Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Dereva aliyefahamika kwa jina la Frank Joachim Kyando (28), mkazi wa Jijini Dar es salaam, amefariki dunia baada ya kutokea ajali ya gari nambari T 194 AAG aina ya Scania katika Kijiji cha Kongolo Mswiswi wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Mei 10, mwaka huu.
Dereva huyo akiwa na tingo wake aitwaye John Joshua Kurwa (24), walitokea Chimala wilayani humo baada ya lori hilo kuanguka mara ya kwanza, kisha kuinuliwa katika barabara ya Iringa/Mbeya na walikuwa wakielekea Mbeya kwa ajili ya matengenezo na baadae ili walirudishe Jijini Dar es salaam kwa matengenezo zaidi.
Lori hilo baada ya kumaliza kupandisha mlima wa Kongolo Mswiswi lilianza kwenda kwa kasi na kupoteza mwelekeo kutoka upande wa kushoto lililopokuwa na kuhamia upande wa kulia ambapo gari hilo lilipaa na kuanguka msituni, ambapo tingo alifanikiwa kuruka huku dereva akiwa katika gari hilo alilaliwa na lori hilo hadi mauti yalipomkuta.
Aidha mashuhuda katika ajali hiyo walijaribu kuunasua mwili wa marehemu bila mafanikio kutokana ukosefu wa vitendea kazi hali iliyowalazimu kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mswiswi ambapo waliomba msaada wa tingatinga kutoka Tazara Kongolo Mswiswi.
Mwili wa marehemu Kyando umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa, jijini Mbeya huku utaratibu wa kuwasiliana na Kampuni ya Mohammed Coach ya jijini Dar es salaam zikifanyika.
Hata hivyo juhudi za kumtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Barakiel Masaki, zilishindikana baada ya simu yake kutopatikana hewani na lori hilo bado lipo eneo la tukio.
Katika hali isiyo ya kawaida vijana wa kijiji hicho walilikimbilia lori hilo wakiwa na pikipiki zao pamoja na madumu wakidhani ni lori la mafuta.
Chanzo cha ajali hiyo imesababishwa na kukatika kwa centre bolt ya gari hilo.
0 comments:
Post a Comment