Habari na Rashid Mkwinda, Mbeya.
Wanawake waishio wilaya ya Ileje, Mkoani Mbeya wametakiwa kuachana na
dhana potofu za kuwaficha watoto wenye ulemavu na badala yake wametakiwa kujitokeza na watoto
hao Agosti 26, mwaka huu kwa ajili ya sensa ya watu na makazi ambayo itaendeshwa nchini
kote.
Zoezi hilo
la sensa limelenga kuhesabu watu ili kupata takwimu sahihi ya wakazi kwa nia ya
kuiwezesha serikali kujua idadi ya watu kwa lengo la kupanga mikakati ya
maendeleo kutokana na idadi kamili ya wananchi.
Akizungumza katika zoezi la uhamasishaji wa sensa
wilayani humo Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Mbeya Bi. Hilda Ngoye amesema kuwa
kumekuwepo na desturi ya wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu na kuwataka
kuwafichua wakati wa sensa ya watu na makazi.
Amesema kuwa wapo baadhi ya wakazi wa
maeneo ya vijijini ambao wamepandikizwa itikadi kuwa zoezi la kuhesabu
watu
lina nia ya kupunguza watu kwa kuwafunga vizazi akina mama na kwamba si
kweli bali serikali inahitaji kuweka mipango juu ya takwimu
sahihi za wakazi wake ili kupanga maendeleo.
Pia amewataka wananchi kujitokeza
kutoa maoni yao
wakati wa uboreshaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kwamba mawazo ya
wananchi yatakayotolewa yatasaidia kuunda Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya
Watanzania katika mfumo wa kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Akizungumzia mikakati ya wanawake kujikwamua
kiuchumi Bi. Ngoye amesema kuwa wanawake wanayo fursa kubwa ya kujiwezesha kwa
kubuni kazi za mikono ikiwemo ufugaji, ususi na ufinyazi na kwamba ili kuweka
uwiano wa kiuchumi katika jamii wanawake wanatakiwa kuacha utegemezi na
kuanzisha vikundi vya ujasiriamali.
Amebainisha kuwa zipo fursa nyingi kwa akina
mama ambazo zikitumiwa ipasavyo wanawake wanaweza kujikwamua kiuchumi na
kuongeza kuwa wanawake waishio maeneo ya mipakani wanazo fursa za kipekee kwa
kutumia rasilimali za hapa nchini na kuwauzia nchi jirani za Zambia na Malawi.
Hata hivyo Bi. Ngoye amekutana na Vikundi saba
vyenye jumla ya akina mama 210 katika kata za Mawindi, Rujewa, Mswiswi, Chimala
vilivyopo katika wilaya ya Mbarali, Itumba iliyopo katika wilaya ya Ileje, Kyimo
iliyopo katika wilaya ya Rungwe na Lisungo iliyopo katika kata ya Kyela.
0 comments:
Post a Comment