Habari na Rashid Mkwinda, Mbeya.
Kikao cha
kamati ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ileje mkoani Mbeya kimepitisha
maamuzi ya kuwasimamisha kazi watumishi wanne wa halmashauri hiyo waliotuhumiwa
katika jaribio la wizi wa sh milioni 86.2 zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi
wa zahanati hewa katika kata ya Ruswisi na Ibaba wilayani humo.
Akitangaza
maazimio ya kamati ya madiwani iliyoketi kujadili tuhuma za watumishi hao
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw. Mohamed Mwala amewataja watumishi
waliosimamishwa kupisha sheria kuchukua mkondo wake kuwa ni Bi. Subilaga
Kapange ambaye kaimu mweka hazina wa wilaya hiyo na watumishi wengine watatu.
Bw. Mwala
amewataja watumishi wengine kuwa ni Ofisa Mipango wa wilaya hiyo Bw.Mchuuzi Limbanga,Bw.Henry
Kagogoro ambaye ni Ofisa Utumishi na Bw. Anyitike Chisunga ambaye ni mhasibu
msaidizi wa wilaya.
Awali kabla
ya kupitishwa kwa uamuzi huo kubadili kikao cha baraza kuwa kamati kuliibuka
majadiliano ya kuzuia kuwepo kwa kikao hicho ambapo Mwanasheria wa halmashauri Bw.Agape
Fue alidai kwamba kwa kuwa suala hilo lipo katika upelelezi wa polisi si vyema
madiwani wakaliwekea mjadala.
Kwa upande
wake Diwani wa kata ya Ibaba Bw. Tata Kibona amesema kuwa suala hilo linapaswa
kujadiliwa katika kamati ili kuweka uwazi juu ya tuhuma zilizopo kwa watumishi
hao na kwamba kitendo cha kuendelea kuficha ukweli kitaendelea kuficha ukweli
juu ya tuhuma za watumishi hao ambao hadi sasa wanaendelea kuripoti kazini.
Naye Diwani
wa kata ya Ruswisi Bw. Rauden Tuya amesema bila kuweka mkazo juu ya suala hilo
kuna hatari ya halmashauri hiyo kupata hati chafu, hivyo ni vyema kuwekea mkazo
wa kuwawajibisha watumishi wenye nia mbaya na halmashauri hiyo.
Mkurugenzi
wa halmashauri hiyo Bi. Sylivia Siriwa amesema kuwa mara baada ya kupata
taarifa za jaribio hilo aliwasiliana na Meneja wa Benki ya NMB kusimamisha
ulipaji wa fedha hizo kwa kuwa hakuna mradi wa aina hiyo katika kata za Ruswisi
na Ibaba na baadaye aliwaonya kwa
kuwandikia barua watumishi hao.
0 comments:
Post a Comment