Pages


NDOA YAVUNJIKA RASMI WAVUTANA KURUDISHIANA FEDHA WALIZOPOKEA.

Chimbuko Letu | 15:10 | 0 comments
Bwana harusi akiwa na mpambe wake kanisani wakimsubiri bibi Harusi
Jamaa wameshika vichwa hali haieleweki


Bi Harusi Naomi Ngoje akiwa amejilalia chumbani akiwa anahuzunika na kushangaa wazazi wake kurudisha mahali ya mchumba wake



HABARI zilizotufikia hivi punde kutoka nyumbani kwa familia ya Bi harusi ambayo ilikuwa ikipinga ndoa isifungwe kutokana na Bwana harusi kushindwa kumalizia sehemu ya Mahari zinadai kuwa ndoa imevunjwa rasmi na kilichobaki ni mzozo wa kurudishiana fedha.

Pande hizo mbili ya Kiume na Kike zimengia kwenye Mzozo na kuvutana kuhusu fedha baada ya Wazazi wa Mwanamke kukubali kurudisha fedha hizo pamoja na vitu walivyopokea huku kikubwa kikiwa ni upande wa Mwanaume kudai wapewe papo hapo.

Vitu vinavyodaiwa ni Fedha taslimu takribani Shilingi 310,000/= ambazo zilitolewa kwa ajili ya Mkaja pamoja na kiingilio, Blanketi na Mashuka.

Kwa habari zaidi endelea kufuatilia mtandao wako huu ambapo mpaka sasa zaidi ya shilingi 50,ooo zimechangwa na ndugu wa Mume na kujaribu kuziwasilisha kwa ndugu wa Bibi harusi hata hivyo ndugu hao wamekataa kuzipokea.

Kwa habari zaidi Jumatatu endelea kufuatlia.

MAHARI YASABABISHA NDOA ISIFUNGWE , WAUMINI NA MCHUNGAJI WAKESHA KANISANI MBEYA

Chimbuko Letu | 14:10 | 0 comments
Bwana Harusi Fadhili Mahenge akiwa ndani ya Suti akisubiri kufungishwa ndoa 
Bi Harusi Naomi Ngoje akiwa amejilalia chumbani akisubiri hatima ya Wazazi ndipo ajiandae kwenda kanisani tayari kwa kufunga ndoa na mchumba wake waliodumu kwa miezi saba.
Bwana harusi akiwa na mpambe wake kanisani wakimsubiri bibi Harusi
Askofu Kenani Mpalala akiwa katika picha ya pomaja na Bwana Harusi na mpambe wake muda mfupi baada ya kuwasili kanisani
Askofu Keenan Mpalala wa kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania akionesha tangazo la Ndoa
Baadhi ya ndugu wa mwanamke wakiwa katika kikao na kuendelea na msimamo wao kuwa mahali lazima imalize ndipo wamtoe binti yao
Jamaa wameshika vichwa hali haieleweki


Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo Ndugu Benson Mbwana(aliyevalia shati rangi ya Zambarau) akionyesha ratiba ya sherehe.
Baadhi ya akina mama wakiangalia ratiba ya harusi
Kanisani
Baadhi ya waumini na majirani wakisubiri kanisani



KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Familia moja ya Makunguru  Mtaa wa Ilolo Jijini Mbeya imesababisha sintofahamu dhidi ya Familia nyingine baada ya kumkatalia binti yao kuolewa kwa madai ya waoaji kutokamilisha Mahari waliyokuwa wamepangiwa.

Tukio hilo la aina yake limetokea leo ambapo Bwana harusi aliyefahamika kwa jina la Fadhili Mahenge(28) Mkazi wa Songea aliyekuwa amuoe Naomi Ngoje na harusi yao kufungwa katika kanisa la Free Pentecoste Church Of Tanzania(FPCT) lililopo Makunguru Jijini hapa kushindwa kufungwa baada ya wazazi wa Bibi harusi kuzuia ndoa hiyo hadi Mahari itakapokamilika.

Wakizungumzia tukio hilo Nyumbani kwa Familia ya Bibi Harusi, Mjomba wa Bibi Harusi Dickson Ngoje amesema tatizo la wao kugomea ndoa hiyo ni kutaka waoaji kutimiza masharti waliokuwa wamekubaliana awali ambayo hadi siku ya mwisho familia hiyo haijatekeleza.

Amesema siku ya kwanza waoaji walifika Nyumbani kwa Mzee Ngoje na kujitambulisha ambapo walipangiwa taratibu za mahari kwa mujibu wa Mila kuwa watatakiwa kutoa Blanket 2, Mashuka mawili, Mkaja(200,000), mbuzi 4, Majembe 4, Ng’ombe Jike 2 na Ngo’mbe Dume 1 pamoja na fedha taslimu Shilingi Laki 3.

Amesema baada ya Familia hiyo ya Waoaji ambao ni Ukoo wa Mahenge kupangiwa vitu hivyo waliondoka na kuahidi kurudi siku nyingine kwa ajili kukamilisha vitu walivyopangiwa ambapo walirudi Septemba 11, Mwaka huu wakiongozwa na Mshenga aliyejulikana kwa jina moja la Mzee Katete wakiwa na Blanketi 2, Mashuka mawili pamoja na Fedha shilingi 10,000/= ambazo walizipokea na kuwaambia hawawezi kuzungumza chochote juu ya Ndoa.

Mjomba huyo anaongeza kuwa baada ya wiki mbili familia hiyo ilirudi na kukuta Nyumbani kuna ukoo mzima wakiwa na Shilingi 200,000/= ndipo walipoambiwa walipe kiingilio shilingi 100,000/= ndiyo wanaweza kupokelewa nyumbani jambo ambalo walilitekeleza kisha kulipa fedha walizokuwa nazo kama Mkaja na kuomba wapewe kibali cha kuandikisha ndoa na taratibu za kumalizia vilivyobaki zikiendelea.

Anasema tangu hapo Ndoa ilianza kutangazwa Disemba 8 na kuisha Disemba 22, Mwaka huu baada ya kutangazwa mara tatu huku tangazo likiashiria ndoa kufungwa tarehe 28/12/2013 ambapo wazazi wakiahidi kumalizia Mahari iliyobaki kabla ya siku ya kufunga ndoa.

Akizungumzia kwa kirefu kashishe hiyo, Mjomba huyo anasema baada ya wazazi wa Mwanaume kusisitiza kumaliza kila kitu hadi ifikapo Disemba 23, Mwaka huu na wao walijikusanya na kupanga taratibu za sherehe hususani ya kumwaga binti yao(Send Off) ambayo ilifanyika Disemba 24, Mwaka huu.

Aidha baadhi ya ndugu wameongeza kuwa familia hiyo haioneshi uaminifu wa kumalizia Mahari hiyo kutokana na ahadi zisizotekelezeka walizotoa tangu kipindi cha nyuma na kuongeza kuwa hata kwenye sherehe ya kumwaga binti yao walifika baadhi ya ndugu wakiwa na Zawadi tofauti na taratibu zinavyotaka.

Wamesema kwa mujibu wa taratibu za Sherehe za SendOff upande wa Mwanaume unatakiwa kuleta zawadi ambazo ni  nguo za Bibi Harusi za kuvaa siku ya Ndoa Pamoja n Harusi lakini wao hawakufanya hivyo ingawa walikuwa na Nguo ambazo tayari zilikuwa zimetumika.

Kwa upande wa Mchungaji aliyekuwa anataka kufingisha Ndoa hiyo ambaye pia ni Askofu wa Kanisa hilo, Mchungaji Kenan Mpalala alipoulizwa kuhusu hali hiyo amesema kwa mujibu wa taratibu za Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 8 pingamizi litolewe ndani ya siku 21.

Amesema upande wa Wazazi wa Mwanamke ulishindwa kuwasilisha pingamizi lao kanisani kabla ya Siku 21 badala yake walifika kutoa malalamiko kuhusu kutomaliziwa kwa mahali jambo ambalo alisema yeye kama Mwandikisha Ndoa halimhusu bali pande mbili wanatakiwa kulimaliza kabla ya Ndoa.

Naye Bwana Harusi Mtarajiwa Fadhili Mahenge(28) alipoulizwa kuhusiana na suala hilo huku akiwa tayari Kanisani kwa ajili ya Kufungishwa Ndoa alisema anachosubiri ni hatma ya Wazazi wa Mwanamke kama wanaweza kumwachia Mkewe iliwanachodai awe anamalizia taratibu.

Amesema yeye kama yeye kwa sasa hana fedha zozote za kuweza kumalizia anachodaiwa zaidi ya kuomba busara za wazazi wa Mwanamke kumruhusu Ndoa ifungwe ndipo aweze kulipa Mahari anayodaiwa kwa awamu kutokana na hali yake ya kiuchumi kuwa Mbaya.

Ameenda mbali zaidi kwa kusema kama Wazazi wa Mwanamke wataendelea kuwa na Msimamo huo basi hata yeye ataomba arudishiwe kile alichokitoa awali ili ajipange upya kwa ajili ya ndoa baada ya kukamilisha madai yao.



Hadi tunaingia mtamboni Mbeyayetu ambayo ilikuwepo sehemu ya tukio timu ya usuluhishi ilikuwa ikiendelea na kazi yake ikiongozwa na Mchungaji, Mwenyekiti wa Mtaa na Mzee Maarufu ambaye ni Katibu wa Chama cha Wakulima (TASO) kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ramadhani Kiboko, huku muafaka ukiwa haujapatikana.

Na EZEKIEL KAMANGA, MBEYA.

TCRA YAWAFUNDA WAANDAAJI WA VIPINDI NA WATANGAZAJI WA REDIO KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI.

Chimbuko Letu | 08:51 | 0 comments
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Tcra ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi, Magreth Mnyagi amesema lengo la washa hiyo ni kuwakumbusha watangazaji kuhusu kufuata maudhui yaliyokusudiwa yanayoelimisha na kuburudisha jamii na kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mgeni rasmi wa Washa hiyo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya, Leonard Magacha ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amesema kukiuka kwa maadili katika baadhi ya vituo vya utangazaji kunatokana na wamiliki kuwaajiri wafanyakazi wasiokuwa na taaluma ya Utangazaji.




Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) Kanda ya Mbeya MhandisDeogratius Moyo wana warsha kuchangia mada

Frederick  Ntobi Naibu Mkurugenzi idara ya utangazaji Mamlaka ya mawasiliano akiwafunda waandaaji wa vipindi  na watangazaji wa radio kanda ya nyanda za juu kusini


Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy akiongoza mijadala katika Warsha ya Siku Mbili kwa kwa waandaaji wa vipindi na watangazaji wa Radio



Baadhi ya watangazaji wakichangia mada


Picha ya pamoja



MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) inaendesha warsha ya Siku mbili kwa Wandaaji wa Vipindi vya Redio pamoja na watangazaji kutoka Mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa uliopo Sokomatola Jijini Mbeya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Tcra ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi, Magreth Mnyagi amesema lengo la washa hiyo ni kuwakumbusha watangazaji kuhusu kufuata maudhui yaliyokusudiwa yanayoelimisha na kuburudisha jamii na kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema vipo vituo vingi ambavyo vimekiuka maudhui yaliyokusudiwa ambayo hayazingatii maadili ya Tanzania na kupelekea uvunjifu wa amani kutokana na kutangaza vitu vinavyokiuka maudhui waliyopewa, hivyo kupitia Washa hiyo itasaidia kuwakumbusha kufuata misingi taratibu na kanuni za utangazaji.

Kwa upande wake Mgeni rasmi wa Washa hiyo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya, Leonard Magacha ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amesema kukiuka kwa maadili katika baadhi ya vituo vya utangazaji kunatokana na wamiliki kuwaajiri wafanyakazi wasiokuwa na taaluma ya Utangazaji.

Magacha amesema shida iliyopo ni kwa wamiliki wa Vyombo vya habari ambao huajiri watu wasiokuwa na taaluma kwa kuogopa kulipa hivyo kutafuta watangazaji wa kuokoteza ambao ndiyo chanzo cha kukiuka Maudhui.

Aidha katika Washa hiyo washiriki waliweza kufundishwa kuhusu Masharti na sheria ya Leseni( Licence conditions and Code of Conduct), Kanuni za Utangazaji pamoja na kutazama DVD mbali mbali zenye makosa kwenye vipindi vya baadhi ya Televisheni na Redio ambapo washiriki walipata muda wa kujadili.

Na Mbeya yetu

WAWILI WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA MKOANI MBEYA

Chimbuko Letu | 05:16 | 0 comments
 Watuhumiwa wawili wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, Kelvin Myovela(kushoto), aliyehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na David Mwasipasa(Kulia) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya.
Mhukumiwa namba moja wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Hakimu Mwakalinga(kushoto) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa na mwenyeshati la Bluu ni Obote Mwanyingili amehukumiwa miaka saba jela kwa kumhifadhi mtuhumiwa.(Picha na Ezekiel Kamanga, Mbeya)

Na  Ezekiel Kamanga, Mbeya
WATUHUMIWA wawili kati ya wanne  wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya.


Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya iliyokuwa ikiendesha vikao vyake katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe chini ya Jaji Samweli Karua, baada ya kuahirishwa kutolewa kwa hukumu hiyo kwa zaidi ya mara tatu na kuzua hali ya sintofahamu kwa ndugu wa washtakiwa na wafuatiliaji wa kesi hiyo.


Awali kabla ya kusoma kwa hukumu hiyo Mwendesha mashtaka wa Serikali., Archiles Mulisa, aliwataja watuhumiwa wote wanne kuwa ni Hakimu Mwakalinga, Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili na Kelvin Myovela wanaokabiliwa na tuhuma za kumuua kwa maksudi aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe John Mwankenja.


 

Alisema watuhumiwa hao wenye kesi namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

 

Mulisa aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali Lugano Mwakilasa kwa upande wa mashtaka huku  Watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili ambao ni Victor Mkumbe na Simon Mwakolo. 


Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa kesi inayowakabili  watuhumiwa hao walilitenda Mei 19,2011 kwa kumuua kwa maksudi John Mwankenja kinyume na kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.


Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua ambaye alianza majira ya saa 14:37 mchana na kukamilisha saa 15:37 alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka na utetezi haubishaniwi kuhusu kifo cha marehemu.


Aliongeza kuwa pande hizo mbili pia hazibishaniwi kuhusu ripoti za kitaalamu na dhamira za mauaji hayo bali kinachobishaniwa ni uhusika wa watuhumiwa hao dhidi ya mauaji hayo.


Alisema katika kutetea hoja zao upande wa mashtaka ulileta mashahidi 11 ambao wote kwa pamoja  wakiongozwa na shahidi namba moja waliwatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.


Shahidi huyo namba moja Weston Jacob(17) mkazi wa Kiwira Mwanafunzi kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari Kipoke ambaye pia ni Mjomba wa marehemu ambaye aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio akiwa nyumbani akijisomea majira ya 2: 30 usiku ambapo marehemu alifika nyumbani na kupiga honi ya gari akitaka afunguliwe mlango.



Mbali na ushahidi huo Jaji Karua alisema pamoja na ushauri wa wazee wa baraza la mahakama ambao pia wanawatuhumu washtakiwa hao kuhusika na tukio hilo nae anakubaliana nao lakini siyo kwa watuhumiwa wote.


Kutokana na ushahidi huo alisema Mshtakiwa namba moja na namba mbili ambao ni Hakimu Mwakalinga na Daudi Mwasipasa wanatiwa hatiani kuhusika moja kwa moja na mauaji kutokana na ukiri wao kwa mlinzi wa amani, Mchukua maelezo na  vipimo vya vinasaba.


Alisema Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye anatiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji hivyo yeye hausiki moja kwa moja na kosa hilo.


Jaji karua alisema kwa upande wa mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela anatiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika nkatika mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja.


Aliongeza kuwa kutokana na kifungu cha sheria cha mwenendo wa makosa ya jinai kifungu namba 300 na 217 washtakiwa namba tatu na namba nne wanatiwa hatiani na mahakama.


Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa, aliiambia mahakama hiyo kwamba itoe adhabu kali kutokana na kitendo alichofanyiwa marehemu na iwe fundisho kwa watu wengine.


Kwa upande wa utetezi ambao siku ya hukumu uliwakilishwa na Wakili Merick Luvinga alisema mahakama iwanee huruma washtakiwa kwa kuwa wote umri wao ni mdogo wanaweza kujifunza na kurudi kuungana na jamii pia ni kosa lao la kwanza hivyo wasipewe adhabu kali.


Kutokana na utetezi huo, Jaji Karua alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuthibitisha kuhusika pasipo shaka kwa washtakiwa namba moja na namba mbili hivyo adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.


Aliongeza kuwa Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili anayehusika kumhifadhi mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka saba kwa kosa hilo sambamba na mshtakiwa namba nne  Kelvin Myovela aliyehifadhi silaha iliyotumika kwenye mauaji.


Alisema kutokana kosa hilo mtuhumiwa huyo atatumikia kifungo jela miaka saba ingawa pia tayari alikuwa amehukumiwa kifungo jela cha miaka 20 kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.

MTU MMOJA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 35 JELA MKOANI MBEYA

Chimbuko Letu | 05:03 | 0 comments


 Mtuhumiwa Baraka Mwandibwa(kulia) ambaye amehukumiwa miaka 35 kwenda jela kwa kosa la mauaji.(Picha na Ezekiel Kamanga, Mbeya)

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
MAHAKAMA kuu kanda ya Mbeya imemhukumu Baraka Mwandibwa kwenda jela miaka 35 mtuhumiwa wa mauaji dhidi ya watoto huku mwingine akiachiwa huru baada ya kukutwa bila hatia.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Mbeya Samweli Karua mbele ya mwendesha mashtaka wa serikali Archiles Mulisa katika vikao vilivyofanyika katika Mahakama ya wilaya ya Rungwe.

Awali mwendesha mashtaka wa serikali Archiles Mulisa aliiambia mahakama kuwa washtakiwa Baraka Mwandibwa na Zuberi Lwila walifikishwa mahakamani hapo wa kosa la kumlawiti na kumuua mtoto Esta James(5) Novemba 21, 2010.

Alisema kosa hilo ni kinyume cha sheria kifungu cha 196 (16) kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambalo walilifanya katika kijiji cha Bulyaga Wilayani Rungwe baada ya kumteka mtoto huyo.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua alisema Mshtakiwa namba moja anatiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ambao ulitoka kwa shahidi namba moja ambaye ni mtoto aliyejulikana kwa jina la Marietha.

Alisema mtoto huyo ambaye alisema siku ya tukio alikuwa akicheza na marehemu ambapo mtuhumiwa alifika na kumpa pipi aina ya Ivory marehemu kisha kuondoka naye ambapo shahidi huyo aliwerza kumtambua mtuhumiwa katika gwaride la utambuzi.

Mbali na hilo alisema ushahidi mwingine ni ushaidi wa Vinasaba ambao unawahusisha moja kwa moja watuhumiwa wote wawili ikiwa ni pamoja na ushaidi wa kimazingira unaomhusisha mtuhumiwa wa kwanza.

Alisema kutokana na ushahidi huo Mtuhumiwa wa kwanza anahusika moja kwa moja na mahakama inamtia hatiani ingwa kwa mujibu wa ushahidi hakuua kwa makusudi kutokana na kutokuwa na vifaa vya mauaji kama visu panga na silaha zingine.

Alisema katika mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa unadamu na mbegu za kiume sehemu zake za siri na hakuwa amejeruhiwa nsehemu yoyote, hivyo mahakama iliona mtuhumiwa hakuua kwa kukusudia bali ilikuwa ni bahati mbaya.

Hata hivyo upande wa Mshtaka uliomba mahakama itoe adhabu kubwa na kali dhidi ya washtakiwa kutokana na mazingira aliyofanyiwa mtoto huyo ili iwe fundisho kwa wanaume wengine wenye tabia za kuwalaghai watoto wadogo.

Akitoa hukumu hiyo Jaji karua alisema anakubaliana na ushauri wa upande wa mashtaka kwamba tukio hilo ni kubwa na mstakiwa wa kwanza Baraka Mwandibwa ataenda jela kwa miaka 35 huku mshtakiwa wa pili Zuberi Lwila akiachiwa huru baada ya kutokuwa na ushahidi wa kuhusika katika tukio hilo.
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger