Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mtonya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, waliosimama barabarani na kuzuia msafara wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati akipita katika kijiji hicho akiwa katika ziara yake ya Mkoa huo leo.
Wananchi hao walifanya tukio hilo kwa ajili ya kuwataka viongozi hao kusimama na kusikiliza kilio chao kuhusu watu waliofika kijijini hapo hivi karibuni na kuezua mabati ya nyumba ya Mjane mwenye watoto nane, aliyefiwa na mumewe wakidai kuwa marehemu alikuwa akidaiwa na chama cha Ushirika cha kukopa na kulipa.
Aidha Wananchi hao walisema kuwa watu hao walifika kijijini hapo na kuanza kazi hiyo ya kuezua mabati na kuondoka nayo na kuiacha familia iliyokuwa ikiishi katika nyumba hiyo ikikosa mahala pa kulala hadi hii leo kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na mabati.
Akizungumza na wananchi hao Mkuu wa Mkoa, Said Mwambungu, aliwataka wananchi hao kupunguza hasira na kuwaahidi kulishughulikia tatizo hilo kwa kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika mikono ya sheria na iwapo watakutwa na hatia wataadhibiwa.
Akitoa agizo la kuwakamata wahusika wa tukio hilo kwa Mkuu wa Wilaya hiyo na Kamanda wa Polisi wa Wilaya hiyo, Mwambungu alisema kuwa, ''Tayari nimekwisha waagiza Mkuu wa Wilaya na Kamanda wa Polisi wa Wilaya hii na wote wapo mahala hapa, ''Mkuu wa Wilaya na Kamanda hebu simameni'',
Nawaagiza kuanzia muda huu anzeni kazi mara moja ya kuwatia nguvuni watu hawa waliohusika na tukio hili la ajabu na watuambie ruhusa hii ya kutesa watu wameitoa wapi na kama waliagizwa na mahakama, Hakimu atatueleza hukumu hii aliitoa wapi ya kuezua mabati kwa deni la mdaiwa''. alisema Mwambungu na kushangiliwa na wananchi hao.
Nyumba hiyo iliyoezuliwa mabati (pichani upande wa kushoto) kama inavyoonekana.
Wananchi wa Kijiji hicho wakishangilia kwa staili ya aina yake na kumpongeza Mkuu wa Mkoa baada ya kutoa kauli hiyo, alipozungumza nao.
Mkuu wa Mkoa akiondoka eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment