Habari na Ezekiel Kamanga, Mbozi.
Watu wawili wamefariki katika matukio mawili tofauti, likiwemo la mtu mmoja kula kande za moto na jingine la kujinyonga katika Wilaya ya Mbozi, Mkoani Mbeya.
Tukio la kwanza limetokea katika Kitongoji cha Mtanila, Kata ya Mlowo, ambapo Said Mnyasa (40), amefariki baada ya kunywa gongo kisha kutafuta supu ya makongoro baada ya kuikosa supu hiyo alikwenda kwa Mama Ntilie anayeuza Kande na kupakuliwa kande hizo za moto.
Baada ya kula kande hizo marehemu alianguka chini na kufariki dunia papo hapo majira ya saa tatu asubuhi, Aprili 12 mwaka huu na mazishi yake kufanyika majira ya saa kumi jioni katika kitongoji hicho.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Bwana Bruno Mwambene amesema kuwa marehemu amekuwa na tabia ya kunywa pombe haramu aina ya gongo na wakati bila hata kula chakula hali iliyomsababishia mwili wake kudhoofu.
Wakati huo huo Tatizo Mwasenga mkazi wa kijiji cha Insani, Kata ya Isansa wilayani humo amefariki baada ya kujinyonga nyumbani kwa wazazi wake kwa kutumia kamba aina ya katani.
Aidha tukio hilo limetokea majira ya saa nane mchana Aprili 12 mwaka huu mtaa wa Ilembo Vwawa mjini alipokwenda kuwatembelea wazazi wake. Marehemu alikuwa akifanyakazi ya kutengeneza pombe ya ndizi (Banana Wine) kwa tajiri aitwaye Bartazar Malya mkazi wa Mlowo.
Hata hivyo sababu za kifo chake hazijaweza kupatikana na Jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa matukio yote mawili na mpaka sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi hilo.
0 comments:
Post a Comment