Habari na Angelika Sulusi, Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amewataka wakulima Mkoani humo kuandaa vema mazao yao kwa kuyasindika na kufungasha vizuri ili waweze kupanua soko lao kwa bidhaa zao kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Kandoro amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na usindikaji na uuzaji wa mazao ya kilimo, yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wajasiliamali kutoka Wilaya zote za Mkoa huo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benjamini Mkapa.
Amesema kuwa wakulima wengi nchini wanauza mazao yao kwa bei ndogo kutokana na kutoyaanda vizuri kwa uyasindika na kuyafungasha vema, hali inayochangia wakose soko la uhakika pia kuyauza kwa bei ya chini.
Amesema kuwa jitihada za makusudi zinatakiwa kumkwamua mkulima wa Tanzania kwa kumpatia elimu ya ujasiriamali katika uandaaji na fungashaji wa mazao ili aweze kupata bei nzuri hivyo kumudu ushindani wa soko.
Kwa upande wake,Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TBS, Agnes Mneney amesema kuwa Shirika hilo limeamua kutumia fedha zake za ndani ili kuwafundisha wajasiriamali kuhusu ubora wa viwango vya mazao ya kilimo na matakwa ya masoko ya nje ili wakulima waweze kunufaika na mazao yao.
0 comments:
Post a Comment