Pages


Home » » MAAFA:- MVUA ILIYOAMBATANA NA UPEPO MKALI NYUMBA 24 ZABOMOKA. - MBEYA

MAAFA:- MVUA ILIYOAMBATANA NA UPEPO MKALI NYUMBA 24 ZABOMOKA. - MBEYA

Kamanga na Matukio | 06:22 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga, Chunya.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imebomoa nyumba 24 katika Kata ya Ifumbo, wilayani Chunya mkoani Mbeya na kusababisha baadhi ya wananchi kuwapa hifadhi waathirika wa janga hilo kutokana na kuharibiwa kabisa nyumba zao.

Hayo yamebainishwa na Diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Michael Zanzi ambaye amesema licha ya nyumba hizo kubomolewa pia mimea ya mazao iliyojitokeza nje ya ardhi hivi karibuni imeharibika baada ya kufukiwa na maji ya mvua.

Naye Afisa Kilimo wilaya ya Chunya Bwana Michael Mwankenja ambape pia ni Mkuu wa Kitengo cha maafa inaharakisha kupeleka mbegu za mtama tani 12, kwa ajili ya kupanda ili kuwawezesha wananchi hao kukabiliana na njaa mwakani.

Hata hivyo amewaomba wananchi  waliopo maeneo ya mabonde kuhama kutokana na ushauri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ambayo imesema kutakuwa na mvua kubwa katika Ukanda wa Nyanda za Juu.

Pia katika Kata ya Kanga wilayani humo mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana majira ya saa kumi jioni imesababisha mto Zira kujaa maji na kupelekea mashamba ya wakazi wa kijiji hicho kufunikwa na maji.

Kwa upande wake diwani wa Kata hiyo amesema kuwa hakuna mtu aliyefariki dunia wala kubomoka kwa nyumba yake isipokuwa kipande cha barabara chenye urefu wa mita 200 kimeharibiwa na mvua hizo.

Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Chunya amesema ofisi yake ilitoa tahadhari Novemba 5, mwaka huu kwamba wananchi wahame katika maeneo yoevu(mabondeni) ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea katika  msimu huu wa mvua.

Mkuu wa wilaya ya hiyo Bwaba Deodatus Kinawiro amewatembelea waliofikwa na maafa hayo na kuwataka wananchi kusaidiana ili kuwapa hifadhi watu waliofikwa na janga hili wakati wakifanya utaratibu wa kuzikarabati nyumba zao.

Mwezi Novemba mvua kubwa zilizoanza kunyesha kata ya Galla ilisababisha maafa kwa wananchi wa kata hiyo ambapo ofisi ya Waziri mkuu, kitengo cha maafa iliweza kutoa msaada wa hali na mali kwa wananchi hao.




Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger