Pages


Home » » WAWILI WAFA KWA MOTO NA MAJI, GARI LATEKETEA MKOANI MBEYA

WAWILI WAFA KWA MOTO NA MAJI, GARI LATEKETEA MKOANI MBEYA

Kamanga na Matukio | 06:17 | 0 comments
Na mwandishi wetu.
Watu wawili wamefariki katika matukio mawili tofauti mkoani Mbeya, ambapo tukio la kwanza Utaratibu wa kujichukulia Sheria mikononi unaendelea kutawala hususani mtaa wa Mwanyanje, Kata ya Igawilo baada ya mwananchi mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja kupigwa na kisha kuchomwa moto ambao uliteketeza mwili wake. 

Mtu huyo alituhumiwa kuwa ni mwizi licha ya kutofahamika alichoiba au aliyeibiwa kijijini hapo aliteketezwa kwa moto katikati ya barabara, nyumbani kwa balozi wa mtaa aitwaye Bwana Albert Mwalyego kwa kutumia kuni na mbao ambazo zilivunjwa katika kibanda cha mjasiriamali kilichokuwa karibu na tukio hilo.

Balozi wa mtaa Mwalyego alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa huo Bwana Elia Jerema ambaye amesema tukio hilo limetokea majira ya usiku wa manane na kwamba kutokana na hali ya mvua hakuweza kusikia kelele za aina yoyote mpaka majira ya asubuhi wakati akiamka alifanikiwa kushuhudia mwili ukimalizika kuteketea na moto, na kisha mwenyekiti huyo kutoa taarifa kituo cha Polisi Uyole.

Tukio la pili mwili wa Mzee Rashid Gervas (61), ulikutwa katika dimbwi lililo pembeni mwa Shule ya Msingi Moto Moto Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoani mbeya.

Marehemu Rashid alitoweka Nyumbani kwake Jumamosi ya Desemba 10, mwaka huu na kupatika siku iliyofuata akiwa ameaga dunia dimbwini humo. Marehemu kabla ya kifo chake alionekana katika Kilabu cha Pombe akiwa na Redio yake pembeni  mwa dimbwi.

Aidha watu wasiofahamika wilayani Mbarali wamechoma gari lenye nambari T 574 BFD  aina ya Canter mali ya Afisa mtendaji wa Kata ya Ruiwa Bwana Jordan Masweve majira ya saa sita usiku wa kuamkia Desemba  11, mwaka huu.

Bwana Jordan ameshitushwa na kishindo kilichotokea usiku huo na alipotoka nje akashuhudia matairi ya nyuma ya gari lake na turubai vyote vikiteketea kwa moto na kukuta mabaki ya petroli na mabaki ya plastiki.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kwamba jeshi lake linafanya uchunguzi ili kuweza kubaini watuhumiwa wa matukio hayo.
 
 
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger