Habari na Ezekiel Kamanga, Chilulumo Mbozi.
Jeshi la Polisi wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya linawashikilia watu Nane kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo tuhuma za kuwabaka ndugu zao .
Hata hivyo wanawake watatu waliobakwa wamefikishwa katika Hospitali ya serikali ya Wilaya hiyo baada ya kutelekezwa na maafisa wa serikali, ambapo Machi 16 mwaka huu walipofika katika kijiji hicho kufanya mkutano wa hadhara na wamesikitika kuachwa hivyo bila kupewa matibabu yoyote.
Miongoni mwa waliolazwa katika hospitali hivi sasa yupo aliyejeruhiwa vibaya kutokana na majeraha na mapanga, ambaye alikuwa akiwanusuru wanawake hao wasibakwe.
Kushikiliwa kwa watu hao kumetokana na vurugu zilizotokea Machi 11 hadi Machi 16, mwaka huu katika kijiji cha Chilulumo wilayani humo kufuatia wananchi kuihoji serikali ya kijiji mapato na matumizi ya fedha za ruzuku hali iliyozua mtafaruku miongoni mwao.
Waliokamatwa katika tukio hilo ni pamoja na katibu kata wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa kata ya Chilulumo Adomari Nakambale anayetuhumiwa kuiba katika stoo ya shule ya kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Mbozi Magharibi Joseph Mwachembe alisema kutokana na tukio hilo ambalo ni la kisiasa limedaiwa kuratibiwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho Bruno Chipungu ambaye alikasirika kuona wananchi wanataka kujua mapato na matumizi ya fedha.
Alisema kabla ya tukio hilo katibu wake wa kata ndiye aliyehoji taarifa ya mapato na matumizi katika mkutano wa hadhara jambo ambalo lilimzulia visa na hatimaye alianza kuharibiwa mali zake likiwemo duka na nyumba yake na kundi la vijana saba wanaodaiwa kutumwa na mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa kufuatia kuharibiwa kwa mali zake katibu huyo alitoa taarifa katika kituo cha polisi cha wilaya hiyo kilichopo Vwawa mjini ambapo alipewa jarada la uchunguzi lenye namba MBO/RB/693/2012&MBO/IR/2012.
Alisema wanashangaa mlalamikaji katika tukio hilo naye anajumuishwa katika vurugu hizo licha ya kutoa taarifa mapema ingawa aliachiwa huru kwa dhamana baada ya kusota rumande kwa zaidi ya masaa 24.
Kwa upande wake katibu kata huyo alipohojiwa kuhusu tukio hilo mara baada ya kutoka rumande alisema anamshangaa Mkuu wa wilaya hiyo Gabriel Kimoro kumjumuisha yeye katika vurugu hizo wakati yeye ni mlalamikaji.
Mkuu wa wilaya ya Mbozi Gabriel Kimoro alisema baada ya kusikia vurugu hizo alikaa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambapo walienda eneo la tukio Machi 16, mwaka huu ambapo waliongea na wananchi na kuwakamata wahusika ambao wako rumande na wanategemea kufikishwa mahakamani (leo) machi 19, mwaka huu.
Alisema chanzo cha vurugu hizo ni masuala ya kisiasa lakini kwa sasa hali ni shwari baada ya yeye kuenda pamoja na kamati nzima ya ulinzi na usalama ya wilaya na kongeza kuwa wanachi ndiyo waliowataja wahusika ambao walikuwa wakifanya vurugu hizo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni katibu kata wa kata hiyo kupitia Chadema Adomari Nakambale, Agnasio Simchimba, Raymund Simfukwe na wengine wawili waliojulikana kwa jina moja moja la Yuda na Agnasio.
Wengine ni Ali Simbeye, Ivod Sambwe na Daniel Simfukwe ambao hadi sasa wako rumande wakisubiri kupelekwa mahakamani.
“ Unajua wananchi hawahudhurii vikao na ndiyo maana wanahoji wakati tayari walikwisha somewa wengine wanaohudhuria vikao hivyo lakini hawa watu pia walitaka kukagua vitabu vya serikali wakati hawaruhusiwi kufanya hivyo na ni kinyume na sheria lakini baada ya mwenyekiti kukataa walimpiga ngumi watu ambao walidhaniwa kuwa ni wa Chadema ndipo hata vijana wa CCM walipojibu mapigo ndiyo vurugu zikaanzia hapo lakini watu tuliowakamata hatukuangalia chama tulichoangalia ni wahusika wa vurugu,” alifafanua Mkuu huyo wa wilaya.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi amethibitisha kukamatwa kwa watu nane kuhusika na vurugu hizo na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya taratibu zote kukamilika.
0 comments:
Post a Comment