Mmoja wa walimu waliokuwa na watoto wao na hivyo kulazimika kulala wima huku wakiwa wamewapakata, wakati wa madai ya mafao yao ya pesa za nauli, posho na mishahara yao ya miezi miwili, na katika hali isiyoyakawaida mtumishi mmoja wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi alimtamkia kuwa mtoto hana baba yake mpaka anaenda naye katika Ofisi za halmashauri hiyo..
Baadhi ya walimu kutoka katika Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari wilayani Mbozi, wakiwa nje ya Ofisi za Halmashauri ya Wilaya hiyo wakisubiria pesa za nauli, mishahara na posho ambazo hawajalipwa kwa takribani miezi miwili mpaka sasa.
Walimu tuna hali ngumu maisha yetu yamewekwa rehani kwenye maduka na Maafisa watendaji wa Kijiji, ambao wamekuwa wakitukopesha pesa za kujikimu.
*****
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Zaidi ya walimu 50 waliopata ajira mpya hivi karibuni katika Shule za Msingi na Sekondari katika Wilaya ya Mbozi, Mkoani Mbeya wamejikuta wakilala chumba kimoja baada ya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya hiyo kufungwa huku walimu hao hawajapata sitahili zao.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea kwa siku mbili mfululizo, baada ya walimu hao waliotokea maeneo tofauti tofauti wilayani humo na baada ya kufika katika Ofisi hizo za Halmashauri hawakuweza kupata stahili zao kama vile pesa za kujikimu, nauli na mishahara kwa muda wa miezi miwili mpaka sasa.
Mnamo Machi 6 mwaka huu, walimu hao walimuona Mkuu wa Wilaya hiyo Bwana Gabriel Kimoro ambapo walilipwa posho ya shilingi laki moja (100,000) kwa kila mmoja kwa ahadi ya kuwa mwishoni mwa mwezi stahili zao zote zingelipwa, lakini mambo yalikuwa tofauti Machi 27 na 28 kwani madai yao yalikuwa hayajashughulikiwa.
Kiongozi wa walimu hao Mwalimu Carlos Magoyo amesema baada ya maafisa wa halmashauri kutawanyika waliamua kulala katika ofisi hizo za Mkuu wa wilaya kwani walikuwa hawana pesa za nauli na kujikimu, kabla ya kutokea msamaria mwema aliyewapa chumba hicho kimoja na kuchanganyika jinsi zote huku wakiimba pambio na kutafuna mahindi ya kuchoma.
Aidha Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Bwana Levson Chilewa amesema madai yao ya posho yanaanza kushugulikiwa mara moja na Ofisi ya fedha ya halmashauri hiyo lakini kuhusiana na mishahara yao ipo nje ya uwezo wake kwani suala hilo linashughulikiwa na Serikali kuu yaani Hazina kuu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Bwana Kimoro ameahidi kufuatilia madai hayo kwa ukaribu zaidi na amesikitishwa kwa kitendo hicho cha kucheleweshwa mishahara kwani baadhi ya walimu wanatoka mbali na mji wa Vwawa na asingependa kuona walimu wakiishi maisha ya kuombaomba.
Naye, Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya Bwana Juma Kaponda amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba atawasiliana na Mkurugenzi wa wilaya hiyo ili walimu hao walipwe mapema iwezekanavyo, ingawa kwa sasa yupo safarini kikazi nje ya mkoa.
Baadhi ya walimu walionekana wakiwa na watoto wadogo na baadhi yao wamekesha wakiwa wamewapakata watoto wao kutokana na kukosa eneo la malazi sambamba na kukosa hata chakula cha watoto ambao wapo chini ya umri wa miaka miwili.
0 comments:
Post a Comment