Habari na Angelica Sullusi, Mbeya.
Hatimaye wanafunzi waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu na kuchelewa kuanza masomo yao kwa kukosa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Mbarali, Kata ya Ubaruku Wilayani hapa wanatarajia kuanza masomo yao mwisho wa mwezi huu baada ya vyumba hivyo kukamilika.
Akizungumza na mwandishi wetu, Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Mikidadi Mwazembe amesema kuwa vyumba hivyo vipatavyo tisa vinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Mwazembe amesema kuwa mafanikio ya ujenzi wa vyumba hivyo yanatokana na jitihada za makusudi za serikali,mfuko wa jimbo na uhamasishaji wa wananchi katika kuchangia ujenzi huo.
Amesema kuwa katika ujenzi huo wamewatumia mafundi wa kawaida ndani ya kata hiyo kwa lengo la kuwawezesha kupata fedha za kujikimu na maisha,lakini ujenzi huo ukiwa chini ya usimamizi wa wahandisi wa ujenzi wa wilaya hiyo ambapo ujenzi huo unatarajia kughalimu kiasi cha shilingi milioni 75.
Mbali na jitihada hizo,Mwazembe amesema mpaka sasa wana mikakati ya kujenga shule nyingine mpya ya sekondari kuanzia mwezi juni mwaka huu,hivyo kuipongeza Kamati ya Maendeleo ya Kata(WODC),chini ya Diwani wa kata hiyo na wananchi kwa ujumla.
Aidha, ameiomba serikali kwenda na kasi ya kuongeza walimu zaidi ili kukidhi matarajio ya wananchi ambao wamekuwa mstali wa mbele katika uchangiaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na majengo ya shule mbalimbali za sekondari.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Cosmas Kayombo, amepongeza jitihada za makusudi zilizofikiwa na uongozi huo katika kufanikisha ukamilikaji wa ujenzi huo wa madarasa ambao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya wananchi.
0 comments:
Post a Comment