TAMKO LA RAIS NA AMIRI JESHI MKUU JAKAYA MRISHO KIWETE KUHUSU TUKIO LA KUSHAMBULIWA NA KUUWAWA KWA WANAJESHI SABA WA JWTZ WALIOKUWA WAKILINDA AMANI DARFUR SUDAN.

Kamanga na Matukio | 02:52 | 0 comments
Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa vijana saba hodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur, Sudan.

Kwa hakika, Rais amesikitishwa sana na kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi wa Sudan na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.

Aidha, Rais Kikwete anaungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo waweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunynge na familia za wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na waassi.”

Rais Kikwete ameongeza kumwambia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”

Amesisitiza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao. “

“Aidha, kupitia kwako, natuma salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza. 


Wajue kuwa uchungu wao ni uchungu wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. Vile vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za marehemu. Amina”.

Kwa walioumia, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia na Watanzania wenzangu katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo tukiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.”

Vijana hao waliopoteza maisha yao na walioumia, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika Darfur kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi kiasi cha kilomita 20 kutoka Khorabeche saa tatu asubuhi jana, Jumamosi, Julai 13, 2013.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

14 Julai, 2013

MISAADA ZAIDI YAENDELEA KUTOLEWA KWA MTOTO ALIYEFUNGIWA NDANI MIAKA MIWILI.

Kamanga na Matukio | 02:48 | 0 comments
 Christian Mwakapusya Mtanzania anaeishi Marekani  akiwa amembeba mtoto Joshua Joseph baada ya kumtembelea nyumbani kwao Iyunga Jijini Mbeya

 David Mwakapusya ambaye alifuatana na Baba yake akitoa msaada wa nguo kwa mtoto ambaye hakufahamika jina lake kwa niaba ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu mtaani hapo.
 Baadhi ya Majirani wa familia ya Joshua wakiwa na nguo walizopewa na Christian Mwakapusya
 Christian Mwakapusya akizungumza na mama mlezi wa mtoto Joshua Joseph Nyumbani kwake Iyunga Jijini Mbeya.

Christian Mwakapusya akizungumza na Amina Mwasankinga aliye simamishwa masomo kwa kisingizio cha ushirikina alipo kutana nae katika Ofisi za Mbeya yetu.
******************

MTANZANIA anayeishi Marekani Christian Mwakapusya aliyeguswa na kitendo alichofanyiwa  mtoto mwenye umri wa zaidi ya miaka miwili kufungiwa ndani na wazazi wake kwa kipindi cha miaka miwili sasa bila kutoka nje pamoja na kukosa matunzo muhimu hali ambayo imepelekea mtoto huyo kudhoofu kiafya.

Kutokana na kuguswa na tukio hilo Mtanzania huyo amelazimika kumtembelea Nyumbani anakoishia na kujionea hali halisi aliyonayo mtoto huyo kwa sasa.

Akizungumza kwa masikitiko nyumbani kwao eneo la Iyunga Mwakapusya amesema Wazazi wanaofanya vitendo kama hivyo wanapaswa kulaaniwa na kukemewa.

Mwakapusya aliyekuwa amefuatana na Mtoto wake wa Kiume David waliofunga safari kutoka Marekani hadi Mbeya kumwona Mtoto huyo wametoa zawadi mbali mbali zikiwemo Nguo na fedha taslimu alizokabidhiwa Mama mlezi pamoja na Balozi wa Nyumba kumi.

Mhanga wa tukio hilo, Joshua Joseph umri unao kadiriwa  kuwa ni kati ya miaka miwili au mitatu  ambaye alikutwa nyumbani hapo akiwa pekee yake huku wazazi wake wakiwa wameondoka kuelekea kwenye shughuli zao .

Balozi wa mtaa huo wa Ikuti Ndugu Aloni Mboya amesema kuwa hali hiyo imenza kujitokeza kwa kipindi cha miaka mitatu sasa hali ambayo imepelekea mtoto huyo kukumbwa na maradhi ya utapiamlo.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2011 mwezi wa tatu alipokea  taarifa kuhusiana na   suala hilo  ambapo baba wa mtoto huyo ndugu Joseph Simoni aliitwa katika ofisi za mtaakwa lengo la kumhoji juu ya malezi ya mtoto huyo.

Wakati huo huo Msamaria mwema huyo kutoka Nchini Marekani pia amezungumza na Mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi (albino) Amina Mwasankinga ambaye alifukuzwa Shule kwa kisingizio cha Ushirikina.

Aidha amemuahidi kumsaidia ili aweze kumaliza masomo yake huku akilaani vikali kitendo cha Walimu wa Shule ya Hollwood ya Wilayani Mbozi kuamini imani za Kishirikina na kumharibia masomo Mwanafunzi huyo.

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger