Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Katika hali isiyo ya kawaida wakazi wa kijiji cha
Matamba kata ya Isange wilayani Rungwe mkoani Mbeya wamemfukuza kazi afisa
mtendaji wa kijiji hicho na kumpachika madaraka mwananchi wa kawaida kushika
wadhifa huo.
Uamuzi huo umefikiwa jana wakati wa kikao cha
kijiji kilichoketi kujadili hali ya maendeleo ya kijiji hicho ambapo,
ilibainika kuwa afisa mtendaji alihusika na wizi wa shilingi milioni moja na
laki sita, kujimilikisha saruji za wananchi zilinunuliwa kwa ajili wa ujenzi wa
shule ya Sekondari ya kata na kutumia vibaya madaraka.
Aidha wananchi hao walimchagua Fomen Mwandembo
ambaye ni mwananchi wa kawaida kukaimu wadhifa huo hadi hapo Serikali itakapo
mleta afisa mtendaji mwingine.
Mwenyekiti wa kijiji hicho John Mwakyoma amesema
kuwa huamuzi huo hauwezi kupingwa kutokana na kwamba imekuwa ni tabia ya
maafisa watendaji kujimilikisha mali
za umma pasipo kuchukuliwa hatua zozote.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Isange Eliasi
Mwasambili amesema kuwa baada ya tukio hilo
walikubaliana kumwamisha kituo cha kazi afisa huyo badala ya kumfukuza.
Kwa mujibu wa sheria za nchi afisa mtendaji
huajiliwa na hapatikani kwa njia ya uchaguzi, hivyo kitendo hicho ni kinyume na
sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana
Mwakyoma amesema anayabariki maamuzi ya wananchi kwani mtendaji huyo wamemuonya
mara nyingi lakini lakini amekuwa akikaidi na kudhoofisha nguvu za wananchi na
maendeleo kwa ujumla kijijini hapo.
0 comments:
Post a Comment