Pages


Home » » WATU WAWILI WAUAWA KIKATILI MKOANI MBEYA.

WATU WAWILI WAUAWA KIKATILI MKOANI MBEYA.

Kamanga na Matukio | 06:35 | 0 comments
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi.
*****
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Watu wawili wameuawa kikatili mkoani Mbeya baada ya watu wasiofahamika kuvamia nyumba zao katika matukio mawili tofauti.

Tukio la kwanza limetokea Kitongoji cha Katabe, Kijiji cha Katabe, Kata ya Katumba, wilayani Rungwe Januari 7 mwaka huu, usiku wa manane saa 9 ambapo Mama Sabina Kyani mwenye umri wa miaka 50 ameuwawa na watu wasiojulikana baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana kisha kumkatakata na mapanga sehemu za mwili wake ikiwemo kisogoni na marehemu alikuwa akiishi na mabinti wawili ambao pia walijeruhiwa vibaya.

Mwenyekiti wa kijiji cha Katabe Bwana Danford Mwakatika amesema majirani wa marehemu huyo walisema walisikia sauti ya yowe toka kwenye nyumba ya marehemu ndipo walipoamka pamoja na walipofika eneo la tukio walikuta tayari watu hao wameondoka na wameshafanya mauaji hayo.

Walisema baada ya kukuta hali hiyo waliamua kuwakimbiza majeruhi katika hospitali ya wilaya ya Rungwe (Makandana) ambao ni mabinti wa marehemu ambapo mmoja hakufahamika jina lake mara moja na mwingine alijulikana kwa jina la Martha Mwakabuta (30) na kisha kutoa taarifa polisi.

Aidha imeelezwa kuwa tukio hilo ni la pili kutokea katika nyumba hiyo ambapo Desemba 29, mwaka uliopita inasadikiwa watu hao hao walivamia nyumba hiyo wiki moja iliyopita na kumjeruhi binti huyo huyo ambaye alilazwa katika hospitali ya Wilaya na baada ya kuruhusiwa ndipo limetokea tukio hilo tena.

Polisi walifika  eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka katika hospitali ya Wilaya ya Rungwe kwa ajili ya kuuhifadhi  ambapo  marehemu alikutwa na jeraha kisogoni.

Katika tukio lingine Benny Simsanga (24) mkazi wa Majengo mapya katika mji mdogo wa Tunduma Wilaya ya Mbozi Mkoani hapa alikutwa amekufa baada ya kuuawa na watu wasiojulikana juzi majira ya saa nne usiku na kisha mwili wake kutelekezwa eneo la Chianga mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni Afisa mtendaji wa mtaa wa Majengo Yonah Simfukwe alisema marehemu alivamiwa na kuawa na watu hao na kumpora pikipiki aliyokuwa akimiliki pamoja na pesa ambazo kiasi chake hakijajulikana .

Aliongeza kuwa marehemu alikutwa na majeraha kichwani ambapo polisi wa pande zote mbili walifika eneo la tukio na hatimaye mwili wa marehemu kuchukuliwa na askari wa Tanzania baada ya kuthibitisha uraia wake na kuhifadhi katika kituo cha afya cha Tunduma.

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Mbeya Advocate Nyombi alilithibitisha kutokea kwa matukio yote mawili na upelelezi bado unaendelea kuwasaka wauaji na kubaini vyanzo vya matukio hayo ambavyo bado havijajulikana.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger