Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika
Shule ya Sekondari Isange na mkazi wa Isanu, Kata ya Isange, Wilaya ya
Rungwe Mkoani Mbeya amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya
kufungia ng'ombe mara baada ya kugundulika na ujauzito wa miezi mitatu
Mei 11 mwaka huu.
Afisa mtendaji wa Kata hiyo Bwana
Anyambege Mwangomo amelitaja jina la marehemu kuwa ni Enitha Ndambo
(15), ambaye alikuwa akiishi na bibi yake Bi Emelia Ndenga.
Marehemu alichukua hatua hiyo ya
kujinyonga wakati mlezi wake akiwa katika kilabu cha pombe na kamba
aliyotumia ilikuwa ndani ya nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi.
Polisi walifika eneo la tukio kwa
lengo la kuukagua mwili wa marehemu na baada ya kuukagua waliuchukua na
kuupeleka katika Zahanati ya Isange kwa ajili ya kufanya upasuaji, ili
kuthibitisha kama alikuwa na ujauzito na mara baada ya upasuaji
waliwaruhusu wanakijiji kuzika mwili wa marehemu na kiumbe cha mtoto
kilichokuwa tumboni.
Mwili
wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na Daktari Kalinga kutoka katika
Hospitali ya Serikali ya Makandana iliyopo wilayani humo, na zoezi la
upimaji wa kubaini wanafunzi walio na ujauzito ulifanywa na Daktari Anna Mwelevu wa Zahanati ya
Isange..
Aidha katika uchunguzi uliofanywa
umebaini aliyemsababishia ujauzito ni mwanafunzi wa shule hiyo hiyo Alex
Mwaitege, anayesoma kidato cha kwanza.
Wakati huo huo Obelo Mwakilasa (46),
mkazi wa Kijiji cha Mwela, Kata ya Kandete wilayani humo ametuhumiwa
kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 na kumsababishia maumivu
makali katika mwili wake.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana
Anania Mwalukasa amesema tukio hilo limetokea Mei 10 mwaka huu, ambapo
mtuhumiwa anadaiwa alimuita mtoto huyo kwenye shamba la michai kisha
kumfanyia ukatili huo.
Baada ya kukuta anakumbana na mkono
wa sheria Mwalikasa alienda kuomba msamaha kwa wazazi wa mtoto huyo ili
wamsamehe, ombi ambalo lilipokelewa na kusamehewa.
Aidha imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alifika kijijini hapo kwa mbinu ya kuhubiri neno la Mungu.
Kwa upande wake Mwenyekiti Bwana
Mwalukasa ameonekana kukasirishwa na kitendo cha wazazi hao kusameheana
nyumbani na kudai kuwa tabia hiyo ikiendekezwa itasababisha kuendelea
kwa vitendo viovu kijijini hapo.
Madhara hayo yaliyosababishwa na
Bwana Mwakilasa kwa mtoto huyo hayajaweza kufahamika kutokana na wazazi
kutompeleka mtoto wao kufanyiwa uchunguzi katika Kituo chochote cha
huduma ya Afya(Zahanati/Kituo cha afya/Hospitali).
Hata hivyo vitendo hivyo vya ubakaji wilayani humo vimeota mizizi kutokana na baadhi ya wazazi kufumbia macho kwa kupewa pesa.
0 comments:
Post a Comment