Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mgogoro kati ya Mwekezaji wa Shamba la Kapunga Rice Project (KRP) na wananchi wa Kijiji cha Kapunga, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, umeingia katika sura mpya baada ya watu wasiofahamika kulichoma Trekta la mwekezaji kwa moto.
Hata hivyo trekta hilo halikuteketea lote baada ya kufanikiwa kuwahi kuuzima moto huo na hasara iliyopatikana kutokana na mto huo haijaweza kufahamika mpaka sasa.
Mkuu wa wilaya hiyo Kanali Cosmas Kayombo ambaye amepata uhamisho na kuhamia wilaya mpya ya Kakonko kufuatia uteuzi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta Jakaya Kikwete, ameweza kutembelea eneo hilo la tukio ili kujionea hali ambayo imemsikitisha.
Tukio hilo ni mfululizo wa matukio ambayo yamefanywa baina ya mwekezaji na wananchi ya kulipizana kisasi, baada ya mara kadhaa mwekezaji huyo kuwafanyia fujo wananchi hao matharani kwa kuteketeza mpunga kwa madawa yaliyonyunyizwa kwa ndege mapema mwezi Januari na kuleta hasara kubwa kwa zaidi ya wananchi 154 wa kijiji hicho.
Wakati hayo yakiendelea kesi inayohusiana na uharibifu huo yao ipo mahakama ya mkoa, licha ya wananchi kulalamikia ucheleweshwaji wa kesi hiyo.
Wakati huohuo leo hii wananchi hao wamepanga kufanya maandamano ya amani kupinga vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na mwekezaji huyo kwani mpaka sasa wananchi wamezuiwa kuutoa shambani mpunga baada ya kukodi mashamba kwa mwekezaji huyo akishinikiza kuuziwa yeye.
0 comments:
Post a Comment