Pages


Home » » UCHAMBUZI:- MIGOGORO YA WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI IMEKUWA IKIKWAKISHA SHUGHULI ZA MAENDELEO - MBEYA.

UCHAMBUZI:- MIGOGORO YA WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI IMEKUWA IKIKWAKISHA SHUGHULI ZA MAENDELEO - MBEYA.

Kamanga na Matukio | 05:09 | 0 comments
Ester Macha, Mbeya.
Chanzo cha migogoro mingi kati ya wananchi na watendaji wa kata na vijijini Mkoani Mbeya  imekuwa sababu mojawapo ya kukwamisha shughuli za maendeleo kama vile ujenzi wa shule za msingi na sekondari, Zahanati,Malambo.

Kwa hali hii nimelazimika kuandika uchambuzi huu kwa uchungu kutokana na na jinsi maendeleo yanavyoshindwa kusonga mbele kutokana na watendaji wasiokuwa waadilifu katika michango ya wananchi ambayo wanajitolea kwa ajiri ya kuchangia shughuli za maendeleo na wao kuamua kujinufainisha na fedha za wananchi huku miradi ya wananchi ikishindwa kuendelea kwa uzembe wa watu wachache ambao hawana uchungu na fedha hizo.

Katika Mkoa wa Mbeya kumekuwepo na migogoro ya mara kwa mara kwa wananchi na watendaji  wa kata na vijiji  kwa muda mrefu sababu ikiwa ni ufujaji wa fedha za wananchi pale wananchi wanapohoji uhalali wa kuliwa fedha hizo hutokea ugomvi mkubwa kwanini wananchi wahoji .

Tatizo la watendaji wa kata na vijiji kukwamisha shughuli za maendeleo limekuwa kikwazo cha maendeleo  kwa Mkoa wa mbeya ambapo hali hiyo imesababisha wilaya zingine wananchi kukataa kuchangia shughuli za maendeleo kutokana na kutosomewa mapato na matumizi kwa viongozi hao  na hata kutoona kinachofanywa licha ya wananchi kutoa michango yao ili kusaidia maendeleo.

Wilaya ambao zimekuwa kiini cha migogoro kati ya wananchi na watendaji wa kata na vijiji ni Wilaya ya Mbarali ambayo kwa muda mrefu imekuwa na matatizo makubwa ya michango inayotolewa na wanananchi ili iweze kusaidia ujenzi wa shule za sekondari za kata, zahanati lakini matokeo yake yamekuwa si mazuri kimaendeleo.

Kutokana na hali hiyo Mbunge wa Jimbo la Mbeya Bw. Dicksoni Kirufi alifanya mikutano katika kata za wiloaya hizo na kuonekana kuwa kuna tatizo la ufujaji wa fedha zinazochangwa na wananchi  na kutosoma mapato na matumizi huku fedha hizio zikiendelea kutumika pasipo kusoma taarifa yeyote.

Lakini kutokana na hali hiyo kuwa mbaya ilimlazimu mbunge huyo kwataka wananchi kutotoa michango yeyote ya maendeleo mpaka pale watakaposomewa mapato na matumizi ya fedha  ya fedha wanazotoa kwa ajiri ya  kusaidia maendeleo.

Baada  ya kutoa angalizo hilo wananchi wakawa na msimamo wa pamoja na kwamba pale walipofuatwa na watendaji wa vijiji na kata walikataa kuchanga michango ya maendeleo wakitaka kusomewa mapato na matumizi ya michango iliyoppita kuwa imefanya kazi gain, na ndipo ilipoibuka migongano kati ya wananchi na watendaji hao.

Kutokana na mtafararuku huo Watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali waliibuka katika kikao kimoja cha kamati ya ushauri cha Mkoa wa Mbeya wakituhumu hatua ya Mbunge  huyo kuwa amekwamisha ujenzi wa vyumba 34 vya madarasa wilayani humo ambavyo vilitakiwa vitumike mwaka 2012.

Nionavyo watendaji wakuu wa halmashauri ilitakiwa kukaa na watendaji wao wa kata na vijiji kuwafahamisha umuhimu kusoma mapato na matumizi kwa wananchi wao kwani hali imekuwa sugu kwa wilaya hiyo ambapo watendaji wamekuwa wakiamua kufuja michango ya wananchi pasipo viongozi wa halmshauri kuchukua hatua zozote kwa watendaji hao.

Nasikia tu oho watendaji wa kata na vijiji ambao watabainika kufuja michango ya wananchi au kutosoma mapato na matumizi tutawachukulia hatua, hayo yamekuwa ni maneno ya kawaida pasipo kuona vitendo kwa wahusika na ndo maana nao wameona ni kitu cha kawaida kukemewa pasipo utekelezaji wowote.

 Ninachojiuliza kwa nini hawa watendaji wa kata na vijiji wamekuwa miungu watu licha ya kuwa wanafuja michango ya wananchi lakini hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao tatizo nini kwa watu hawa na tujue kwanini wanaamua watakacho wakati  michango hiyo inatolewa na wananchi ili kusaidia shughuli za maendeleo iweje watendaji wa kata wachukue maamuzi yao.

Nasema hivyo kutokana na malalamiko kutoka wananchi ambayo yamekuwa hayana suluhu yeyote licha ya watendaji hao kuhusishwa na tuhuma hizo lakini cha kushangaza uongozi huo umekuwa ukifumbia macho tatizo  hilo na kudai watuhumiwa bado wanachungwa na hata muda mwingine watendaji hao huhamishiwa kata zingine ili kuwasahaulisha wananchi na kuletewa mtu mwingine.

Kwanini mtendaji wa kata akigundulika kufuja michango ya wananchi kwanini ahamishiwe kata nyingine badala ya kufukuzwa kazi ili fundisho kwa watendaji wengine  wenye tabia kama hizo wasiwe na uroho wa kufuja michango ya wananchi.

Nasema hivi kwasababu ikitolewa adhabu kama hiyo ya kuwafukuza kazi itakuwa ni adhabu tosha kuliko kuwapeleka kata zingine kufanya kazi kwani hata kule akienda utakuwa mtindo ule ule hivyo hakutakuwa na suluhu yeyote katika kutatua tatizo hili la michango ya wananchi ambalo limekuwa ni kero kubwa ambayo ni sugu na kuisha kwake ni  watendaji wakuu wa halmshauri kuingilia kati suala hili.

Karibu wilaya zote za Mkoa wa Mbeya zimekuwa  na migogoro ya wananchi na watendaji kata na vijiji juu ya michango ya wananchi kwanini dawa isipatikane kwa watu hawa ili shughuli za maendeleo ziendelee pasipo vikwazo vya watu hawa.

Kwa matatizo haya mafanikio hayawezi kupatikana mfano wilaya ya Mbarali  imekuwa na migogoro mikubwa inayohusu michango ya wananchi ,kwa kata ya Ruiwa karibu mil.20 zimeliwa, kata ya Utengule usangu mil.34, kata ya Ipwani mil.2, luango, lakini kati ya watendaji hawa ni mmoja tu ambaye amefikishwa mahakamani ambaye hata hivyo kesi yake ina zengwe zengwe tu inaendeshwa huku mtuhumiwa akiendelea kupata mshahara wake kama kawaida.

Kwa upande wa hawa wengine wamehamishwa kutoka kwenye kata zingine ambako nako walishafuja fedha za wananchi sasa kwanini viongozi hawa wa halmshauri wafanye hivi ina maana wanafurahia kitendo kinachofanywa na watendaji hawa ambao wamekuwa mstari wa mbele kukwamisha maendeleo.

Kufuatia hali hiyo kukithiri Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw.Abbas Kandoro ametoa agizo kwa watendaji wote wa kata na vijiji kuwa ifikapo Desemba 30 mwaka huu wawe wamesoma mapato na matumizi kwa wananchi wao kabla Mkuu huyo wa Mkoa hajapita kwenye kwenye kata na vijiji kukagua vitabu na kuongea na wananchi kujua kama wamesomewa mapato na matumizi na watendaji hao.

Nionavyo ni kweli Bw. Kandoro amesema hilo na tunachohitaji ni utekelezaji kwa watendaji hao kwani viongozi wengi wa mkoa wamekuwa wakikemea  ufujaji wa michango ya wananchi na kutosoma mapato na matumizi lakini hilo limekuwa ni sawa na hakuna  kwani hakuna anayeshtuka juu ya onyo hilo.

Kwasababu Bw.Kandoro ni kiongozi anayependa maendeleo naamini kuwa  suala hili ambalo limekuwa ni tatizo sugu kwa muda mrefu litaweza kupatiwa ufumbuzi wa kina.

Mimi naamini kwamba agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya litafanyiwa kazi kwa mapana zaidi na hata kama halitafanyiwa kazi basi itafutwe dawa nyingine ambayo itakuwa mualobaini kwa watendaji wa kata na vijiji ambao wamekuwa wakijinufainisha na michango ya wananchi pasipo kufahamu kuwa wananchi wanalima vibarua ili waweze kupata michango kwasababu wana uchungu na maendeleo na wanataka watoto wasome.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger