Pages


Home » » WALIMU WATARAJIWA 200 WAHITIMU CHUO CHA UALIMU MORAVIAN MBEYA

WALIMU WATARAJIWA 200 WAHITIMU CHUO CHA UALIMU MORAVIAN MBEYA

Kamanga na Matukio | 05:45 | 0 comments
Mgeni Rasmi wa hafla ya mahafali ya wanachuo wa Chuo cha Ualimu Moravian Dr Victoria Kanama, ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya K'S iliyopo jijini hapa na pia ni Mkuu wa Bodi ya Chuo Kikuu cha TEKU, akimkabidhi mmoja wa wahitimu cheti chake.
****** 
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Chuo cha Ualimu cha Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi Mbeya Tanzania, kimefanya mahafali ya pili ya kuhitimu mafunzo ya Ualimu Mei 2 mwaka huu.

Wahitimu wa mafunzo ya ualimu 200 wa ngazi ya Cheti na stashahada wamehitimu katika chuo hicho kilichopo Mtaa wa Forest ya zamani karibu na Kituo cha mabasi madogomadogo Kadege jijini hapa.

Sherehe hiyo ilifunguliwa kwa maombi na Baba Askofu wa kanisa la Moaravian Tanzania Alinikisa Cheyo, ambapo pia alisema kanisa linathamini mchango mkubwa wa elimu, ndio dhumuni lililopelekea kujenga chuo hicho cha ualimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Eliackim Mtawa, amesema kuwa chuo hicho kilianza rasmi mwa 2009 na kupata mafanikio makubwa kwani kati ya wahitimu 91 wa cheti wahitimu 90 walifaulu vizuri na wahitimu 13 wa stashahada walifaulu na kwamba wanajivunia matokeo hayo kwa mshikamano uliopo baina ya Bodi ya chuo, walimu, wanachuo na mmiliki ambaye ni Kanisa la Moravian.

Hata hivyo chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo huduma ya maji na vifaa vya kufundishia, ambapo kanisa limemekuwa likifanya jitihada za kuzitatua mara pesa inapopatikana.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho Bwana David Mwankina amelitaka kanisa kuondoa urasimu ili kuharakisha maendeleo ya chuo hicho, ikiwa ni pamoja na kuongeza majengo kutokana na ongezeko la wanachuo.

Katika risala yao wahitimu wamesema kuwa ualimu sio jalala la watu walioshindwa hivyo wameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kutoa mtaala mpya utakaosaidia ubora wa elimu nchini kwa kuchukua walimu wenye sifa.

Kwa upande wake mgeni rasmi Dr Victoria Kanama, ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya K'S iliyopo jijini hapa na pia ni Mkuu wa Bodi ya Chuo Kikuu cha TEKU, amewataka wahitimu kufuata maadili mazuri ya ualimu na hivyo kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho, ambapo pia alikazia suala la kujiendeleza kielimu zaidi na kutobweteka.

Pia ameipongeza serikali kwa kuajili walimu wote waliohitimu mwaka uliopita.

Kanisa la Moravian linamiliki miradi mbalimbali mkoani Mbeya kikiwepo Kituo cha redi cha kurushia Matangazo Baraka FM, Chuo cha Ufundi (MVTC), Kiwanda cha uchapaji (press), Hospitali Mbozi Mission, Chuo cha ualimu na Vituo vya kulelea watoto yatima vya Mbozi na Nsalaga.

Wakati huo huo Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Moravia Jimbo la Kusini Magharibi Mchungaji Zacharia Sichone,  amemshukuru mgeni rasmi kwa hotuba yake ambayo italeta mwelekeo mzima wa chuo hicho na kwa kanisa kwa ujumla.

Wahitimu hao wataanza mitihani yao ya Taifa Mei 7 mwaka huu na wameahidi kufanya vema ili kuendeleza sifa ya chuo hicho na mgeni rasmi aliwatakia baraka njema katika mitihani yao.

Chuo hicho kinaendelea kupokea maombi ya wanachuo wapya ambao watakuwa na sifa kama za daraja la nne alama 27 badala ya 28 za awali.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger