Habari na Mtandao huu, Mbeya.
Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imeunda kamati ndogo ya watu 10 itakayoandaa mikakati ya kuhakikisha hamasa ya mfuko wa afya ya jamii CHF inatolewa kwa wananchi ili waweze kujiunga kwa wingi.
Kamati hiyo imeundwa na mkuu wa wilaya Jackson Msome aliyekubaliana na wadau wengine waliohudhuria mkutano wa wakuu wa Idara za halmashauri hiyo wa kupata taarifa za maendeleo ya CHF na pia kujadili mradi mpya wa kuwasaidia wanawake wajawazito wasio na uwezo kupata huduma za matibabu chini ya utaratibu wa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF.
Msome amesema ili kuhamasisha wananchi kujiunga kwa wingi ni lazima mikakati madhubuti iwekwe ikiwemo utoaji elimu kwa wakazi juu ya kuwa na bima itakayowahakikishia huduma ya afya pale wanapopata matatizo ya magonjwa.
Awali akizungumzia sababu za wananchi waliokuwa wamejiunga na mfuko huo kujitoa,mganga mkuu wa wilaya Dokta Sungwa Ndagambwene alisema baadhi walikatishwa tama na kasoro zilizobainika ikiwemo uhaba wa dawa jambo ambalo alisema hivi sasa limewekewa mikakati tofauti na kipindi hicho.
0 comments:
Post a Comment