MHARIRI wa Picha wa Kampuni ya Tanzania
Standard Newspaper Limited (TSN), Athumani Hamisi ameziomba kampuni,
taasisi, wizara na watu binafsi kumsaidia ili aendeshe maisha yake.
Kwa takribani miaka minne, Athumani
amekuwa akitibiwa baada ya mwili wake kupooza kutokana na ajali ya gari
iliyoharibu uti wa mgongo aliyoipata Septemba 12, 2008 eneo la Kibiti,
Pwani na kwenda kutibiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kwenye Hospitali ya
MilPark ya Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam, Athumani alisema kwa sasa amekuwa anatumia kati ya Sh
750, 000 mpaka 900,000 kwa mwezi kwa ajili ya gharama za chakula, vifaa
na gharama ndogondogo za wanafunzi.
Alisema kila mwezi anawalipa muuguzi na
msaidizi wake Sh 370,000 na ada ya watoto watatu ambayo ni Sh milioni
2.4 ikiwa ni Sh 200,000 kwa muhula mmoja kwa mtoto mmoja.
“Maisha ya ulemavu ni ghali na sikutarajia hali hii. Nilikuwa nasaidia sana omba omba na yatima, lakini sasa nimekuwa ombaomba.
Ndugu wote wamenikimbia waliobaki ni
marafiki wa kweli walioniingiza katika familia zao. Hali yangu ni mbaya
sana kiuchumi,” alisema Athumani.
“Sina uwezo wa kulipa nyumba kwa gharama
zozote zile, ninaomba Watanzania watakaoguswa wanisaidie nyumba na kwa
ushauri wa daktari nimeshauriwa nisiishi mbali na mazingira ya
hospitali,” alisema.
Msaada huo unaweza kupelekwa kwa akaunti
namba za CRDB, 01J2027048800, Posta Benki namba 010-00090488 na kwa
namba za mitandao ya simu za M-Pesa 0757825737, Tigo-Pesa 0655531188,
Airtel Money 0784531188, M-pesa ya Chris Mahundi 0767298888 na Airtel
Money ya Ephraim Mafuru namba 0686710977.
Aidha, Athumani alimshukuru Rais Jakaya
Kikwete kwa kumtembelea katika Hospitali ya Muhimbili na kuagiza
apelekwe nje kwa matibabu zaidi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
pia kampuni anayoifanyia kazi ya TSN na waumini wa dini zote na marafiki
zake waliohangaika.
“Ukweli ulio wazi, nashukuru kwa Mungu
na kujivunia kuwa TSN.Nimelelewa na TSN kwa miaka sita sasa. Imenilea
nikiwa mgonjwa kwa miaka minne, nikiwa bado niko ndani ya ajira jambo
ambalo ni gumu sana sehemu nyingine,” alisema Athumani.
0 comments:
Post a Comment