Na Ezekiel Kamanga, Kyela.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM)
Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kimeanza kuwajengea uwezo viongozi wake kuanzia
ngazi ya kitongoji, kijiji, matawi na Kata ili kusaidia utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi mkuu uliopita.
Akizungumza na Kituo hiki, Katibu
wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Kyela, Richard Kilumbo alisema
zoezi hilo lilianza mwezi machi na linatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu.
Alisema lengo la mafunzo kwa
viongozi wa matawi, vitongoji, vijiji na Kata wa Chama cha mapinduzi ni
kuwajengea uwezo juu ya namna ya kusaidiana na uongozi wa serikali katika
kutatua kero mbali mbali katika jamii pamoja na kusaidia utekelezaji wa ahadi
zilizotolewa kwenye uchaguzi mkuu 2015.
Alisema Wilaya hiyo yenye vitongoji
zaidi ya 300, vijiji 101 na Kata 37 itasaidia viongozi hao kuwa kiungo kizuri
kati ya Chama na Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa jamii.
“Lengo letu tunataka kuwe na
mahusiano mazuri baina ya wananchi, Serikali iliyopo madarakani na Chama
kuanzia ngazi ya chini ya tawi kwani hili litasaidia sana kusukuma gurudumu la
maendeleo ili kwendana na kasi ya Rais” alisema Katibu huyo.
Aliongeza kuwa endapo viongozi
hao watakuwa na maelewano mazuri na uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na
Madiwani waliopo itasaidia kuisimamia serikali katika utekelezaji wa miradi
mbali mbali katika maeneo yao.
Alisema mara nyingi viongozi wa
serikali hawana mahusiano mazuri na uongozi wa chama katika ngazi za chini
jambo linalosababisha kutokuwa na maendeleo pamoja na miradi mbali mbali
kukwama.
Katibu huyo alisema lengo linguine
la mafunzo hayo ambayo wahusika hufuatwa kwenye maeneo yao ni kuondoa makando
kando ya uchaguzi uliopita kwa kile alichodai bado kuna mgawanyiko baina ya
wanachama na viongozi.
“pia ikumbukwe kuwa katika
kipindi cha uchaguzi kulikuwa na matabaka ambayo sio kweli kuwa yameisha licha
ya kuhubiriwa kwenye majukwaa lakini tunachofanya sasa ni kuelezana madhara ya
mgawanyiko katika shughuli za maendeleo kwa jamii tunayoiongoza” alisema
Katibu.
0 comments:
Post a Comment