika ibada ambapo mtoto wa Mchungaji huyo aitwaye Lydia Mwamwaja kupanda madhabauni na kushuhudia kuwa yeye anajihusisha na ushirikina ndipo waumini haowalipotaharuki na kumwamuru mchungaji huyo aondoke kanisani hapo na familia yake lakini mchungaji alikataa.

Alipopekuliwa mtoto huyo wa mchungaji alikutwa na hirizi mkono wa kushoto, ambapo alikiri kuwa yeye anajihusisha na masuala ya kushirikiana.

Tukio hili ni lapili kutokea kanisani hapo baada ya lile la kwanza la mwaka 2008,ambapo familia hiyo ya mchungaji ilihusishwa na imani za kishirikina.

Kwa upande wake Mchungaji Mwamwaja, amesema kuwa yeye na familia yake hupendelea kuangalia ni mikanda ya Nijeria, ambapo hujifunza mambo hayo ya ushirikina.

Hata hivyo waumini wawili wa kanisa hilo waliamua kuondoka hivyo kusababisha kanisa kubaki na waumini wachache wengi wao wakiwa ndugu wa familia ya mchungaji huyo.

WATU WAWILI WAMEFARIKI KATIKA MAZINGIRA MAWILI TOFAUTI.

Kamanga na Matukio | 05:19 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watu wawili wamefariki Mkoani Mbeya katika matukio mawili tofauti, likiwemo la mtoto kufariki baada ya kutumbukia mtoni wakati akicheza na wenzake.

Tukio hilo la mtoto huyo aitwaye Alfa Sadiki(2),limetokea katika Kijiji cha Lukululu,Wilaya ya Mbozi Mei 26 mwaka huu majira ya saa sita mchana.

Baba mzazi wa mtoto huyo Bwana Sadick Eliakimu Swajiamesema wakati tukio yeye alikuwa amesafiri kuelekea Tunduma.

Tukio jingine limetokea Kijiji cha Mbuyuni,Kata ya Mbuyu,Wilaya ya Chunya Salome Herman(20) alifariki dunia baada ya kupigwa na jiwe,alipokuwa akipitia njiani Mei 26 mwaka huu majira ya saa tatu usiku.

Katika tukio hilo Bwana Joseph Mwandyehe alikuwa na ugomvi baina yake na wenzie watatu katika eneo la Kilabu cha Mbuyuni, ndipo alipokuwa amelewa alichukua jiwe kwa nia ya kuwapiga wagomvi wake alirusha jiwe na bahati mbaya lilipowakosa basi moja kwa moja na kumkuta marehemu ambayea alisababishiwa majeraha.

Baada ya kupingwa jiwe hilo marehemu alianguka na kukimbizwa katika Kituo cha Afya Mbuyuni na kufariki Mei 27 majira ya saa nne asubuhi.

Wakazi wa eneo hilo mara baada ya kupata taarifa za kufariki, wananchi walitaka wamuue lakini aliokolewa na Katibu tarafa Romward Mwashiuya, kwa kumficha kayika nyumba ya kulalia wageni  kumuepusha kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali.

Bwana Jose[h alipelekwa katika kituo cha Polisi cha Chunya  Mei 17 mwaka huu.

Hata hivyo Kamanda wa jeshi la polisi Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa matukio yote na kwamba uchunguzi kuhusiana na matukio haya.

MWENYEKITI NA MKEWE WASABABISHA WANANCHI KUSUSIA MKUTANO.

Kamanga na Matukio | 04:55 | 0 comments
Mke wa Mwenyekiti wa Kijiji wa Kijiji cha Motomoto Bi Salome Ipopo aliyeketi, ikiwa amekwepa kamera, ambaye alivuruga mkutano kwa kuporomosha matusi kwa kila mwananchi aliyekuwa akichangia hoja katika mkutano wa hadhara baada ya mumewe kutuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji na kufuja pesa za mradi wa maji.
Wananchi wa Kijiji cha Motomoto wakielekea katika mkutano wa hadhara wa kijiji hicho.
Wananchi walioitikia wito wakiwa wameshikwa na butwaa na wakiwa hawajui kinachoendelea baada ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Motomoto Bwana Kassim Mwagala kukana shutuma za kuuza ardhi ya kijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Motomoto Bwana Mwagala, aliyevalia kofia nyeupe akikwepa kupigwa picha.
Kufuatia majibizano hayo wananchi hawakuridhishwa na majibu ya Mwenyekiti na kwamba agenda nyingine zilifichwa hali iliyosababisha wananchi kugoma kuendelea na mkutano na kiongozi huyo kuahirisha mkutano, huku wananchi wakimzomea na kumtaka yeye na serikali yake kujiuzuru mara moja, kitendo ambacho alikipinga na kudai kwamba agenda hizo ziletwe ili mkutano uitishwe siku nyingine.(Picha na Ezekiel Kamanga)

MKE WA MWENYEKITI AVURUGA MKUTANO WA KIJIJI CHA MOTOMOTO, BAADA YA MUMEWE KUWEKWA KITIMOTO.

Kamanga na Matukio | 04:42 | 0 comments
Mke wa Mwenyekiti wa Kijiji wa Kijiji cha Motomoto Bi Salome Ipopo aliyeketi, ikiwa amekwepa kamera, ambaye alivuruga mkutano kwa kuporomosha matusi kwa kila mwananchi aliyekuwa akichangia hoja katika mkutano wa hadhara baada ya mumewe kutuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji na kufuja pesa za mradi wa maji.(Picha na Ezekiel Kamanga).
*****
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mke wa Mwenyekiti wa Kijiji wa Kijiji cha Motomoto Bi Salome Ipopo amevuruga mkutano kwa kuporomosha matusi jana kwa kila mwananchi aliyekuwa akichangia hoja katika mkutano wa hadhara baada ya mumewe kutuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji na kufuja pesa za mradi wa maji.

Hayo yamebainishwa katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji hicho ambapo kila aliyesimama kuchangia hoja mwanamke huyo alikuwa akimtusi na kumzomea kwamba akitaka akalie yeye kiti hicho.

Pamoja na mtuhumiwa Bwana Kassim Mwagala ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, pia wananchi wamekosa imani na Serikali ya kijiji ambapo wajumbe wake ni Moses Njenge, Bi Tukuswiga Kyagi, Bwana Ally Sanga, Adrea Mwailafu, Erick Kipoke, Isaya Joel, Ezron Mwakajila.

Wengine ni Bi Betina Lwiba, Siasa Sagupina, Afyusisye Mwakalinga, Fredy Mwabutenga, Kulwa Mustafa na Mandela Ambwene na Afisa Mtendaji wa Kijiji Bwana Emmanuel Gwimile.

Katika mkutano huo Mwenyekiti na Halmashauri yake wanatuhumiwa kuuza hekari 8 kwa shilingi 250,000 tu hali inayoonesha ni ubadhilifu kwani hakuna kamati yoyote iliyokaa na kuidhinisha uuzwaji wa ardhi na kwenye mikutano iliyopita kiongozi huo alidai atazirejesha lakini mpaka sasa hajazirejesha.

Aidha alidai kuwa alipewa baraka na mkutano wa hadhara, kwani alidai fedha hizo zilitumika katika ukarabati wa Ofisi ya Serikali ya kijiji hali iliyopelekea wananchi kumzomea.

Uongozi huo pia unadaiwa kuchakachua pesa za mradi wa maji ambapo taarifa katika mkutano huo ilisomwa na Afisa mtendaji Bwana Gwimile, ambapo alidai kuwa makusanyo ya pesa za mradi huo ni shilingi 250,000 na kwamba zimetumiwa kwa ajili ya kufunga vifaa vya bomba kijijini hapo.

Agenda hiyo ilipingwa vikali na wananchi hao kwamba vyanzo vingine vya mradi huo havija ainishwa katika taarifa ya Afisa mtendaji, pia wananchi walihoji kwanini hakutumiwa fundi bomba wa kijiji hicho Usaje Edson Mwambeje, ambaye amesomeshwa na kijiji kwa ajili ya kuendesha mradi huo.

Mbali ya taarifa hiyo kukataliwa pia wananchi walikataa kusomewa taarifa ya mapato na matumizi hadi mkutano utakapoitishwa tena..

Kwa upande wake fundi huyo amesema kwamba hakupewa ushirikiano wa kutosha na Kamati nzima ya maji kijijini hapo na kwamba aliitwa na Mwenyeki wa kijiji akiwa na mke wake ofisini, wakimtaka asiendelee na kazi hiyo na hivyo kamati hiyo kuiongoza mwenyewe, ambapo alitumia fursa hiyo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kufuatia majibizano hayo wananchi hawakuridhishwa na majibu ya Mwenyekiti na kwamba agenda nyingine zilifichwa hali iliyosababisha wananchi kugoma kuendelea na mkutano na kiongozi huyo kuahirisha mkutano, huku wananchi wakimzomea na kumtaka yeye na serikali yake kujiuzuru mara moja, kitendo ambacho alikipinga na kudai kwamba agenda hizo ziletwe ili mkutano uitishwe siku nyingine.

Hata hivyo kabla ya mkutano huo Afisa Mtendaji alimzuia Bi Tupokigwe Ipopo, asiulize swali akidai kwamba si mkazi wa kijiji hicho, na wananchi kumzoea kiongozi huyo na kudai kuwa mwanamke huyo ni mkazi halali na ana haki ya kuuliza swali lolote.

Wakati huo huo Wakazi wa Kijiji cha Malamba, wilayani humo wamemtaka Mwenyekiti wao Ngumbushe Mwalyego  kurejesha, pesa za kijiji hicho shilingi 1,400,000 ambazo alizipokea baada ya tozo la faini ya mifugo kutoka kwa wafugaji wa kisukuma, ambapo alikiri kupokea pesa hizo na kwamba angezirejesha lakini tangu Novemba mwaka jana hajaziresha na hataki kuitisha mikutano.

Wameongeza kuwa endapo hatafanya hivyo watamuondosha madarakani mara moja pamoja na serikali yake.VIONGOZI WAJIMILIKISHA ARDHI WILAYA YA MBARALI.

Kamanga na Matukio | 03:31 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbarali.
Viongozi 7 wa Kijiji cha Itamba, Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wanatuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji hicho kwa wafanyabiashara na wao kujimilikisha sehemu kubwa ya ardhi hiyo kinyume na makubaliano.

Hayo yamebaika baada ya kutembelea Kijiji hicho na kukutana na wananchi zaidi ya 200, ambao wameulalamikia uongozi wa kijiji hicho.

Viongozi waliotajwa na Mwenyekiti wa Kijiji Bwana Venance Magiye ambaye anadaiwa kumiliki hekari 35, Afisa Mtendaji wa kijiji Bwana Damson Simasilya hekari 10, Mwenyekiti wa ulinzi Bwana Ally Mpwaga hekari 20, Mjumbe Bwana Aidan Sangula hekari 60.

Wengine ni Bwana Amir Mlamata hekari 20, Majulisho Mwandungu hekari 30 na Jackson Nyiboma hekari 15 ambao wote ni wajumbe.

Ili kuleta usawa katika makubaliano ya mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo miaka 3 iliyopita waliridhia kila mwananchi apate hekari 2 kwa gharama ya shilingi 2,000 kila hekari.

Aidha, mbali ya kujimilikisha hekari hizo zote viongozi hao wanadaiwa kuuza ardi ya kijiji kwa wananchi zaidi ya 11 wasio wakazi wa kijiji hicho cha Itamba.

Mtandao huu umebahatika kunasa wahusika na hekari walizonunua ambapo Bwana Maso ameuziwa hekari 100, Bwaba Samike hekari 20, Bwana Gorogobo hekari 10, Mwalimu Amani hekari 10, Bwana Mbule hekari 20, Bwana Mabeva hekari 18.

Wengine ni Bwana Kilembe hekari 10, Bwana Seti Mhemeji hekari 10 wote ni wakazi wa Kijiji cha Mabadaga, Bwana Majiva wa Kijiji cha Ukwavila ameuziwa hekari 20 na Bwana Chaina wa Kijiji cha Itamba hekari 10.

Hata hivyo katika kuonesha kujichukulia madaraka mmoja kati ya viongozi Bwana Amir Mlamata aliuza shamba la Kijiji kwa gharama ya shilingi 1,300,000 kwa Bwana Kilangila Dotto (67) mkazi wa Itamba bila hata kutoa stakabadhi.

Kwa upande wake  Myenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Magiye amesema kuwa yeye hajauza isipokuwa ardhi hiyo baadhi yao walishindwa kuiendeleza, hivyo walipewa watu wengine, lakini hakubainisha ni wakazi wa kijiji hicho au la na kwamba atatoa ufafanuzi katika mkutano utakaofuata.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA VIJIJINI YAITELEKEZA SHULE iILIYOGHARIMU MIL 80.

Kamanga na Matukio | 03:05 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoani Mbeya imeitelekeza Shule ya Sekondari Galijembe yenye Kidato cha tano na sita, iliyopo Kata ya Tembela wilayani humo.

Hayo yamebainishwa na wananchi baada ya mtandao huu kutembelea shule hiyo na kukuta vyumba vya madarasa yapatayo nane yaliyojengwa kwa nguvu zao, ambapo Serikali haijatoa chochote katika ujenzi huo wa shule hiyo.

Katika uchunguzi huo imebainika kuwa ni zaidi ya miaka 7 halmashauri imeitelekeza shule hiyo ya kisasa iliyojengwa kwa matofali ya saruji, kuezekwa kwa mabati na vyoo vya kisasa, kwa madai kuwa inaichukua shule hiyo kutoka mikononi kwa wananchi hao kwa lengo ya kuiendeleza.

Mtandao huu ulifanikiwa kuiona barua iliyoandikwa na uongozi wa kijiji hicho Mei 5, 2011 juu ya kumkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya vijijini, yenye Kumbukumbu nambari KIJ/145 yenye kichwa cha barua "KIJIJI CHA GARIJEMBE KUKABIDHI MAJENGO MATATU YENYE VYUMBA 8 VYA MADARASA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA".

Aidha nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa Afisa mtendaji wa Kata ya Tembela na Diwani wa kata hiyo, Katibu tarafa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya, Ofisi ya Mbunge Jimbo la Mbeya Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya na Afisa Elimu Sekondari.

Katika hali ya kushangaza au kusikitisha uongozi wa wilaya haujawahi kufika tangu kupokea kwa barua hiyo na wala hawajaiendeleza huku majengo kubaki kama maghofu, bila kujali pesa nyingi zilizowekezwa na wananchi wa kijiji hicho.

Hata hivyo barua hiyo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho kwa niaba ya kijiji, na kupokelewa na Halmashauri hiyo Mei 9, 201.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Mchungaji Lackson Mwanjale, aliahidi kukutana na wananchi Mei 22 mwaka huu kwa nia ya kuzungumza naye, lakini licha ya kufika kijijini hapo kiongozi huyo alitoa sababu ya kuwahi msibani, hali iliyowasononesha wananchi hao wasijue la kufanya.

Kata hiyo ya Tembela ipo kilomita 22 kutoka jijini Mbeya na haina shule yoyote ya kidato cha 5 na 6, hivyo wanafunzi wanaojaliwa kuendelea na masomo hulazimika kusoma jijini hapa au Wilaya ya Rungwe ambako kuna shule hizo na kupingana na dhana ya kusogeza huduma kwa wananchi kuwa tete.

Shule hiyo imegharimu zaidi ya shilingi 80,000,000 ambazo zote ni nguvu za wananchi huku Serikali haijatoa chochote kama ilivyoada kuwa wananchi wajenge hadi kufikia usawa wa lenta na Serikali kumalizia.

BREAKING NEWS:- Viongozi wajimilikisha ardhi Wilaya ya Mbarali.

Kamanga na Matukio | 05:17 | 0 comments
*Mwenyekiti ajimilikisha hekari 35 za ardhi, Afisa mtendaji wa kijiji hekari 20 na mwingine auziwa hekari 100.

****Endelea kufuatilia mtandao huu ili kupata taarifa kamili****

BREAKING NEWS:- HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA VIJIJINI YAKABIDHIWA SHULE YA SEKONDARI, YAITELEKEZA!!

Kamanga na Matukio | 05:14 | 0 comments
*Mbunge aingia mitini kuongea na wananchi.
*Madarasa 8 yajengwa kwa nguvu za wananchi, ni zaidi ya miaka 5 hayajatumika.
*Wakuu wa wilaya watatu wa ahidi bila utekelezaji.

NAO WANAFURAHIA MAISHA KAMA WENGINE

Kamanga na Matukio | 05:09 | 0 comments

Nimewakuta kijiji kimoja hivi mbali lakini hata nikikutonya huwezifika.
Wanatokea katika nyumba hii
Na baadaye hujichanganya na wenzao katika maeneo haya nyakati za jioni.(Picha na Rashid Mkwinda).

MTOTO AFA MAJI AKIJARIBU KUOKOA KANDAMBILI/YEBOYEBO.

Kamanga na Matukio | 05:08 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mkazi wa Kitongoji cha Mwanjelwa, Kijiji cha Itaka, Kata ya Itaka, Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya Daniel Bahati Mgala (3) amefariki dunia katika kisima cha maji ya kufyatulia matofali.

Tukio hili limetokea kijijini hapo Mei 23 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi wakati marehemu akiwa na mwenzake alikuwa akiifuata Yeboyebo moja iliyotupwa na mwenzie katika kisima hicho alipojaribu kuifuata alizama na kufa papo hapo baada ya kunywa maji hayo.

Aidha mwenzake alipoona kazama alimwita mzazi Bahati Mgala na alipofika alikuta mwanae amekwishafariki ndipo alitoa kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Bwana Nsinkini na Mwenyekiti Bwana Mwashilindi.

Viongozi hao baada ya kupewa taarifa hizo moja kwa moja walizifikisha katika Kituo cha Polisi, ambapo askari wa jeshi hilo walifika na Daktari wa Zahanati ya Nambizo Bwana Mtambo na kuthibitisha kifo hicho cha mtoto huo.

Mara baada ya kukamilika uchunguzi mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko ambapo maziko yalifanyika katika makaburi ya Kijiji cha Shitungulu, Wilaya ya Mbozi majira ya saa tano asubuhi.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa tukio hili na kwamba uchunguzi wa tukio hili unaendelea.

KAMANDA NYOMBI AFANYIWA SHEREHE YA KUAGWA NA MJATA NA APEWA UCHIFU.

Kamanga na Matukio | 05:49 | 0 comments
Pichani aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi(wa pili kulia), ambaye ametawazwa kuwa Chifu na kupewa jina la Chifu Mwalyembe, akishikana mkono na Chifu wa kabila la Wanyiha katika sherehe ya kumuaga zilizofanyika katika Uwanja wa monesho ya Nanenane maarufu kwa jina la Uwanja wa John B. Mwakangale jana. Kamanda Nyombi amehamishiwa makao makuu ya jeshi hilo Jijini Dar es salaam.
Kamanda Nyombi akiwa na baadhi ya machifu wa makabila ya Mkoa wa Mbeya, jana katika sherehe ya kuagwa kwake.
Kamanda Nyombi akisalimiana na mmoja wa wanachama wa Chama cha Muungano wa Jamii Tanzania(MJATA).
Chifu Merere wa kabila la wasangu.
Baadhi ya wanachama wa Chama cha Muungano wa Jamii Tanzania(MJATA), waliohudhuria sherehe za kumuaga aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Nyombi.
Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya(Mbeya Press Club), Bwana Christopher Nyenyembe, akizungumza jambo katika sherehe za kuagwa kwa Kamanda Nyombi.
Kamanda Nyombi(Kulia) akiwa sambamba na Mwenyekiti wa MJATA Chifu Soja Masoko.
Mwenyekiti wa MJATA Chifu Soja Masoko, akizungumza katika sherehe za kuagwa kwa Kamanda Advocate Nyombi.
Burudani haikuwa nyuma, Wanachama wa MJATA akisherehekea kutawazwa kwa Kamanda Nyombi kuwa chifu, ambapo jina hivi sasa anaitwa Chifu Mwalyembe.(Picha na Ezekiel Kamanga na Ronard Bahame).

MICHUANO YA NYOMBI CUP YAENDELEA MKOANI MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:48 | 0 comments

Kikosi cha timu ya Forest, kilichoibuka na ushidi wa goli 3-1 dhidi ya timu ya Isanga katika mashindano ya Kombe la Nyombi, na kuibuka na ushindi wa goli 3-1, katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, Jijini Mbeya.
Kikosi cha timu ya Isanga kilichofungwa goli 3-1 dhidi ya  timu ya Forest, jijini hapa.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi wa mkoa wa Mbeya Bwana Adam Simfukwe akisalimiana na waamuzi wa mpambano huo katika ufunguzi wa michuano ya Kombe la Nyombi, katika uwanja wa Ruanda Nzovwe.

KAMPENI ZA UCHAGUZI CHUO KIKUU CHA TEOFILO KISANJI (TEKU) ZAZINDULIWA RASMI.

Kamanga na Matukio | 05:45 | 1comments
*Wanawake wawili wajitokeza kugombea nafasi ya Urais na Makamu Rais.
Habari na Ezekiel Kamanga.
Kampeni za uchaguzi wa kumpata Rais wa Chuo kikuu cha Teku, zimezinduliwa rasmi jana katika ukumbi wa Mwasakafyuka huku wagombea wakinadi sera zao.

Kampeni hizo zilizinduliwa na Dakta Mozes D, na kusimamiwa na mkufunzi wa chuo Bwana Alawi Mikidadi ambapo Mkurugenzi wa uchaguzi Bi Nyemba Joyce aliweka hadharani wagombea watakao wania viti vya urais na makamu rais.

Majina hayo upande wa rais ni Bi Somi Irene, Bwana George Godbless na Joshua Jason na upande wa Makamu ni Bi Wilson Gwantwa, Bwana Yohanna Yesse na Deus Petro.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Bwana Kavenga Emmanuel amesema kwamba mchakato wa uchaguzi ulianza Mei 9 mwaka ahuu kwa kujaza fomu ambapo wanachuo 70 walijitokeza kuomba nafasi mbalimbali.

Aidha Mei 19 na 20 wagombea walifanyiwa wagombea usaili na kwamba majina yaliyotajwa hapo juu ndio yaliyopitishwa na tume hiyo na kwamba kampeni zimeanza rasmi jana ambazo zitaendelea mpaka Mei 28 asubuhi na uchaguzi utafanyika Mei 29 mwaka huu na matokeo yatatangazwa mei 30 mwaka huu na viongozi wote Rais na baraza la mawaziri kuapishwa Juni mosi mwaka huu.

Mwenyekiti huyo Bwana Kavenga amewataka viongozi hao kufanya kampeni za amani bila matusi kwani kampeni kwa kufanya hivyo haitawasaidia kupata kura, bali itawashushua heshima zao.

Kwa upande wake Rais anayemaliza muda wake Bwana Ambukege Imani ameishukuru tume ya uchaguzi kwa mchakato mzima na anafurahi kumaliza muda wake chuo kikiwa na amani na kuwataka watakaopata nafasi za kuongoza wazingatie sheria, demokrasia na upendo ili kuleta mshikamano katika chuo, ili wanaoongozwa wajisikie kuwa na amani kuwepo chuoni hapo badala ya kutatua migogoro isiyokuwa na maana.

Baadhi ya wabunge walipita bila kupingwa, kutokana na baadhi ya maeneo waliyokuwa wakiyagombea kutokuwa na wapinzani.

Hata hivyo kujitokeza kwa wanawake kumeleta msisimko wa uchaguzi huo huku wanawake wakitoa majigambo kuwa wanawake wanaweza hata pasipo kuwezeshwa na kwamba chuo hicho hakijawahi kupata viongozi wa juu ambao ni wanawake na kwamba imefika zamu yao kuongoza.

RAIS DKT. JAKAYA KIKWETE AMUAPISHA PROFESA MARK MWANDOSYA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM JANA.

Kamanga na Matukio | 05:19 | 0 comments
 Waziri wa nchi katika ofisi ya Rais asiye na Wizara maalum Profesa Mark Mwandosya akila kiapo mbele ya Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ikulu jijini Dar es Salaam jana asubuhi.Wapili kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue.Na watatu kulia ni Karani wa Baraza la Mawaziri Bwana Gerson Mdemu.
Profesa Mwandosya akipokea miongozo ya kazi baada ya kula kiapo Ikulu jana asubuhi.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza na kumtakia mafanikio Profesa Mwandosya muda mfupi baada ya kumuapisha ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimsaidiaWaziri wa nchi katika ofisi ya Rais asiye na Wizara maalumu Profesa Mark Mwandosya kushuka katika ngazi za Ikulu baada ya kumuapisha jana asubuhi.
Waziri Profesa Mark Mwandosya akiwa katika mazungumzo na Rais Dkt. Jakaya Kikwete muda mfupi baada ya kula kiapo Ikulu jijini Dar es Salaam jana asubuhi.(picha na Freddy Maro).

AJIRA KWA WATOTO, JAMANI HII YOTE ANGALAU WAPATE CHOCHOTE NA KWENDA SHULE.

Kamanga na Matukio | 05:18 | 0 comments

Watoto hawa walikutwa Mtaa wa Mabatini Jijini Mbeya, wakijishughulisha na biashara ya uuzaji wa sambusa na maandazi, hii yote ni kuhakikisha angalau wanapata kiasi chochote cha fedha kitakachowawezesha kwenda shule na kiasi kingine kikisaidia matumizi ya nyumbani.(Picha nq Godfrey Kahango).

WATU WAWILI WAFARIKI KATIKA MATUKIO MAWILI YA AJALI MKOANI MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:17 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watu wawili wamefariki dunia, katika matukio mawili ya ajali ya barabarani wilayani Mbarali na Rungwe, Mkoani Mbeya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi amesema ajali ya kwanza iliyotokea katika Wilaya ya Mbarali, mei 20 mwaka huu majira ya saa 10 jioni barabara ya Mbeya/Iringa gari nambari T 536 APU likiwa na tela lenye nambari T 330 APD aina ya Scania.

Gari hilo lilikuwa likitokea Jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Mbeya likiendeshwa na dereva aitwaye Ismail Kiteve iliacha njia na kupinduka kisha kusababisha kifo chake.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo iliyopo Rujewa, na chanzo cha ajali hiyo kimetajwa kuwa ni mwendokasi na upelelezi wa tukio hili unaendelea.

Aidha, Kamanda Nyombi amesema ajali nyingine imetokea Wilaya ya Rungwe majira ya saa 7 mchana, eneo la Katela barabara ya Mbeya/Tukuyu wilayani humo ikihusisha gari aina ya Toyota Coaster lenye nambari T 672 AWK.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Steven Mwambola(40), mkazi wa Mtaa wa Bagamoyo Tukuyu ilimgonga mwendesha pikipiki nambari T 628 BUL aina ya T-Better aitwaye Salim Jimu(26), mkazi wa Ntokela na kusababisha kifo chake papo hapo na abiria wake Gody Julius(17) kujeruhiwa.

Hata hivyo majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mission Igogwe na dereva wa gari amekamatwa na gari lipo kituo cha polisi, kutokana na  mwendokasi uliyopelekea ajali hiyo na upelelezi wa tukio hili unaendelea.

UCHAMBUZI WA KILIMO CHA TUMBAKU

Kamanga na Matukio | 05:17 | 0 comments
Habari na Ester Macha, Chunya.
Zao la Tumbaku ni zao ambalo limekuwa likiwakomboa wananchi na hivyo kupunguza ukali wa maisha waliyonayo hasa maeneo ya vijijini ambako wananchi wake wamekuwa na maisha magumu,licha ya kuwakomboa wananchi pia hata serikali imekuwa ikiongeza mapato yake kupitia halmashauri zake za wilaya zinazolima zao hilo.


Kilimo hicho cha Tumbaku kimekuwa kiingizia serikali dola za kimarekani 614.8 kutokana na ushuru unaotolewa baada ya mauzo ya zao hilo kwa wakulima.Kwa kutambua hilo serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vyama vya ushirika ambavyo vimeundwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima vinaboreshwa na hata kusaidia ili viweze kupata mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha lengo likiwa ni kumsaidia mkulima ili aboreshe kilimo cha tumbaku.Vile vile hata ukiangalia katika halmashauri za Wilaya nchini ambazo zinalima tumbaku katika mapato yao ya halmashauri asilimia kubwa wamekuwa wakipata mapato makubwa kutokana na kilimo cha zao hilo na ndio kimekuwa mkombozi kwao.Hata hivyo kilimo hicho kwa muda mrefu kimekuwa mkombozi kwa wakulima na hivyo kumwondolea umasikini  na hata halmashauri za Wilaya nchini ambazo mikoa yake inalima Tumbaku zimekuwa zinaongeza kipato kutokana na uuzaji wa Tumbaku ambapo kwa miaka miwili mfululizo zaidi ya sh.Bil.26 zimepatikana.Hivi karibuni  Chama kikuu Cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Wilayani Chunya (CHUTCU LTD) kilifanya mkutano mkuu wa kawaida  na kuhudhuliwa na wanachama  wa vyama vya ushirika vya Msingi 21(AMCOS) ambavyo vinalima zao la Tumbaku  kupitia wanachama wake wa vyama vya ushirika vyenye wakulima zaidi ya 8,057.Akizungumza  kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bi. Mariamu Mtunguja anasema kuwa mkutano huo uwe  na manufaa na ambao utalenga kujadili na kujenga ushirikiano na kukuza zao la tumbaku ambalo ni kichocheo cha maendeleo kwa wakulima.Bi. Mtunguja anasema kuwa ili vyama vya ushirika viweze kuwa imara hakuna budi viongozi wanaopata madaraka kuhakikisha kuwa wanatatua matatizo ya wakulima ambao wamekuwa na matatizo mbalimbali katika kilimo cha Tumbaku hususani maeneo ya vijijini."Ndugu zangu viongozi hakikisheni mnafanya kazi vizuri ili kuondoa maswali kwa wakulima wenu kuwa mlipokuwa madarakani mlifanya nini, badala ya kiongozi kuhoji ushirika umemfanyia nini alipokuwa madarakani "alifafanua kiongozi huyo.Hata hivyo Katibu Tawala huyo aliwataka wanaushirika kuwa mfano mzuri wa  kuigwa na wengine kwa kuondoa migogoro iliyopo ndani ya ushirika badala  yake wafanikishe maendeleo  mazuri kwa  wakulima waliowachagua na kwamba hiyo itawafanya waliowachagua wawe na imani na uongozi uliopo madarakani.Akizungumzia kuhusu takwimu za uzalishaji wa zao hilo Kiwilaya Bi.Mtunguja anasema kuwa mekuwa ukipanda  kutoka tani 5,361 kwa msimu wa mwaka 2008/2009 hadi tani tani 7,540 kwa msimu wa mwaka 2009/2010 ikiwa ni ongozeko la zaidi ya asilimia 28.9 huku msimu wa mwaka 2010/2011 kukiwa na tani 12,570 zilizalishwa ambayo ni sawa na ongozeko la asilimia 40.21.Hata hivyo Katibu Tawala huyo anasema kuwa kuongozeka kwa uzalishaji huo kumechangiwa na wanaushirika kuanza kujitegemea na hivyo kurudisha tija kwa wakulima kutokana na bei ya pembejeo inayotolewa bila faida ambazo zilikuwa zinawekwa na makampuni wakati wao wakiwa wanafanya biashara ya tumbakuAidha anaongeza kuwa  bei nzuri ya Tumbaku iliyotolewa kwa msimu wa mwaka 2008/2009/2010 ambayo  ilitokana na utaratibu wa wakulima kupitia vyombo vyao vya ushirika  kuagiza na kusambaza pembejeo kumejenga imani  kubwa na makampuni kuamini kuwa wanaushirika wanaweza wakiamua kwa umoja wao.Anasema kuwa  pia mfumo huo unaweza kupunguza kasi ya ongozeko la gharama za kilimo cha tumbaku hasa pembejeo za kilimo ambazo zimekuwa shida kwa wakulima.Hata hivyo Katibu Tawala huyo anasema kuwa kutokana na kuthamini wakulima wake serikali itaendelea kuunga mkono kwa kuvidhamini vyama vya ushirika kupata mikopo kutoka katika mabenki mbalimbali ili waweze kuboresha kilimo cha tumbaku.Kuhusu kudangwanywa wakulima Bi. Mtunguja aliwataka wakulima kuacha kudanganywa na watu wasiopenda  maendeleo ya ushirika kwa kuwaambia pembejeo zinatolewa na wanaushirika  kwa bei  kubwa na hazijakidhi

viwango na kusema kuwa yote ni kutaka kuwakatisha tamaa ili warudi kwenye shida walizokimbia.Aidha Bi. Mtunguja anasema kuwa licha ya kuwa na ongozeko hilo la uzalishaji wa tumbaku la zaidi ya asimilia 100 bado bei ya tumbaku ilishuka kutoka wastani wa USD 2.34 kwa kilo katika msimu wa mwaka 2010/2011 hadi kufikia wastani wa dola 1.4 kwa tumbaku ya mvuke katika msimu wa kilimo uliopita.Anasema kuwa hata baada ya  mahitaji kuongozeka kimataifa tumbaku ilihitajika tena kwa wingi na ndio maana msimu ujao wa mauzo  bei ya msingi ya Tumbaku ya mvuke imepanda kufikia dola za kimarekani 1.82 kwa kilo na bado kuna makampuni yamelata mahitaji mengine.Aidha Katibu Tawala huyo amewataka wakulima wa tumbaku kulima mazao mbadala kutokana na zao hilo kuendelea kupigwa vita na wanaharakati mbalimbali duniani.Anasema kuwa licha ya kuwa zao hilo bado linaendelea kupigwa vita lakini ni vema wakulima  pia wakajikita zaidi na mazao mengine ambayo yanakubali katika maeneo hayo ambayo nayo yatakuwa mkombozi kwa mkulima.Bi. Mtunguja anasema kuwa kauli hiyo hailengi kukataza kilimo cha zao hilo bali kuanza kuchukua tahadhari  mapema kwakuwa hakuna ajuaye nini yatakuwa matokeo ya hoja zinazojadiliwa na kupiganiwa na wanaharakati wanaopinga uvutaji wa sigara.Aliyataja mazao yanayoweza kupewa nafasi na kuleta manufaa makubwa kwa wakulima kuwa ni pamoja na ufuta unaostawi katika ardhi ya wilaya ya Chunya, karanga pamoja na alizeti.Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHUTCU Wilaya ya Chunya Bw. Sebastian Mogela amekiri ushirika kuendelea  yategemea makampuni ni kuchelewa kupiga hatua kimaendeleo akisema yapo kwaajili ya kufanya biashara yapate faida na si kutoa misaada kwa wakulima.Bw.Mogela amesisitiza kuwa za umuhimu wa chama kikuu hicho kuwa na maofisa ugani wake ili waweze kusimamia kwa karibu kilimo hicho na kuleta manufaa zaidi kwa wakulima badala ya kuendelea kutumia wataalamu wa makampuni yanayonunua tumbaku.Anasema kuwa hiyo itasaidia wakulima kupatiwa ushauri kupitia maafisa wao kuliko kutumia makampuni binafsi anayonunua tumbaku.Hata hivyo kwa kutambua umuhimu wa zao la tumbaku bodi  ya Tumbaku nchini  hivi karibuni ilifanya mkutano wake maalamu ambao lengo lake kuu ilikuwa ni kujadili kupandisha kiwango cha uzalishaji kutoka tani 50,000 mwaka 2009 hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka 2010 jambo ambalo lilifikiwa kwa kuzalisha tani 126 sawa na asilimia 103.Akizungumza katika huo maalamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Vita Kawawa anasema kuwa pia lengo kubwa ya mkutano huo pia ni kuangalia changamoto za zao hilo na  na mafanikioAnasema halmashauri za Wilaya nchini  pia zinaongeza kipato kutokana na uuzaji wa Tumbaku ambapo kwa miaka miwili mfululizo zaidi ya shilingi bilioni 26 zimepatikana.Pia Bw. Kawawa anasema kuwa  mkutano huo uelekeze nguvu zake kuwakomboa wananchi wa Mkoa huo jinsi ya kufaidika kwa kupata ajira kutokana na kiwanda cha kusindika Tumbaku ambacho mpaka sasa kimekaa bila kufanya kazi zaidi ya miaka 10.Hata hivyo Meneja Mkuu wa CHUTCU Wilayani Chunya Bw.. Bakari Kassia ametaja mikoa ambayo inalima tumbaku kuwa ni Mbeya, Shinyanga, Ruvuma, Iringa,Tabora, Rukwa mkoa wa katavi,Singida na Kigoma.Anasema kuwa katika mikoa hiyo nane ndo imekuwa ikizalisha tumbaku kwa wingi na kwamba kwa Mkoa wa Mbeya ni Wilaya ya Chunya ambayo inalima kwa Tarafa tatu ambazo ni Kiwanja, Kwimba na Kipembawe.Hata hivyo anasema kumekuwepo na changamoto mbali mbali katika halmashauri ya wilaya ya Chunya kushindwa kuwahimiza wananchi kuhusu kilimo cha tumbaku  wakati ndo kinaongoza kuwapatia mapato, kingine ni maafisa ushirika kushindwa kuhimiza wananchi kutokana na halmashauri kushindwa kuwapatia mahitaji muhimu ili waweze kuwahimiza wananchi.

MIRADI 7 ILIYOGHARIMU MILIONI 407.3 YAFUNGULIWA WILAYANI MBARALI WAKATI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA.

Kamanga na Matukio | 05:58 | 0 comments
  Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Peter Pinda akiwasha Mwenge wa Uhuru kitaifa jana katika Uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine ulipo jijini Mbeya. 
*********
Habari na Angelica Sullusi, Mbarali.
Jumla ya miradi saba inayogharimu kiasi cha shilingi milioni 407.3 imefunguliwa na Kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa Kapteni Honest Mwanosa, katika Wilaya ya Mbarali ambapo shilingi milioni 102.6 zimechangiwa na wananchi,milioni 39.2 fedha za halmashauri na milioni 265.4 zikitolewa na Serikali Kuu
 

Kapteni Mwanosa amefungua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kijiji cha Itipindi kata ya Mawindi kilichogharimu shilingi milioni 83.8 kilifunguliwa shilingi milioni 2.4 zikichangiwa na Halmashauri na Serikali Kuu ikichangia milioni 81.4. 
 
Banda la upimaji wa VVU kwa hiari katika kijiji cha Mkunywa lililogharimu shilingi milioni 2.5 fedha toka halashauri na nyumba ya mwalimu Kata ya Madibila iliyogharimu milioni15.5,milioni 14.5 nguvu za wananchi na milioni moja toka Serikali Kuu.
 
Pia ametembelea na kuweka jiwe la msingi katika miradi mingine ya maendeleo ya wananchi ambapo ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya sekondari Mshikamano Kata ya Igurusi vinavyogharimu shilingi milioni 44.2, shilingi milioni tisa imechangiwa na wananchi,milioni 32.4 kutoka halmashauri na milioni moja ikitoka Serikali kuu.

Miradi mingine ni ghala la kuhifadhia mazao katika kijiji cha Mbuyuni kata ya Mapogoro lililogharimu shilingi milioni 79.1 za wananchi, ufunguzi wa kituo cha raslimali kilimo katika kijiji cha Igomelo kilichogharimu shilingi milioni 150 fedha kutoka serikali kuu.

DC MBEYA ALITAKA JESHI LA POLISI KUFUATA MAADILI YA KAZI YAO.

Kamanga na Matukio | 05:58 | 0 comments
Na Kenneth Ngelesi, Mbeya
Mkuu wa wilaya ya Mbeya Dr Noman Sigalla amelitaka jeshi la polisi kuacha kutumia ubabe na kutopendelea baadhi ya watu wa kada fulani katika kutekeleza majukumu yao kwani kufanya hivyo huchangia watu kutokuwa na imani na jeshi hilo na baadaye kutokea vurugu.
 
Rai hiyo alitoa na Mkuu huyo mpya wa wilaya mbele ya kamati ya ulinzi na usalama  ya wilaya wakati akikabidhiwa ofisi hiyo na mtangulizi wake aliyestaafu Evansi Balama ambapo  shughuli za makabidhiano  zilifanyika siku ya jumatano katika ofisi za Mkuu wa wilaya zilizopo Mbeya mjini.
 
Dr. Sigalla amesema kuwa kutokana na uzoefu wake kwamba baadhi ya askari wa jeshi hilo wamekuwa na tabia ya kutoa maamuzi yenye upendeleo wa jamii au vyama fulani  hivyo kupekelea vurugu sisizo za lazima.

Amesema kuwa kutokana na wananchi wengi kuwa na uelewa wa hali juu wamekuwa wepesi wa kung’amua mambo juu ya utendaji wa baadhi ya askari na wananchi wengi kutokubaliana na maauzi hayo.

Ametaka wananchi wa wilaya ya Mbeya kutokuwa tayari kunyanyasika na mtu kutokana na ubaguzi wa chama, kabila, kwani kwa kufanya hivyo ni kudhorotesha maendeleo ya wilaya na mkoa na taifa pia.

Amesema inapotokea mtu amevunja sheria za nchi jambo ambalo alisema kuwa hata kuwa tayari kuona mwanachi yeyote ananyanyasika na jeshi hilo kwa tatizo la kihitikadi za vyama.

Akizungumzia suala la migororo ya ardhi alisema kuwa anatambua wazi kuwa ni moja ya changamoto kwake kwani wilaya aliyotoka ya Hai Mkoani Kilimanjaro ndiko kwenye migogoro zaidi.

Mkuu huyo wa wa wilaya alisema hatalifumbia mambo jambo la watumishi wasio waaminifu katika ofisi yake kwani katika taarifa aliyopata kutoka kwa mtangulizi wake inaonyesha kuwa watumishi wengi wamekuwa wakitoa taarifa zisizosahihi hasa wakurugenzi.

Hata hivyo alitoa wito kwa watumishi wa serikali kufanya kazi kwa kushirikiana na vyombo vya habari kwani watumishi wengi wamekuwa wakikwepa kufanyakazi na wanahabari.
 
‘Inasikitisha sana na mara nyingine serikali inalaumiwa na wananchi kwa sababu ya watumishi ambao hawako  tayari kufanyakazi na vyombo vyetu vya habari, sasa unakuta kuna mradi serikali imetumia zaidi mil 800 lakini siku ya kufungua mnashindwa kuwaita waandishi wa habari ambao hata malipo yao hayazidi shilingi laki mbili  kama mnafanya hivyo mnadhani wananchi watajuaje kwamba serikali  yao inafanyakazi’ alisema Dr Sigalla

Kwa upande wake Mkuu aliyemaliza muda wake wa utumishi Evans Balama alisema wilaya ya Mbeya mjini ni ngumu kuliko wilaya zote alizowahi kufanyakazi hasa katika utekezaji wa majukumu ya kiserikali wananchi wengi wamekuwa wabishi.

Aidha amebainisha baadhi ya idara zenye matatizo na kumtaka Dr Sigalla kuwa makini nazo na zimekuwa zikileta migogoro mingi ikiwa ni pamoja na Idara ya Ardhi ambayo  watumishi wake wengi siyo waaminifu na Jeshi la polisi.

Dr Sigalla ameteuliwa kuwa  Mkuu wa wilaya ya Mbeya hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete akitokea wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro uteuzi ulifanyika nchi nzima, na kuapishwa Mei 16 pamoja na wakuu wote wa wilaya nane za mkoa na Mkuu wa Mkoa huyo Abasi Kandoro, Ikulu ndogo iliyopo Mbeya mjini na kukabidhiwa jukuma la kuziongoza halmashauri mbili ambazo ni Mbeya mjini na Mbeya vijijini.

HUKU NA KULE NA KULE + UKOSEFU WA NISHATI JIJINI.

Kamanga na Matukio | 05:57 | 0 comments
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini(CHADEMA) Joseph Mbilinyi,"Sugu" akiwahutubia wakazi wa Mabatini Jijini Mbeya, ambapo alifika kwa lengo la kuwahamasisha kuhusina na suala la maendeleo jijini humo.
  Mafundi wa Umeme wakiwa wanaweka nguzo za taa  za barabarani eneo la Mwanjelwa kama walivyo kutwa barabara hizo zimeenezwa maeneo mengi ya barabarani jijini humo ambapo wananchi wameonekana kufurahishwa na kitendo cha kuwekewa taa barabarani, licha ya kutengeneza taa hizo lakini zimekuwa zikiharibiwa na madereva wazembe kutokana na wakati mwingine kuibiwa kwa Circut braker hali inayopelekea kushindwa kwa kufakazi kwa ufanisi.
Mkazi wa Mabatini akiwa ametoka kutafuta nishati ya kuni kwa ajili ya mahitaji  ya kupikia nyumbani kama alivyokutwa jana.
Kijana ambaye hakufahamika jina lake mara moja akiwa amemsaidia Bibi kizee kubeba kuni alipotoka polini kutafuta nishati ya kuni za kupikia nyumbani,eneo la Mabatini jijini Mbeya
(picha na Godfrey Kahango).
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger