Tuzo ya mwalimu bora duniani yazinduliwa

Chimbuko Letu | 23:17 | 0 comments


Mwenyekiti wa Wakfu huo Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.
Baadhi ya walimu jijini Mbeya  wameipokea kwa mtazamo tofauti  juu ya kuzinduliwa kwa tuzo ya mwalimu duniani, atakaye thibitisha kuwa mchango wake kwa jamii umekuwa bora zaidi na kujishindia shilingi bilioni 1 na milioni 650.KWA HABARI KAMILI INALETWA KWAKO NA GREYSON SALUFU...... Bofya hapa chini kwa habari kamili.

WANYANYASAJI WA WATOTO WAANZA KUCHUKULIWA HATUA MKOANI MBEYA.

Chimbuko Letu | 07:40 | 0 commentsJESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja Mwanahawa Nasoro(32) Mkazi wa Mtaa wa Airport Kata ya Iyela Jijini Mbeya akituhumiwa kumfanyia vitendo vya unyanyasasaji Mtoto wa ndugu yake.
 
Mwanamke huyo anatuhumiwa kumtesa, mtoto John Msumba(3) ambaye ni Shangazi yake baada ya kumfungia ndani kumnyima chakula na kumpa kipigo kikali kilichompelekea kuwa na majeraha mwilini mwake pamoja na maumivu makali yaliyosabisha kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu zaidi.
 
Akizungumza na Mtandao huu, Mjumbe wa Mtaa wa Airport, Rehema Mohammed alisema kuteswa na kukamatwa kwa Mwanamke huyo kuligundulika Machi 12, Mwaka huu majira ya saa nne asubuhi kufuatia kuwepo kwa msiba jirani na nyumba yake.
 
Alisema wakati watu wako msibani na mlango wa nyumba ya Mwanamke huyo ukiwa umefungwa na kufuli kwa nje ilisikika sauti ya Mtoto akilia ndani jambo ambalo liliwashangaza wengi ndipo alipotoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa Enock Mwampagama ambaye pia alitoa taarifa kwa Mtendaji wa Mtaa aliyelitaarifu Jeshi la Polisi.
 
Alisema baada ya Mwanamke huyo kubanwa alikiri kuwepo kwa Mtoto ndani na kwamba alikuwa akimfanyia hivyo kutokana na tabia yake ya kujisaidia haja kubwa hovyo hali iliyokuwa imemchosha na kuamua kumpa adhabu kama hiyo.
 
Alipoulizwa kuhusiana na wazazi wa Mtoto huyo alidai kuwa hafahamu mahali alipo mama mzazi na kuongeza kuwa baba yake aliyefahamika kwa jina la Sumba Dinda kuwa yupo machimboni Wilayani Chunya kwenye Migodi ya Dhahabu.
 
Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa Mwanamke huyo anashikiliwa hadi hapo Afya ya mtoto ambaye ni mhanga wa Tukio hilo itakapoimarika ndipo atakapofikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
 
Wakati huo huo baadhi ya Wasamaria wema wameziomba taasisi zinazoshughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto zikiwemo Mtandao wa Waandishi wa habari Wanawake na Jinsia (TAMWA) na Taasisi ya Jinsia (TGNP) kuingilia kati maswala hayo ili kukomesha vitendo hivyo katika jamii.
 
Aidha baadhi ya wasamaria wema wajitokeza kuchangia fedha za matibabu ya mtoto huyo yanayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya baada ya mmoja wa Waandishi wa Mtandao huu ambaye pia ni Mtangazaji wa Kituo cha Redio cha Bomba cha Jijini Mbeya kuendesha harambee fupi katika kipindi chake na kufanikiwa kukusanya shilingi 35,000/= zilizotumika kununulia madawa.
 
Mbali na hilo TAMWA inaombwa kushughulika moja kwa moja na mtoto huyo ili kuhakikisha haki inapatikana ikiwa ni pamoja na kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia uliokithiri ndani ya jamii kutokana na juhudi ziliooneshwa na mtandao huo katika kukabiliana na hali hiyo kwa kutoa Elimu kwa wanahabari mara kwa mara katika kuibua vitendo hivyo na kuvikemea.


Na Ezekiel Kamanga.

WATOTO WAWILI KATI YA MAPACHA WANNE WAMEFARIKI DUNIA, RAMBIRAMBI KUTOKA USWISI ZAPOKELEWA KIJIJINI KWAO.

Chimbuko Letu | 07:26 | 0 comments

Jeneza likiwa na mwili wa Marehemu tayari kwa Ibada ya Mazishi iliyofanyikia Nyumbani kwao Chiwanda.

Mchungaji wa Kanisa la Africa Mission Church wanakosali wazazi wa Marehemu akiongoza ibada ya Mazishi.

baadhi ya Waombolezaji wakielekea Makaburini.

Joseph Mwaisango akiwa amebeba Jeneza lenye mwili ya marehemu kuelekea Makaburini tayari kwa safari ya mwisho


Mchungaji akisoma neno la Mungu kutoka kwenye Biblia lenye ujumbe kwa Waombolezaji na wafiwa ambapo alisema hata kama alikuwa ni mtoto mchanga alikuwa akivuta pumzi kama sisi hivyo naye amepaswa kupewa heshima zote kama binadamu.

Mwili wa Marehemu ukishushwa kaburini.

Kaburi likifukiwa baada kukamilika kwa taratibu zote ambapo mwili wa marehemu ulizikwa katika makaburi ya Kijiji wanakozikwa Wananchi wengine.

Kwa mujibu wa mila za kabila la Wanyamwanga vijana hawa walikuwa wakisiliba kaburi baada ya kumaliza mazishi.

Ezekiel Richard Kamanga ambaye ni mwandishi wa Habari kutoka redio ya Bomba fm ya Jijini Mbeya akizungumza machache kwa wafiwa na wanakijiji kwa niaba ya Wanahabari wenzao ambao hawapo pichani Venance Matinya wa gazeti la JamboLeo na Joseph Mwaisango wa mbeya yetu blog
KATIKA hali ya kusikitisha Watoto wawili kati ya Wanne ambao ni mapacha waliozaliwa kwa pamoja na mwanamke Aida Nakawala Mkazi wa Kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Nimonia.

Watoto hao wamefariki kwa mida tofauti ambapo Mtoto wa Kwanza alifariki Nyumbani kwao baada ya kuugua ghafla ndipo hali za wengine zilipoanza kutia shaka na kulazimu Waandishi wa Habari wa Mtandao wa Mbeya Yetu, Gazeti la Jambo Leo na Redio ya Bomba Fm waliohudhuria mazishi ya Mtoto huyo kulazimika kuwakimbiza katika Hospitali ya Wazazi Meta kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo baada ya kupokelewa kwa watoto hao Watatu mtoto mmoja aliaga dunia baada ya kuchelewa kupata matibabu kutokana na kubanwa na kifua na kusababisha kushindwa kupumua vizuri.

Hali za watoto wawili waliobaki wanaendelea vizuri na matibabu na kwa mujibu wa Daktari anayewatibu amesema taratibu za Hospitali hiyo ni kupokea watoto waliochini ya Miezi miwili lakini hao wamezidi umri huo hivyo badala ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya wataendelea kuwepo Meta hadi hapo hali zao zitakapoimarika.

Baadhi ya wananchi na wauguzi katika Hospitali ya Wazazi Meta wamesema sababu ya watoto hao kuugua ni kutokana na  kukosekana kwa uangalifu wa karibu katika malezi ya watoto hao ukilinganisha na maisha ya vijijini kukosa watu wenye uelewa wa afya za watoto.

Wengine wameitupia lawama moja kwa moja Serikali kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka tangu watoto walipozaliwa ili kujiridhisha na mazingira wanayopaswa watoto hao kuishi kwa kuwapatia msaada wa karibu na ushauri wa kitaalamu.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, Thobias Mwalwego, alikiri kuwepo kwa urasimu katika Idara yao kwa madai kuwa tangu watoto hao walipokuwa wamezaliwa walipata taarifa na kuchukua hatua kwa afisa mmoja kufika kijijini na kuchukua picha zao.

Alisema urasimu unakuja kutokana na Ofisi ya Wilaya na Mkoa kukosa fungu la dharula ambapo barua za maombi zote hupelekwa makao makuu kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii ambapo Ofisi yake huchukua muda mrefu kurudisha majibu kutokana na waombaji kuwa wengi.

Alisema kila ofisi katika Ngazi ya Mkoa ingekuwa na fungu la Dharula kama ilivyo katika Ofisi zingine hali ambayo ingeweza kusaidia kuepusha vifo vya watoto hao kutokana na kupatiwa msaada wa ushauri na makazi rafiki kwa malezi ya mapacha wanaozidi wawili.

Aidha alishauri kila Halmashauri Nchini kutenga bajeti za kusaidia majanga kama hayo na vitu vya dharula wakati Serikali inajipanga kutekeleza kutokana na taratibu zake kuchukua muda mrefu ili kuweza kukabiliana na hali yoyote na muda muafaka.
 Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Ahmed Issa katikati na Joseph Mwaisango wa Mbeya yetu Blog wakimkabidhi Aida Nakawala msaada wa pesa kiasi cha shilingi laki tano 500,000/ toka wa watanzania waishio nchini Uswisi

Baadhi ya watumishi wa  Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu kusini wakiwa wamewabeba watoto hao

Joseph Mwaisango alipokwenda kuwatembelea Hospitali ya wazazi Meta watoto wawili waliobakia na hali zao kwa sasa zinaendelea vizuri
Wakati huo huo Umoja wa  Watanzania waishio nchini Uswisi (TAS) wametoa msaada wa Fedha taslimu shilingi Laki tano(500,000/=) kwa mama Aida Nakawala kwa ajili ya kusaidia kulea watoto wengine waliobaki.

Akikabidhi msaada huyo kwa mama huyo kijijini kwao Chiwanda Wilayani Momba, Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Ahmed Issa kwa niaba ya Watanzania hao alisema wameguswa sana na hali hiyo na kuahidi kuendelea kuchangia kila mara.

Aidha alisifu utendaji kazi wa Waandishi wa Habari hususani Mbeya yetu Blogwaliofanikisha kuibua jambo hilo na kulitolea taarifa kila wakati jambo lililosaidia kufahamisha watu wengi wakiwemo wanaoishi nje ya Tanzania na kutuma kile wanachokuwa wameguswa nacho.

Mbali na Hilo, Meneja wa TMA Kanda ya Mbeya, Ahmed Issa, pia amejitolea kuusafirisha mwili wa Marehemu kutoka Hospitali ya Meta Mbeya hadi Kijijini kwao Chiwanda Wilayani Momba kwa ajili ya taratibu za Mazishi.

BARAZA la Ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra ccc) lazinduliwa Mbeya.

Chimbuko Letu | 07:25 | 0 comments
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Michael Kadeghe, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, wakati akizindua Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri wa nchi kavu na majini Mkoa wa Mbeya, katika hafla iliyofanyika jana katika ukumbi wa Haoteli ya Mtenda Sunset iliyopo Soweto Jijini hapa.


Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Taifa, Oscar Kikoyo alisema katika kuondoa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike kurubuniwa na madereva kutokana na kupewa misaada katika magari yao Baraza   limeanza kuunda Vilabu vya Mabaraza katika mashule kwa lengo la kutoa elimu.
Saidi Madudu ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa baraza hilo akipokea kitambulisho toka kwa mgeni rasmi

Katibu wa baraza hilo  Brandy Nelson akipokea kitambulisho toka kwa mgeni rasmi

Saidi Madudu ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa baraza hilo 


Picha ya pamojaBARAZA la Ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra ccc) limetakiwa kubuni njia mbadala itakayosaidia kuondoa changamoto ya usafiri kwa wanafunzi pindi wanapoenda na kutoka mashuleni.

Mwito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Michael Kadeghe, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, wakati akizindua Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za usafiri wa nchi kavu na majini Mkoa wa Mbeya, katika hafla iliyofanyika jana katika ukumbi wa Haoteli ya Mtenda Sunset iliyopo Soweto Jijini hapa.

Kadeghe alisema hivi sasa kuna changamoto ya usafiri kwa wanafunzi nchi nzima hali inayosababisha wanafunzi kuhangaika kutafuta usafiri wa kuwarudishwa makwao kutokana na asilimia kubwa kutoka mbali na shule ziliko hivyo kuwaletea usumbufu na kushundwa kuelewa vizuri masomo yao.

Alisema kama baraza litaishauri vizuri Serikali kuona inasaidia vipi katika kutatua changamoto hiyo ili kuwa na usafiri maalumu kwa wanafunzi  wa shule za kawaida ili kuwawezesha kuondokana na usumbufu unaojitokeza na kusababisha Wanafunzi kurubuniwa na baadhi ya madereva wanaowapa lifti.

Alisema hivi sasa wanafunzi wanarubuniwa sana na baadhi ya madereva ambao siyo waaminifu ambapo huwapa msaada wa usafiri kutokana na wanafunzi hao kusimamisha kila gari kutokana na magari mengi ya abiria kuwakataa wanafunzi kwa madai kuwa wanapata hasara  kwa kuwajaza kwenye gari moja.

Aidha alitoa wito kwa baraza hilo kushirikiana bega kwa began a Serikali pamoja na taasisi zingine ili kutatua kero mbali mbali za wananchi kuhusiana na usafiri ambapo aliongeza kuwa magari mengi ni chakavu na bado yanaendelea kutoa huduma pamoja na mwendo kasi unaosababishwa na baadhi ya abiria kumchochea Dereva kuongeza mwendo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Taifa, Oscar Kikoyo alisema katika kuondoa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike kurubuniwa na madereva kutokana na kupewa misaada katika magari yao Baraza   limeanza kuunda Vilabu vya Mabaraza katika mashule kwa lengo la kutoa elimu.

Aliongeza kuwa kazi ya Baraza siyo kukamata magari yanayofanya kinyume na taratibu za usalama barabarani bali kazi yao ni kushauri na kutoa elimu kwa wasafiri juu ya haki zao ili serikali kupitia vyombo vyake iweze kuchukua hatua.

Alisema Mkoa wa Mbeya ni wa Saba kuzindua Baraza hilo ambapo baada ya kuzinduliwa rasmi wataanza kazi kwa kuwasilisha na kupokea maoni ya watumiaji wa usafiri, kupokea na kusambaza maoni na taarifa juu ya haki za watumiaji wa sekta ya usafiri, kushauriana na wadau kuhusu upatikanaji wa huduma bora na kuunda kamati za kushauriana nazo.

Baraza la Mkoa wa Mbeya lilizinduliwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Michael Kadeghe na kuwakabidhi vitambulisho wajumbe Watano wanaounda baraza hilo ambao ni Saidi Madudu ambaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti, Katibu Brandy Nelson na wajumbe wakiwa ni Jimmy Ambilikile,  Rosta Kihwani na Oswald Ngulangwa.

Naye katibu wa Baraza hilo Mkoa wa Mbeya, Brandy Nelson ametoa wito kwa wadau wa usafiri Mkoa wa Mbeya kutoa ushirikiano na baraza ili liweze kufikia malengo waliyowekewa kwa kuwasaidia kutoa taarifa na maoni juu ya namna ya uboreshaji wa sekta ya Usafiri Mkoani Mbeya.

UMOJA WA MADEREVA WA MABASI TANZANIA (UWAMATA) KANDA YA MBEYA WAMELALAMIKIA JESHI LA POLISI KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI NA MAMLAKA YA UDHIBITI WA NCHI KAVU NA MAJINI(SUMATRA) MKOA WA MBEYA KWA KUWANYANYASA WAWAPO KAZINI.

Chimbuko Letu | 07:22 | 0 comments
Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala, alisema amepokea malalamiko yao na kwamba Jeshi la Polisi litakutana na Askari wanaolalamikiwa hasa wa Wilaya ya Rungwe na amemwagiza Mkuu wa usalama Barabarani kurekebisha kasoro zote ili kila upande ufanye kazi kwa amani.


Mkuu wa Usalama Barabarani, Butusyo Mwambelo, alikanusha kuwafukuza madereva ofisini kwake bali alidai kuwa viongozi wanatetea wahalifu hali hiyo isipodhibitiwa itasababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.


Ofisa Mfawidhi wa SUMATARA kanda, Amani Shamaje, 
Mwenyekiti wa Madereva kanda ya Mbeya, Damas Mwandumbya, katika mkutano baina yao na viongozi  uliofanyika katika ukumbi wa Miami uliopo  Ilomba Jijini Mbeya


Mwandumbya akisoma risala yao kwa mgeni rasmi
Baadhi ya viongozi wa madereva toka wilaya zote za mkoa wa Mbeya walihudhuria kikao hicho

Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA) kanda ya Mbeya wamelalamikia Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya udhibiti wa nchi kavu na Majini(SUMATRA) Mkoa wa Mbeya kwa kuwanyanyasa wawapo kazini.

Malalamiko yao yalitolewa jana na Mwenyekiti wa Madereva kanda ya Mbeya, Damas Mwandumbya, katika mkutano baina yao na viongozi  uliofanyika katika ukumbi wa Miami uliopo  Ilomba Jijini Mbeya mbele ya Mgeni rasmi Kaimu Kamanda wa  Polisi Mkoa Robert Mayala ambaye piani  Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya.


Mwandumbya akisoma risala yao kwa mgeni rasmi alisema wanaotuhumiwa kula rushwa ni pamoja na Askari Polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani wa Wilaya za Rungwe na Mbeya ambao waliwataja kuwa ni   Jane,Vaileth, Shabani, Denis, Hezron na Azimio pamoja na Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo, ambaye imedaiwa kuwapa malengo Askari wake ili mgao afikishiwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.


Aliongeza kuwa Mgao mwingine wa pesa hizo umetajwa kwenda kwa Mkuu wa Usalama Barabarani nchini na kila Dereva anapokamatwa au kusimamishwa hulazimika kutoa shilingi elfu tano katika kila kituo anachosimamishwa ndipo gari huendelea na safari.


Alisema hali hiyo husababisha Madereva kujaza abiria kupita kiasi  ili kukidhi malengo ya waajiri na kumudu kulipa Askari wa Usalama Barabarani na kama wasipotoa hukamatwa na kutozwa faini au kupelekwa mahabusu hali inayowafanya kufanya kazi katika mazingira magumu.


Aidha Madereva hao walimtuhumu Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa Mbeya kwa kuwafukuza ofisini kwake na kuwa na lugha chafu inayowadhalilisha madereva hali inayopelekea kugoma au kutishia kugoma kutokana na kauli za kiongozi huyo kwa lengo la kushinikiza kuondolewa Mkoani Mbeya.


Mbali ya shutuma hizo kwa Jeshi la Polisi pia Madereva hao walitupia lawama SUMATRA  kwa kuruhusu magari ya aina ya Noah ambayo yameanza kusafirisha abiria bila kukidhi vigezo hali inayosababisha baadhi ya magari ya abiria aina ya Hiace kushindwa kufanya kazi kutokana na magari hayo kufanya kazi kiholela huku Jeshi la Polisi na SUMATRA wakifumbia macho.


Akijibu risala yao ambayo ilijaa tuhuma, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya Robert Mayala aliwapa fursa wanaotuhumiwa kujieleza mbele ya mkutano huo uliojumuisha madereva ili kujiridhisha na majibu.


Mkuu wa Usalama Barabarani, Butusyo Mwambelo, alikanusha kuwafukuza madereva ofisini kwake bali alidai kuwa viongozi wanatetea wahalifu hali hiyo isipodhibitiwa itasababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Aidha alikiri kupokea changamoto na mapungufu aliyoelezwa na madereva hayo kwa madai kuwa atayafanyia kazi na yeye mwenyewe atajirekebisha ili kuendelea kudumisha hali ya usalama barabarani pamoja na abiria.


Kwa upande wake Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala, alisema amepokea malalamiko yao na kwamba Jeshi la Polisi litakutana na Askari wanaolalamikiwa hasa wa Wilaya ya Rungwe na amemwagiza Mkuu wa usalama Barabarani kurekebisha kasoro zote ili kila upande ufanye kazi kwa amani.


Alihitimisha kwa kuwataka Madereva kutii sheria bila shuruti ili kuepusha ajali na kuwataka madereva wakatae kutoa rushwa na Askari atakaye walazimisha watoe taarifa kwake kwa hatua zaidi.

Na Ezekiel Kamanga
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger