Habari na Angelica Sullusi, Mbeya
Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 2.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya, Juliana Malange wakati akiwasilisha bajeti ya Halmashauri hiyo katika kikao maalum cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni kwa ajili ya kujadili rasimu ya bajeti ya halmashauri hiyo.
Amesema kati ya fedha hizo, shilingi Bilioni 1.67 zitatumika kwa ajili ya miradi ya kuwafikishia wananchi maji katika maeneo yao na shilingi milioni 34.2 zitatumika kwa ajili ya usimamizi wa miradi hiyo.
Amesema sambamba na bajeti hiyo Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto la UNICEF limeahidi kutoa shilingi milioni 520 kwa ajili ya kuboresha za maji na usafi wa mazingira mashuleni.
Wakichagia hoja wakati wa kujadili bajeti hiyo, baadhi ya madiwani wamesema kuwa huduma za upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo sio za kuridhisha na hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
Madiwani hao wamesema kuwa mji mdogo wa mbalizi unastahili kupewa kipaumbele katika suala la upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira, kwa kuwa mji huo ndio kioo cha halmashauri na chanzo kikuu cha mapato yanayokusanywa na halmashauri hiyo.
0 comments:
Post a Comment