Habari na Angelica Sullusi,Mbeya.
Sakata
la Mgomo wa Madaktari limeingia katika sura mpya Mkoani Mbeya baada ya
Bodi ya Hospitali ya Rufaa Mbeya ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, kutishia kusitisha mikataba ya madaktari waliogoma hasa
wale ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo.
Akizungumza
kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa
wa Mbeya, Dk. Norman Sigalla amewaambia waandishi wa habari leo kuwa
Bodi imefikia uamuzi huo baada ya kuona madaktari hao wamevunja mkataba wao na hospitali hiyo ambao unawataka kufanya kazi bila kugoma.
Aidha,
amesema kabla ya kuwaandikia barua hiyo, juzi bodi ya Hospitali
ilikutana na kuwaita madaktari wote kwa barua ili wakae nao na
kuwasikiliza madai yao lakini hakuna daktari hata mmoja aliyejitokeza
kwenye kikao hicho.
Ameongeza
kuwa kwa mujibu wa sheria za kazi mtumishi asipofika kazini kwa muda wa
siku tato mfululizo anakuwa amejifuta kazi mwenyewe, hivyo kama
madaktari hao hawataripoti kazini kufikia leo, watalazimika kuwaondoa na
kuwarejesha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye aliwatuma kwenda
kufanya mazoezi ya vitendo hospitalini hapo.
Akizungumzia madaktari waliosajiliwa ambao wanashiriki mgomo huo, Dk. Sigalla amesema na wao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye mwajiri wao.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky
amezungumzia madhara yaliyosababishwa na mgomo huo kwa wagonjwa, kuwa
tangu madaktari hao kugoma kuwa wagonjwa waliofika hospitalini hapo kwa
matibabu wameathirika kwa namna moja ama nyingine kwa kuwa hakukuwa na
huduma ya kuridhisha.
0 comments:
Post a Comment