Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Sindano ya ganzi yamsababishia mauti mtoto
Tumaini Rataniel Mtajiha (5), mkazi wa Kijiji cha
Hagomba Kata ya Itaka baada ya kuchomwa na daktari wa zahanati binafsi ya
Sisika, inayomilikiwa na mwalimu mmoja katika Mtaa wa Ichenjezya, Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya.
Tukio hilo
la kusikitisha limetokea Aprili 22 mwaka huu majira ya saa tano asubuhi baada
ya mtoto huyo kufikishwa katika Zahanati binafsi, akiwa na jipu katika makalio ndipo
Daktari alipompokea na kumtoza shilingi 20,000 baba mzazi wa marehemu Bwana
Rataniel Mtajiha (45), ili apewe huduma.
Sababu ya kuchomwa sindano ya ganzi ni kutokana na
mtoto huyo kuonaonekana ni mwoga hivyo achomwe sindano hiyo, na baada ya kuchomwa
mtoto huyo alifariki papo hapo.
Baada ya tukio hilo Bwana Mtajiha
alitoa taarifa Kituo cha
Polisi Vwawa, ambapo walifika na kumchukua Daktari huyo (Jina
linahifadhiwa), mwili wa mtoto na jalada lake pamoja na sampuli ya dawa
alizotumia hadi
kwenye Hospitali ya Wilaya ili kufanyiwa uchunguzi majira ya saa 10:00
jioni.
Aidha, baada ya kutafakari kwa kina Hospitali hiyo
ya wilaya, walitoa taarifa mkoani na kuagiza mwili ufanyiwe uchunguzi Aprili 23
mwaka huu, baada ya jopo la mkoani kuwasili wilayani Mbozi ili kufanya
uchunguzi wa kina.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoani Mbeya hakuweza
kupatikana kuthibitisha tukio hili, na hivi sasa Daktari wa Zahanati hiyo
anashikiliwa na Kituo cha polisi Vwawa akisubiri uchunguzi kufanyika.
Wakati huo huo baba mzazi Bwana Mtajiha, amesema
hakutegemea mwanae kufikwa na mauti kwani, muda wote alikuwa anacheza licha ya kukabiliwa na jipu hilo.
0 comments:
Post a Comment