Pages


Home » » TAZAMA YATOA MSAADA

TAZAMA YATOA MSAADA

Kamanga na Matukio | 05:05 | 0 comments
Na.Shomi Mtaki, Mbozi
Kampuni ya kusafirisha mafuta kwa njia ya Bomba kwa nchi za Tanzania na Zambia (TAZAMA) Pipelines Limited, kanda ya mkoa wa Tanzania, imetoa msaada wa madawati 200 yenye thamani ya shilingi Milioni 8.3 kwa shule ya msingi Ichenjezya wilayani hapa.

Msaada huo unafuatia maombi yaliyofanywa na mbunge wa jimbo la Mbozi Mashariki Godfrey Zambi (CCM) ya kutafuta misaada ili kupunguza kero kubwa ya uhaba wa madawati unaiyo ikabili shule hiyo iliyopo katikati ya mamlaka ya mji mdogo wa Vwawa.

Msaada huo ulikabidhiwa shuleni hapo na mwakilishi wa kampuni hiyo Peter Chacha, kwa niaba ya Meneja mkuu wa kanda ya mkoa wa Tanzania Abraham Saunyama, ambaye  hakufika katika hafla hiyo kutokana na kukabiliwa na shughuli zingine za kikazi.

Katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa na viongozi wa shule hiyo,viongozi wa  wilaya na idara ya elimu  wakiongozwa na mbunge huyo, Chacha alikabithi jumla ya madawati 50 ambayo alisema ni ya awamu ya kwanza.

Kwa mjibu wa taarifa ya Meneja mkuu, kampuni hiyo itaendelea kutekereza sera za kusaidia sekta mbalimbali za kijamii kwa wananchi ambao bomba hilo limepita jirani kwa sababu wanatoa mchango mkubwa wa kulinda bomba hilo.

Alisema shule hiyo ambayo ipo mita saba jirani na bomba hilo itapewa msaada huo kwa awamu  tatu kabla ya Septemba mwaka huu, ambapo kampuni hiyo itakuwa imekamilisha ahadi yake ya kutoa madawati 200.

Kwa upamde wake Zambi alisema kuwa, anaipongeza kampuni hiyo kwa kukubali ombi lake na kuharakisha kutoa msaada huo ambao utasaidia kupunguza kero ya uhaba wa madawati ambao ni mkubwa shuleni hapo.

Mbunge huyo alisema kufuatia msaada huo ni mategemeo yake kuwa Tazama itakamilisha ahadi yake haraka iwezekanavyo ili kuwanusuru wanafunzi wasiendelee kukaa chini.

Alisema mfuko wa jimbo umechangia shilingi milioni moja na katika mpango wa kuongeza vyumba vya madarasa, mfuko huo utatoa bati zitakazotoshereza kuezeka chumba kimoja kabla ya Juni mwaka huu.

Awali akisoma taarifa ya shule hiyo mwalimu mkuu wa shule  Judica Mongi alisema kuwa,shule hiyo yenye wanafunzi 1814 wakiwemo wasichana 998 ina madawati 110 tu yaliyo chini ya lengo la madawati 604.

Alisema idadi kubwa ya wanafunzi wanakaa chini hivyo kamati ya shule iliyoketi Januari mwaka huu iliazimia  wazazi kutengeneza madawati 378 lakini hadi sasa ni madawati mawili tu yaliyotengenezwa.

Kampuni ya TAZAMA pipelines limited inamilikiwa na nchi mbili za Tanzania na Zambia, ikiwa imepewa jukumu la kusafirisha mafuta yasiyosafishwa kutoka Dar es Salaam hadi Ndola Zambia umbali wa kilometa 1,710.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger