Pages


Home » » DC MBEYA AWATAKA MADEREVA WA MAGARI YA ABIRIA NA MIZIGO KUJIENDELEZA KIELIMU

DC MBEYA AWATAKA MADEREVA WA MAGARI YA ABIRIA NA MIZIGO KUJIENDELEZA KIELIMU

Kamanga na Matukio | 03:04 | 0 comments
Habari Angelica Sullusi, Mbeya.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama amewataka madereva wa magari ya abiria na mizigo nchini kuhakikisha wanajiendeleza kielimu ili kuwa na taaluma ya kutosha katika fani hiyo kwani ndio wadau wakubwa katika suala zima la usalama wa raia na mali zao.

Balama amesema hayo wakati akifungua kongamano la madereva wa Mkoa wa Mbeya lililoandaliwa na Chama cha Madereva Tanzania (TDA) tawi la Mbeya kwa kushirikiana na Shirika la usalama la PTA lenye makao yake makuu Jijini Dar es Salaam.

Aidha,amewataka madereva hao kukataa kuendesha chombo cha usafiri  ambacho ni kibovu na kisichokuwa na bima kwa ajili ya kulinda usalama wao na kupunguza ajali zisizo za lazima wawapo barabarani.

Amesema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa na tabia ya kukubali kuendesha barabarani vyombo vibovu na kujikuta vyombo hivyo vikiwaharibikia wakiwa katika mwendo mkali na hivyo kuwa chanzo cha ajali isiyokuwa ya lazima na kusababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali zenye thamani.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi,Mwenyekiti wa chama cha Madereva Mkoa  wa Mbeya, Proterce Chrispine amesema kuwa kongamano hilo limeandaliwa na TDA kama sehemu ya mkakati wa kupunguza ajali za barabarani mkoani Mbeya.

Amesema kuwa Mkoa wa Mbeya umekuwa na ajali nyingi za barabarani ambapo kwa mwaka jana 2011 zilitokea ajali zaidi ya 2800 zilizosabisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za wananchi, huku akidai kuwa  katika  mwezi Oktoba pekee mwaka jana zilitokea ajali 325.

Kwa upande wake Afisa wa Shirika la PTA, Fanuel Sabini amesema kuwa madereva ni wadau wakubwa katika suala zima la usalama wa raia na mali zao hivyo ni vema wakashirikishwa katika mambo mbalimbali ya kiusalama.

Semina hiyo ya madereva wa magari, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri imefanyika Jijini Mbeya kwa lengo la kuanzisha mkakati wa kupunguza ajali mkoani hapa.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger