Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Watu wawili wamefariki dunia mkoani Mbeya katika matukio mawili tofauti likiwemo la la mtu mmoja, aliyefahamika kwa jina la Ganika Ngisi (75) lililotokea katika kitongoji cha Ngyeke Mapinduzi, wilaya ya Kyela mkoani Mbeya baada ya kuuawa na wananchi wenye hasira kali.
Chanzo cha mauaji hayo ni tuhuma za kichawi kwani mara kadhaa alikuwa akituhumiwa na tuhuma hizo, na uchunguzi unaendelea kufanyika ili kuweza kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu wawili ambao ni Amon Benson (30) na Amani Angolile (31) wote wakazi wa Ipinda wilayani humo kwa mahojiano.
Katika tukio jingine Shadi Mwamtobe (20), mkazi wa mtaa wa Soko kata ya Ruanda, amefariki baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni wakati akicheza mwenzake pembezoni mwa ukuta wa hoteli ya Mfikemo, iliyopo Kata ya Ruanda jijini Mbeya.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 7 mchana na kufariki wakati akifanyiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa, Mbeya.
Wakati huo huo Jeshi la polisi linawashikiria watu wawili kwa kujihusisha na biashara haramu ya pombe ya moshi (Gongo), Kissa Hajangwa (50) mkazi wa Itenzi jijini hapa, ambaye amekamatwa akiwa na lita 4 za gongo. Pia Helena Kasege (45) ambaye amekamatwa kwa tuhuma za kumiliki mitambo ya kutengenezea pombe hiyo.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Advocate Nyombi amethibitisha matukio yote na kwamba watuhumiwa wote wawili wapo mahabusu.
0 comments:
Post a Comment