Pages


Home » » WAKULIMA WA ZAO LA KAHAWA WAANZA KUKUTANA KUBORESHA

WAKULIMA WA ZAO LA KAHAWA WAANZA KUKUTANA KUBORESHA

Kamanga na Matukio | 04:59 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Muungano wa Vikundi vya wakulima wa zao la Kahawa Wilaya ya Mbozi, Mkoani Mbeya (MVIKAMBO), wameanza ziara katika Kata mbalimbali za wilaya hiyo kwa lengo la kuboresha uzalishaji wa zao hilo, licha ya kuzalisha kahawa nyingi ambazo hazina ubora na kutonufaika nayo.

Hayo yamebainishwa siku ya kwanza ya ziara hiyo iliyochukua siku saba na kuanzia katika Kata ya Nambizo na Itaka, ambapo msimamizi wa zao hilo katika wilaya hiyo Bwana Francis Kabale amesema kumejitokeza kwa tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wa zao hilo kutokuwa waaminifu.

Msimamizi huyo amepinga vikali uuzaji wa Kahawa mbichi (Chery), na kwamba mkulima yoyote atakayebainika kukiuka agizo hilo atafikishwa mahakamani, ili kujipu shtaka la kukiuka.

Bwana Kabale amewataka wakulima kuanika zao hilo katika vichanja badala ya kuanika chini, ambapo kahawa huchanganyika na uchafu hali inayopunguza ubora kwenye soko la dunia kuwa na soko duni licha ya kuwa na ladha.

Hata hivyo Mwenyekiti wa MVIKAMBO Bwana Fred Mgala amesema wanunuzi holela huwarubuni wakulima kwa kununua kahawa kwa bei ya chini shambani (kukata kichwa), kitu ambacho humtia hasara na kutonufaika kwa chochote, jambo linalomfanya mkulima kuendelea kunyanyasika.

Kwa upande wake mwakilishi wa Bodi ya Kahawa nchini (TCB) bwana Jimmy Mchau, amesema kwamba hayupo tayari kuidhinisha kahawa chafu itokayo wilayani humo ili kahawa hiyo kutoka daraja la 9 la hivi sasa na kufikia daraja la 5 ili kupata soko la kimataifa, na kwamba sababu zinzopelekea katika daraja la sasa zinaweza kuepukika.

Katika mkutano huo Taasisi ya utafiti wa zao la Kahawa (TACRI), Kituo cha Mbimba Mbozi kiliwakilishwa na Bwana Dismas Pancras ambaye amesema miche bora ya zao hilo inapatikana katika shamba darasa lililopo Kata ya Itaka hivyo wakuliMA wafike eneo hilo kujipatia miche hiyo.

Wakati huo huo mtoa mafunzo wa Shirika la INADEA Bwana Pascal Lala amesema asasi yake inatoa mafunzo kwa wakulima na uongozi kwa gharama ndogo sana ili kuwawezesha wakulima na viongozi kufanyakazi kwa ufanisi, matharani kutoa vitabu 9 kwa mafunzo ya wakulima kwa gharama ya shilingi 3,500 na shilingi 4,000 kwa mafunzo ya uongozi ambapo hupata vitabu 7.

Kata zitakazonufaika na mpango huo wa mafunzo ni Nambizo, Itaka, Bara, Harungu, Msia, Igamba na Isansa, nyingine ni Ruanda, Iyula, Mlangali, Nyimbili, Isandula na Ihanda, ambapo mafunzo yatahitimishwa Aprili 19 mwaka huu na wakulima wameushukuru uongozi wa MVIKAMBO kwa kuwafungua.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger