Rais Dk Magufuli amteua Dk Kikwete kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM.

Chimbuko Letu | 14:16 | 0 comments
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli amemteua Rais mstaafu wa awamu ya Nne Dk Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
 Taarifa kamili ya Uteuzi wake.

Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wanaokabiliwa na kesi namba 1/2014 ya uhujumu uchumi wameanza utetezi wao

Chimbuko Letu | 14:12 | 0 comments


Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wanaokabiliwa na kesi namba 1/2014 ya uhujumu uchumi wameanza utetezi wao mbele ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa  wa Mbeya Rashid Chaungu.

Watumishi hao ni pamoja na Martin Bakalaza ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri,Upendo Atu Sanga Mkurugenzi wa Halmashauri,Afidh Mgagi Mweka Hazina wa Halmashauri,Abiud Fungamtama Afisa Elimu Vifaa na Marther Mgata Afisa Elimu Taaluma ambao kwa pamoja  wanatuhumiwa kwa makosa manane ya kujipatia shilingi 4,750,000/= kwa kutumia madaraka yao vibaya.

Mbele ya Mahakama Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU Nimrod Mafwele aliiambia Mahakama kuwa kwa pamoja wakitumia madaraka ambapo walijipatia kiasi hicho cha fedha kwa kutumia nyaraka mbalimbali mnamo Novemba 6 mwaka 2012 kwa madai ya kuendeshea semina ya wasimamizi wa mtihani wa kidato cha pili na gharama za mafuta kwa ajili ya kusambazia mitihani katika Wilaya ya Mbeya.

Walioanza kujitetea wakiongozwa na Wakili Nguli wa kujitegemea Mika Thadayo Mbise ni Martin Bakalaza,Upendo Sanga na Afidh Mgagi ambapo Mshitakiwa wa kwanza Martin Bakalaza ameiambia Mahakama kuwa yeye alipata maagizo kutoka kwa Viongozi wake kuwa akope pesa kwa ajili ya kufanikisha mitihani kwa kuwa pesa za mitihani zilichelewa kufika kwa wakati.

Bakalaza ameiambia Mahakama kuwa baada ya agizo hilo alikopa pesa taslimu shilingi 4,750,000/=kutoka kwa Mlipa Fedha Sevelina Mwaifwani na kulipa chakula na mafuta kisha kukabidhiwa stakabadhi za malipo katika maeneo husika.

Alipoulizwa na Wakili wa TAKUKURU kwamba taratibu zote zilifuatwa Bakalaza alidai kuwa taratibu zilifuatwa na pesa alizirejesha kwa Sevelina kama alivyokopa awali.

Mshitakiwa wa Pili Upendo Sanga ameiambia Mahakama kuwa yeye kama Mkurugenzi alitoa kibali kwa Bakalaza ili kuazima fedha hizo ili kufanikisha shughuli ya kitaifa hivyo alitimiza wajibu wake ili kutokwamisha zoezi la mitihani kwani fedha za mitihani zitumwa kwenye akaunti ya  shughuli za maendeleo.

Mweka Hazina Afidh Mgagi aliwasilisha utetezi wake mbele ya Mahakama kuwa kama Mweka Hazina aliruhusu fedha hizo zikopwe kokote ili kufanikisha mitihani ya kidato cha pili baada ya kupokea fedha za mitihani katika akaunti tofauti hivyo kama taratibu za fedha zingefuatwa mitihani isingeweza kufanyika hivyo Bakalaza alikuwa sahihi kukopa pesa hizo na alirejesha kwa njia ya masurufu.

Mgagi akiongozwa na Wakili Mbise aliomba Mahakama ipokee vielelezo vya Benki pamoja na Vibali vya kuomba fedha kutoka ofisi ya fedha kama ushahidi na utetezi wake Mahakamani jambo ambalo lilipingwa na Mwendesha Mahitaka Nimrod Mafwele.

Jambo hilo lilizua mabishano ya kisheria kuwa vielelezo vipokelewe au la hali iliyopelekea Mafwele kuomba kuahirisha kesi wakati Afidh akijitetea ambapo Hakimu alipinga hali iliyomfanya Hakimu Chaungu kuahirisha kesi kwa muda ili Mafwele atafakari uamuzi wake.

Mahakama iliendelea kusikiliza utetezi wa Afidh na baadae kupokea vielelezo hivyo kama uetezi wake na pande zote ziliridhia vitumike kama utetezi wake katika kesi hiyo.

Kwa pamoja Watuhumiwa wote watatu waliiomba Mahakama iwaondolee mashitaka yanayowakabili kwa kuwa walikuwa wanatimiza wajibu wao na kwamba hawajamsababishia hasara mwajiri wao kama mashitaka yanavyodai.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 26 mwaka huo wakati Abiud Fungamtama na Marther Mgata watapowasilisha utetezi wao mbele ya Mahakama na dhamana kwa washitakiwa inaendelea.

Mganga maarufu wa jadi aliyefamika kwa jina la Shija Ndula Jinan’gai kuamua kusalimisha matunguli yake katika Kanisa la Nyumba ya Maombi(House of Prayer Shield of faith) Pambogo Kata ya Iyela jijini Mbeya.

Chimbuko Letu | 08:21 | 0 comments


Mganga maarufu wa jadi aliyefamika kwa jina la Shija Ndula Jinan’gai(35)mkazi wa Mapogolo Kata ya Madibira Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ameachana na kazi hiyo na kuamua kusalimisha matunguli yake katika Kanisa la Nyumba ya Maombi(House of Prayer Shield of faith) Pambogo Kata ya Iyela jijini Mbeya.


Shija Ndula mwenye familia ya Mke na watoto wanne ambaye sasa anafahamika kwa jina la Mussa Shija amesema ameitumikia kazi hiyo takribani miaka saba kabla ya kuamua kuachana na kazi hiyo  na kujiunga na Kanisa linaloongozwa na Mchungaji Isaya Laiser chini ya Kiongozi wake Mkuu Nabii Mulilege Mkombo maarufu(Mzee wa Yesu) kutokana na kutopata mafanikio katika uganga wa kienyeji.

Akiongea kwa ujasiri mganga huyo amesema kuwa kazi aliyokuwa akiifanya kwa muda wote huo hakupata mafanikio yoyote licha ya kutoza fedha nyingi kwa wateja wake kuanzia shilingi laki moja hadi milioni mbili ambazo alizitumia kwa anasa tu.

Hata hivyo mke wa mganga huyo Debora Mwandu(30) amesema kuwa yeye anamshukuru Mungu kwa maisha mapya ndani ya Yesu kwani mganga ambaye ni mume wake aliacha kazi yake ya ufundi wa kushona nguo akidai hapati faida yoyote na kujiingiza kwenye uganga akidai kuwa mizimu imemwambia huko ndiko kwenye mafanikio.

Pamoja na kufanya kazi hiyo kwa miaka saba hakuwahi kununua uwanja wa kujenga nyumba wala kuweka akiba benki huku mambo yao yakienda mrama kutokana na mapato najisi ambapo wateja wake wengi walikuwa ni wahalifu wakiwemo majambazi ambao walikuwa wakiomba dawa ili wafanikiwe katika uhalifu.

Baadhi ya wateja walikuwa wanandoa,wanasiasa na wafanyabiashara ambao walikuwa wakihitaji dawa kwa ajili kuboresha biashara zao lakini alijua kuwa huo ulikuwa ni utapeli ambao ulikuwa unamkosanisha na Mungu.

Hata hivyo katika kazi hiyo mganga huyo alikutana na changamoto kutoka kwa walimu wake ambao walidai kuwa ili kuongeza umaarufu ni vema kutumia viungo vya bindamu hali iliyomkosesha amani kutokana na mauaji ya banadamu jambo ambalo amepingana nalo na kuamua kumwishia Yesu.

Vitendo hivyo pia viliendana na matumizi ya wanyama pori ambazo ni nyara za Serikali  kama mafuta ya Simba au ngozi za wanyama hali ambayo aliona ni hatari kwa maisha yake kwani wakati wowote angeweza kukumbana na mkono wa sheria.

Mganga huyo ametoa wito kwa waganga wa kienyeji kuachana na kazi hiyo kwani haina tija kwa jamii pia huleta uchonganishi kwa jamii na kusababisha mauaji  yasiyo ya lazima kwa jamii isiyo na hatia wakiwamo walemavu wa ngozi.

Aidha ametoa rai kwa wananchi kwamba hivi sasa waganga hao wamenda mbali zaidi kwa kudai kujihusisha na mtandao wa free mason kwa kudai kuwaondolea umaskini watu huku wakiwatoza fedha nyingi na wananchi wengi hutapeliwa kwa matumaini ya kupata utajiri.

Kwa upande wake Mchungaji Laiser wa Kanisa la nyumba ya maombi amesema ujio wa mganga huyo ni kufuatia mfungo wa mwezi mzima ukiokuwepo kanisani kwake hivi karibuni,aidha amesema Kanisa lina mpango wa kumnunulia cherehani ili aendelee kushona  aweze kujikimu kimaisha.

Mussa Shija alimaliza kwa kutoa wito kwa waganga wa kienyeji kuachana na mila potofu za uchonganishi kwa jamii ili kuleta amani katika jamii,Mkoa na Taifa kwa ujumla.

WANAWAKE WAMETAKIWA KUJITOKEZA KUPIMA AFYA ZAO ILI KUEPUKANA NA UGONJWA WA SHINGO YA KIZAZI

Chimbuko Letu | 07:49 | 0 comments
 Picha hii imetumika kupamba habari, lakini haijachukuliwa katika eneo husika la habari hii.
 
 
Na Ezekiel Kamanga.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya Daktari Gerald Yubaha amewataka wanawake kujitokeza kwa wigi katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali ili kupima afya zao ili kubaini na kuondoa ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi Wilayani humo.

Yubaha ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani iliyofanyika Kiwilaya katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Itumba Mei 12 mwaka huu ambapo Wauguzi na wahudumu wa Afya walifanya maandamano ya kumkumbuka Muuguzi wa kwanza Duniani ambapo maandamano hayo yalipokelewa na Mkuu wa Wilaya Rosemary Senyamule.

Kaimu Mganga Mkuu amesema kuwa baadhi ya changamoto ni pamoja na ukosefu wa mashine za kupimia vipimo katika Wilaya ambazo zingebaini magonjwa mbalimbali yakiwemo ya shingo ya uzazi kwa akina mama kwani kwa sasa huduma hiyo huipata katika hospitali ya wazazi Meta iliyopo Jijini Mbeya na Hospitali yake hutumia gharama kubwa kuwasafirisha wagonjwa wanaowabaini.

Tangu kuanza kutolewa elimu ya ugonjwa wa shingo ya uzazi wagonjwa wanne walibainika na ugojwa huo ambapo wawili kati yao walifariki kutokana na kuchelewa kupata matibabu na wawili walisafirishwa hadi Mbeya ambapo wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta.

Katika maandamano wauguzi hao walibeba mabango mbalmbali ili kufikisha ujumbe kwa serikali ambayo baadhi yakidai malimbikizo ya stahiki mbalimbali wanazodai watumishi wa sekta ya Afya ambayo hayajalipwa kwa muda mrefu.

Akijibu kero hizo za Wauguzi Mkuu wa Wilaya alisema Serkali imejitahidi siku hadi siku kuhakiksha wanalipa malimbikizo yao kwa wakati kadri fedha zinapopatikana kwani serikali haipo tayari haipo tayari kuona watumishi wake wanaishi maisha duni.

Alisema Serikali ina majukumu mengi ikiwa ni pamoja na upanuzi wa Hospitali hiyo ambapo ujenzi unaendelea ili kuwaondolea adha ya wananchi wa wilaya hiyo badala ya kusfiri umbali mrefu na wengi hupoteza maisha kwa kukosa gharama za kuwasafirisha ndugu zao wanapokuwa wanahitaji matibabu zaidi Mbeya.

Aliwataka kuendelea kuwa wavumilvu na kuwapongeza kwa moyo wa uzalendo ambao wamekuwa wakifanya wa kutoa huduma licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu na kuwajali wagonjwa wanaofika hosptalini kwa ajili ya kupata huduma.

BREAKING NEWS: LIVE MUDA HUU, WAANDISHI WA HABARI WA JIJI WAHAMASIKA BAADA YA MBEYA YETU BLOG PAMOJA NA BOMBA FM RADIO KUKARABATI KIPANDE CHA BARABARA BLOCK T

Chimbuko Letu | 14:04 | 0 comments

Hivi ndivyo Barabara ilivyokuwa kabla
Waandishi wa Jiji wakiwa wamefika kuwashangaa wenzao wakiwa wanafanya kazi ya kutejenga Taifa , wa pili kutoka kushoto ni Mwandishi wa Habari wa Bomba Fm Radio Richard Kamanga aliyekuwa akifanya kazi ya kutengeneza Barabara hiyo akiongea nao.
Baadhi ya wamachinga na wananchi wa eneo hilo aibu zikiwa zimewashuka na kuamua kushirikiana na Waandishi wa Habari kutoka Bomba Fm  Radio na Mbeya yetu Blog kuendelea kutengeneza njia hiyo
Waandishi wa Jiji wakiahidi kuleta kifusi kwa ajili ya kurekebisha Barabara hiyo
 Wachina wakiwa wamefika eneo la tukio na kuahidi kuwa nao wataongeza nguvu katika ujenzi wa Barabara hiyo
Mchina akipata maelekezo juu ya Barabara hiyo
Hii ndio kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Mbeya yetu Blog sambamba na Bomba Fm Radio .

Picha na Mbeya yetu

********************
Wakati kazi ikiendelea baada ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuingia Mitini, na tukio hili kuripotiwa muda mchache uliopita kupitia Mtandao huu na Bomba Fm Radio huku waandishi hao wakiendelea ya kujenga Taifa ndipo Ghafla waandishi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya walipoweza kufika na kuwashangaa wenzao wakiendelea kupiga kazi na baada ya kuona aibu waliamua kuahidi kuleta kifusi kwa ajili ya matengenezo ya Barabara hiyo.

Nao Baadhi ya wamachinga wapenda maendeleo waliweza kujitokeza kwa ajili ya kuwaunga mkono waandishi wa habari walioanzisha kazi hiyo na kuwasaidia kazi inayo endelea ya ukarabati wa kipande hicho cha barabara.
Wachina nao hawakuwa mbali baada ya kusikia ripoti ya tukio hili wakaamua kufika kujionea wenyewe, na wao kuahidi kutoa mchango wao wa kuweza kutengeneza barabara hiyo.
 

Hii ndio Hali halisi ya Barabara ya Block T ambapo imeharibika na kusababisha Dala dala kutaka kugomea kupita katika Eneo hilo kuhofia kukwama.
Hii ni sinto Fahamu ambapo wakati waandishi wa Habari waliojitolea kurekebisha Barabara hiyo wakiendelea na kazi ya kuziba mashimo hayo , watumishi wa Jiji wenyewe walikuwa ndani ya Gari lao wamefunga vioo na kushangaa kinacho endelea bila kuonesha ushirikiano wowote na Baadae waliondoka, Jambo ambalo limewashangaza watu wengi, Huku wakiwa wameahidi wangerekebisha Muundombinu huo.
Mmoja ya Gari dogo likiwa limesimama baada ya kuona kuwa Njia ni mbaya 
Baadhi ya Waandishi wa Habari Kutoka Bomba Fm wakishirikiana na Mbeya yetu Blog wakianza kuchukua Kifusi na Kuziba Barabara hiyo.
Msimamizi Mkuu na Mwandishi wa Mbeya yetu Blog Joseph Mwaisango akiwa anaendelea na kazi ya kuziba eneo hilo lililoharibika
Hali halisi ya Njia hiyo
Mmoja wa wasukuma Mkokoteni akiwa amejitosa kupita katika tope na kuendelea na safari , kutokana na kwamba alikuwa hana Njia nyengine zaidi ya hiyo
Baadhi ya Waandishi wa Habari kutoka Bomba Fm Radio wakiendelea na Kazi
Kazi imepamba moto ambapo waandishi wa Habari kutoka Bomba FM wakiwa wamekomaa kuendelea kuziba mashimo katika barabara hiyo iliyo haribika kwa kiwango kikubwa huku wakazi na wafanya biashara wa eneo hilo wakiwa wanatazama bila kufanya juhudi zozote za kutengeneza, lakini wakisikia kuna mgomo wanakuwa wakwanza kwenda andamana na shughuli za kijamii kama hizi kuzisusia 
Kazi ikiwa inaendelea kwa kasi ili  kupisha Magari yaanze kutumia Njia hiyo huku Wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo wakiwa wanapaangalia tu, na Jiji kufika hapo na gari lao bila kufanya kitu chochote
Kazi ikiwa inaendelea kwa kasi kubwa
Kila mmoja yupo bize
Kazi inaendelea kusonga mbele Picha na Mbeya yetu
********************************
Mbeya yetu Blog kwa ushirikiano mkubwa kabisa na Bomba Fm Radio (elimisha burudisha) waamua kurekebisha kipande cha barabara inayo tumika kupitia daladala zinazo toka uyole kuelekea s/kuu kipande hicho kilichopo Block 'T'

 Ushirikiano huo wa vyombo hivyo viwili vya habari umekuja baada ya madereva wa daladala kutaka kuweka mgomo kwaajiri ya kipande hicho cha barabara kuwa kibovu kinachokuwa ni tatizo kwa daladala hizo.

Wakati tukio hilo la ukarabati  likiendelea Halimashauri ya Jiji la Mbeya wamefika na kuwashangaa tu bila hata kuchukua hatua yoyote na hatimaye kuondoka vivyo hivyo, wamachinga wa maeneo hayo pia wamegoma kutoa ushirikiano wakati wakiambiwa kuhusu masuala ya mgomo huwa mbele kwaajiri ya kuchafua amani.

Bomba Fm Radio na mbeya yetu Blog wamechukua hatua hiyo ili kuepusha migomo isiyo kuwa yalazima kutokana na kupenda amani na kuwajali watanzania ambapo Halimashauri ya Jiji ilitoa ahadi ya kutengeneza lakini mpaka sasa haijaweza kufanya jambo lolote kuhusiana na sehemu hiyo.


Mtazamo : Halimashauri ya Jiji la Mbeya mnapo wahamisha watu kutoka sehemu moja kuelekea sehemu nyingine tunaomba muhakikishe mmewawekea miundombinu ya kutosha ili kuepusha mambo machache yanayo weza kuwa ni tatizo kwa wananchi

MAMA WANNE APELEKWA KATIKA KITUO MAALUMU NA WATOTO WAKE WAWILI WALIOBAKI KWA AJILI YA UANGALIZI.

Chimbuko Letu | 08:38 | 0 comments

 
UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kupitia kitengo cha Ustawi wa jamii  umemtafutia kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru Ophans Centre Mama aliyejifungua mapacha wanne na kubakia wawili baada ya kuugua Nimonia kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
 
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa Hospitali hiyo kumfuata mama mwenye watoto hao Aida Nakawala(25) pamoja na mapacha wake waliobaki kutoka kijijini kwao Chiwanda Wilaya ya Momba mkoani hapa na kuwalaza hospitalini hapo kwa uangalizi wa karibu kwa muda wa zaidi ya wiki moja.
 
Aidha baada ya afya za watoto hao  kuimarika kwa kiwango kikubwa pia Uongozi wa Hospitali hiyo imemtafutia hifadhi katika kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru kilichopo Uyole jijini Mbeya kwa ajili ya uangalizi wa karibu kutoka kwa wauguzi na maafisa wa ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
 
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwakabidhi watoto hao pamoja na mama yao kwenye uongozi wa kituo cha Nuru Orphans centre, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Aisha Mtanda, alisema wameguswa na mazingira anayoishi mama huyo na kuamua kumpa uangalizi kwa miezi sita zaidi.
 
Alisema jukumu hilo halipaswi kufanywa na Hospitali kwa kuwa tayari  walikuwa wamemaliza jukumu lao la kumhudumia alipokuwa ana matatizo lakini wamelazimika kubeba jukumu hilo baada ya kuguswa na mazingira na hali ya makazi ya familia hiyo.
 
Alisema Hospitali imekubaliana na uongozi wa Kituo cha Nuru kwamba apewe hifadhi mama huyo na watoto wake ili apate uangalizi wa karibu ikiwa na lengo la kunusuru maisha ya watoto waliobaki kutokana na wengine kupoteza maisha kiuzembe kwa ugonjwa wa Nimonia.
 
Aliongeza kuwa Hali ya hewa ya Mkoa wa Mbeya kwa siku zijazo kunakuwa na baridi kali sana hivyo watoto wasipokuwa kwenye uangalizi wa karibu wanaweza kupatwa na ugonjwa wa Nimonia tena kwa kukosa matunzo kama ya awali.
 
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Nuru, Amanda Fihavango alisema alikubali jukumu la kuwapokea watoto hao pamoja na mama yao kutokana na kuguswa na hali iliyowakuta ya kupotea kwa watoto wawili kati ya wanne.
 
Aliongeza kuwa ingawa anakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kiuchumi atajitahidi kwahudumia kadri ya uwezo wake na kuomba wasamaria wema watakaoguswa na jambo hilo kujitolea kwa hali na mali kufanikisha kuokoa uhai wa watoto hao pamoja na wengine anaowalea.
 
Alisema kituo chake hupokea watoto waliookotwa baada ya kutupwa na wazazi wao au mama zao kufariki mara baada ya kutoka kujifungua ambao hupelekwa na Serikali kupitia Ustawi wa Jamii ingawa haichangii fedha zozote baada ya kuwapeleka.
 
Mtu yoyote mwenye kuguswa anaweza kuwasilisha mchango wake kituoni hapo au kuwasiliana na Meneja wa Kituo cha Nuru kupitia namba za Simu  0754 043004 kwa ajili ya kusaidia watoto hao pamoja na mama yao kuishi hapo kwa muda wa miezi sita.
 

TIMBWILI LAZUKA BAADA YA VIONGOZI WA SERIKALI KULA PESA ZA WANACHI.

Chimbuko Letu | 01:17 | 0 comments

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mapelele kata ya Ilemi, jijini Mbeya anashtumiwa kwa kutafuna pesa shilingi 1,300,000 zilizochangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya serikali ya mtaa.

Bofya hapa kusikiliza habari kamili inayoletwa kwako na mwandishi wetu Greyson Salufu Chatanda.


MTENDAJI WA KIJIJI NA HALMASHAURI YA KIJIJI WATIMULIWA KIJIJI CHA IWIJI KWA UFUJAJI WA MBOLEA ZA RUZUKU

Chimbuko Letu | 07:27 | 0 comments
Kushoto Afisa tarafa Aaron Sote akipokea funguo toka kwa mtendaji Anton Ndisa 

Afisa Kilimo wilaya Marselin Mlelwa atitoa takwimu  za mgao wa mbolea iliyotolewa Octoba 10 mwaka jana kwa kijiji hicho baada ya kupitishwa na Kamati ya Mbolea ya Wilaya ambayo mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya.

Wananchi wakifuatilia mkutano huo kwa makini


Saimoni Kasebele moja kati ya wajumbe kamati ya mbolea ambayo haikufanya kazi kijijini

Moja kati ya wananchi ambao waliwekwa mahabusu na mtendaji baada ya kufuatilia mgao wa mbolea


Wajumbe waliotimuliwa


Mbolea inayosadikiwa kuibwa Kwa picha zaidi tazama hapa PICHA ZAIDI
Wananchi wa kijiji cha Iwiji Kata ya Iwiji wilaya ya Mbeya wamemtimua Mtendaji wa Kijiji hicho ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Kata aliyefahamika kwa jina la Anthon Ndisa kwa tuhuma za ubadhilifu wa Mbolea za ruzuku mifuko 189 iliyotolewa na serikali kwa kipindi cha msimu wa 2013/2014.

Hatua hiyo imechukuliwa na wananchi hao katika mkutatano wa hadhara uliofanyika kijijni hapo ambapo Afisa Kilimo wilaya Marselin Mlelwa atitoa takwimu  za mgao wa mbolea iliyotolewa Octoba 10 mwaka jana kwa kijiji hicho baada ya kupitishwa na Kamati ya Mbolea ya Wilaya ambayo mwenyekiti wake ni Mkuu wa Wilaya.

Afisa Tarafa ya Isangati Aaron Sote ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ndiye alisimamia mkutano huo amesema kuwa Afisa kilimo ndiye mwenye jukumu la kutoa taarifa ya mgao wa mbolea kama kamati ilivyopitisha.

Baada ya kufunguliwa mkutano  na Mwenyekiti wa kijiji Patson Ngao Afisa Tarafa alimkaribisha Afisa Kilimo kusoma jinsi mgao wa mbolea ulivyokwenda ambapo alisema Kitongoji cha Mabula kilipata mbolea ya Dap mifuko 20 Urea 20, Kitongoji cha Iwiji Dap mifuko 8 Urea 20,Kitongoji cha Soweto mifuko 6 Dap na Urea mifuko 16.

Kitongoji cha Magole kilipata Dap mifuko 6 na Urea mifuko 16,Kitongojo cha Mtukula Dap mifuko 6 na Urea mifuko 16 wakati Kitongoji cha Ntinga kilipata Dap mifuko 8 na Urea mifuko 20 wakati Kitongoji cha Vimetu kikipata Dap mifuko 7 na Urea mifuko 20.

Katika mgao huo kulikuwa na upungufu wa mifuko 50 ya Dap na Urea mifuko 36 ambayo wakulima hawajapatiwa na kwamba ikifika wananchi wagawiwe ili kukamilisha idadi ya mifuko 189 kwani hivi sasa mifuko iliyogawiwa ni mifuko 139 tu.

Baada ya kusomwa taarifa hiyo wananchi walitaharuki wakidai kuwa hesabu hizo zimetengezwa na Mtendaji Anthon Ndisa kwa manufaa yake kwani wananchi hawajapata mbolea hiyo licha ya kutoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya kupitia Afisa Pembejeo Lupakisyo Masuba.

Kutokana na kutoridhishwa na taarifa hiyo na kwamba wananchi wamehujumiwa na uongozi wa kijiji kupitia viongozi wa vitongoji ambao walikiri kupokea mbolea hiyo na kuigawa wakati kuna kamati mbolea ya kijiji ambayo ndiyo ilikuwa na jukumu la kugawa ambapo uongozi wa kijiji ukidai kamati hiyo ilivunjwa.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya pembejeo Simon Kasebele amesema kuwa kati iliyokuwa na wajumbe sita ambao ni Mwenyekit Venance Lwinga,Lucia Mose,Sara Kasalama,Patson Kayelewe na Eva Makanika haikufanya kazi kutokana na agizo la Mtendaji aliyedai kuwa kamati imevunjwa wakati siyo kweli bali ilikuwa ni njama za kuwahujumu wananchi kwa manufaa yao.

Baada ya majadiliano marefu wananchi waliamua kuirudisha Kamati ya Mbolea huku wakimtaka Mtendaji kuondolewa haraka ili kuepusha ufujwaji wa mali za kijiji na kuwatimua wenyeviti wote wa vitongoji na kumwacha Mwenyekiti wa kijiji pekee Patson Ngao wakidai hahusiki na ubadhilifu kwani alizungukwa na Mtendaji kupitia wenyeviti wa vitongoji.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Marselin Mlelwa amesema taarifa ataifikisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ili kutoa maamuzi kwa vile Mtendaji ni Mwajiriwa hivyo lazima taratibu za utumishi lazima zifuatwe.

Ili kuhakikisha hakuna nyaraka zozote zinachukuliwa Ofisi Mwenyekiti na Kamati ya Mbolea watafanyia shughuli zao katika ghala la Kijiji wakati Mtendaji aliagizwa kubaki na funguo hadi hapo Halmashauri itakapotoa taarifa zake baada ya ukaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Upendo Sanga amekiri kupokea taafa za malamiko ya wananchi wa Iwiji na kuwataka kuwa na subira kwani serikali ina utaratibu wake ambao lazima ufuatwe pindi mtumishi anapotuhumiwa kwa jambo lolote ikiwa na pamoja na kuunda Tume ya Uchunguzi na Wakaguzi ili kupata Ushahidi.

Uchunguzi uliofanywa baada wananchi kulalamikia utaratibu uliotumika kugawa mbolea hiyo Mtendaji wa Kijiji alirejesha mifuko 50 ya Dap ambayo imehifadhiwa kwa mmoja wa Mawakala kijijini hapo ili kuficha ushahidi na kuonekana mbolea hiyo ilikuwepo wakat ukweli ni kwamba mbolea hiyo tangu itolewe mwezi Octoba wananchi hatanufaika nayo kwa kuwa msimu wa kilimo umepita na kijiji kukabiliwa na hatari ya njaa.

Mbali ya tuhuma ya Mbolea Mtendaji anatuhumiwa kufuja fedha za serikali na michango ya wananchi kwa ajili ya kituo cha Afya hivyo wamemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri anapofanya uchunguzi wa Mbolea afanye ukaguzi pia mradi wa Kituo cha Afya na kama ikibainika Mtendaji na Halmashauri ya Kijiji wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Na Ezekiel Kamanga
 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger