Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Watu wawili wamefariki dunia mkoani Mbeya katika matukio mawili tofauti, yaliyotokana na Pikipiki na mwingine anusurika kifo baada ya kuvamiwa na kuanza kukatwa viungo vyake kwa kutumia kisu kikali.
Tukio la kwanza limetokea majira ya saa nne usiku, barabara ya Mbeya/Iringa katika eneo la Inyala wilaya ya Mbeya Vijijini Adam Mathias (19), ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Imezu amefariki dunia baada ya kuanguka na pikipiki yenye nambari za usajili T 566 BJC na kumsababishia kifo chake papo hapo.
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi hali iliyompelekea kushindwa kumudu pikipiki hiyo, na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya.
Tukio la pili limetokea Kiwira barabara ya Mbeya/Tukuyu majira ya saa 8 mchana, Februari 12 mwaka huu pikipiki yernye nambari za usajili T 830 BWE aina ya T – BETTER ikiendeshwa na Frank Mwansasu (19) mkazi wa Kiwira iligongana na gari aina ya Toyota Hiace ikiendeshwa na Seleman Michael na kusababisha kifo cha dereva wa pikipiki papohapo.
Chanzo cha ajali hii ni mwendokasi wa dereva wa pikipiki ambapo yeye na wenzake walikuwa na pikipiki hizo katika shamrashamra za kuanza kampeni za uchaguzi wa Diwani Kata ya Kiwira, kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo.
Aidha mwanafunzi Ikusubila Sichinga (17), mwanafunzi wa Kidato cha nne shule ya sekondari Itiji amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa vibaya baadhi ya viungo vyake vikiwemo mguu wa kulia na mikono na mtu aliyemvizia njia alipokuwa akitokea shuleni majira ya saa 10 jioni.
Katika hali ya kujitetea binti huyo alipiga kelele huku kijana huyo akiendelea kukata fundo la goti na viwiko vya mikono kwa kutumia kisu kikali.
Baada ya kuona kelele zikizidi kijana huyo alimdhalilisha binti huyo kwa kumchania nguo zake za shule na nguo za ndani kisha kijana huyo kutokomea katika msitu wa Itende, ambao hivi sasa ni Hifadhi ya Halmashauri ya jiji la Mbeya.
Baada ya kufuatilia kelele za binti huyo katika msitu huo kijana Aman Aman (19), alisaidia kumbeba umbali wa mita 20 kutoka katika njia akisidiwa na mama mmoja na mlinzi wa shule hiyo kisha kumfikisha shuleni kabla ya kumpeleka Hospitali ya Rufaa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bwana Festo Mtagawa amesema tukio hilo ni la kwanza kufanyika shuleni hapo, na amewataka wazazi na wanafunzi kuchukua tahadhari katika msitu huo hivi sasa kwa kuwa msitu huo una vichaka, kutokana na wanafunzi wa shule za sekondari ya Itende na Itiji hutumia njia iliyopo katikati yam situ huo ili waweze kufika haraka shuleni.
Baba mzazi Peter Sichinga ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Moravian Ushirika wa Itende amesema amesikitishwa na Jeshi la Polisi kushindwa kufika eneo la tukio, licha ya kutolewa taarifa na kupewa PF3 kwa ajili ya matibabu.
Mwanafunzi huyo Ikusubila amelazwa katika Hospitali hiyo wadi namba mbili, akiendelewa kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ambayo yamesababisha kuvuja damu nyingi.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa matukio yote.
0 comments:
Post a Comment