Pages


Home » » Wanafunzi zaidi ya 120 wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey, hawataweza kufanya mitihani yao ya mwisho kutokana na taarifa zao kutokuwepo Wizarani.

Wanafunzi zaidi ya 120 wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey, hawataweza kufanya mitihani yao ya mwisho kutokana na taarifa zao kutokuwepo Wizarani.

Kamanga na Matukio | 02:33 | 0 comments
Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey Jijini Mbeya.
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
 Wanafunzi zaidi ya 120 wa Mwaka wa Pili wa Chuo cha Uuguzi cha Aggrey kilichopo Mwanjelwa Jijini Mbeya ndoto za kuwa Madaktari na Wauguzi bora zimezidi kuyeyuka baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa hawataweza kufanya mitihani yao ya mwisho kutokana na taarifa zao kutokuwepo Wizarani.
 
Taarifa hizo zilibainika juzi baada ya Wanafunzi hao kukusanyika nje ya Majengo ya Chuo hicho wakitaka kuandamana kuelekea kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ili kumweleza madai yao ya muda mrefu ambayo yameshindwa kujibiwa na uongozi wa chuo hicho.
 
Moja ya madai ya wanafunzi hao waliyokuwa wanataka kumweleza Mkuu wa Mkoa kama wangekuwa wamepata Kibali ni pamoja na kutotambuliwa na Baraza la Wauguzi Tanzania (Midwives Councils)ambapo usajili wake haujafanyika Licha ya Uongozi wa Chuo kukiri kuwa wanaendelea kulifanyia kazi na kulitafutia ufumbuzi.
 
Madai mengine ni kurejeshewa fedha za Mafunzo ya Vitendo ambazo walichangia na ambazo walitakiwa kupewa kabla ya kwenda kufanya mazoezi hayo kama fedha za kujikimu, vitabu vya rejista ambavyo vilileta gumzo na kusababisha hofu na hatma ya wanafunzi baada ya Uongozi wa Chuo kushindwa kuthibitisha namna ya upatikanaji wa vitabu hivyo kutoka Wizarani.
 
Kutokana na mkasa huo Uongozi wa Chuo ulipotakiwa kuwaeleza wanafunzi mwenye jukumu la kuleta vitabu Chuoni alisema havipatikani bali wanachofanya ni kuchukua kwenye mitandao na kuvichapisha kwa madai kuwa Wizarani havipatikani kabisa hali iliyosababisha vurugu na mabishano makubwa.
 
Wanafunzi hao walidai kuwa uongozi haujui lolote hivyo wanawaongopea kwa sababu badhi ya wanafunzi walifika Wizarani na kuuliza juu ya upatikanaji wa vitabu hivyo na kujibiwa kuwa anayetakiwa kufuata vitabu hivyo Wizarani ni Chuo na si vinginevyo ambapo waliongeza kuwa baada ya kutoka Wizarani walirudisha majibu kwa Uongozi wa Chuo ambao umeshindwa kulifanyia kazi.
 
Kutokana na utata huo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbeya alimwamuru Makamu Mkuu wa Chuo hicho kuthibitisha ukweli wa madai ya wanafunzi haokuhusu kwenda Wizarani na kupewa majibu kisha kuwaletea jambo ambalo alishindwa kulijibu na badala yake aliamua kupiga Simu Wizara ya Afya  na Ustawi wa Jamii kitengo cha Mafunzo.
 
Simu hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Wizara ya Afya aliyejitambulisha kwa jina moja la Dk. Mwamasage ambapo Simu hiyo iliwekwa sauti ya Juu (Loud Speaker) iliyokuwa ikisikika na wanafunzi, Wanahabari pamoja na Askari wa Jeshi la Polisi waliofika kutuliza ghasia Chuoni hapo.
 
Mkurugenzi huyo alisema Suala la kufuata vitabu ni la viongozi wa Chuo na Si vinginevyo na kuongeza kuwa vitabu hivyo vinapatikana na kuna kampuni inayofanya kazi ya kuchapisha ambako Chuo kinatakiwa kufuata vitabu hivyo.
 
Maongezi hayo ya Simu yalisema pia Uongozi wa Chuo hicho haufuati taratibu za uendeshaji wa Chuo na kufanya kazi za ubabaishaji ambapo aliongeza kuwa Wizara haitambui kama Chuo hicho kimeanza kufanya kazi na kama kuna wanafunzi wanaotakiwa kufanya mtihani Mwezi Agost Mwaka huu kutokana na Uongozi wa Chuo hicho kutopeleka Orodha ya Majina ya wanafunzi Wizarani.
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa  Mafunzo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii alisema ili wanafunzi waweze kuruhusiwa kufanya mitihani ilitakiwa Chuo kupeleka usajili wa wanafunzi kabla ya Mwezi Machi Mwaka huu lakini kipindi hicho kimeshapita hivyo uwezekano wa kufanyika kwa Mtihani wa Nacte ni mdogo.
 
“ Sikia nikwambie OCD hicho chuo ni wababaishaji na hawataki kufuata taratibu za kuendesha Chuo hata hivyo Wizarani hatuna taarifa kama kuna Wanafunzi wanaotakiwa kufanya Mitihani Mwaka huu” Ilisikika Sauti kutoka katika Simu aliyokuwa akisikiliza Mkuu wa Polisi Wilaya pamoja na Wanafunzi.
 
Aidha kufuatia kauli hiyo ambayo ilizua hofu kubwa na kusababisha baadhi ya Wanafunzi kuanza kulia kwa uchungu na wengine wakihoji hatma yao ni ipi kutokana na Ada walizopoteza pamoja na Muda waliokaa Chuoni hapo ambapo walisema Wengine wameomba ruhusu makazini mwao na wengine wamesafiri kutoka mbali huku wengine wakilalamikia hali za uchumi wa familia zao ambazo zimelazimika kuuza mifugo na mazaoili watoto wao wasome.
 
Hata hivyo katika Hali isiyokuwa ya kawaida Meneja wa Chuo hicho Jackson  Kamugisha alifika Chuoni hapo na kuwakuta wanafunzi wakiwa wamekusanyika wakizungumza na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbeya ( Jina limehifadhiwa kutokana na kutokuwa msemaji wa Jeshi la Polisi) hakutaka kuwasilikiza badala yake alishuka katika gari yake ndogo na kuingia Ofisini kisha kuzunguka katika eneo la Chuo kwa takribani kwa dakika 20 na hatimaye kutokomea kwa Gari lingine mbele ya Askari waliokuwa hawajui cha kufanya.
 
Kutokana na kukosekana kwa majibu ya kuridhisha kwa wanafunzi hao waliamua kutoingia madarasani hadi hapo Chuo hicho kitakapotatua Matatizo yao bila kujali ushauri wa Mkuu wa Polisi ambaye pamoja na kukiri udhaifu wa Chuo hicho  pia aliahidi kupewa muda wa wiki moja ili atoe taarifa kwa viongozi wake wa juu kuhusu hatua zitakazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kumjulisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ili aweze kufika na kulitatua suala lawanafunzi hao.
 
Hata hivyo ushauri ulionekana kupuuziwa na Wanafunzi hao ambao waliamua kuandamana baada ya Siku mbili na kuelekea katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo walipokelewa na Katibu Tawala Msaidizi wa Wilaya ya Mbeya Geophrey Anania ambaye aliwasihi wanafunzi hao kurudi Chuoni nay eye kukutana na Wawakilishi wa Wanachuo.
 
Akizungumzia Suala hilo Katibu Tawala huyo alisema Ishu za Vyuo za Uuguzi ni ngumu kutokana na Mfumo ambao unatumika kusajili Vyuo hivyo kutoka Moja kwa moja Wizarani ambapo Mkoa na Wilaya unakuwa hauna nguvu ya kutoa maamuzi hata kama kuna matatizo yanayoonekana.
 
Aliongeza kuwa kutokana na madai ya wanafunzi wa Chuo cha Aggrey amejaribu kuwasiliana na Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkoa ambao  walijibu kutolijua kabisa suala hilo hali inayosababisha kuleta ugumu katika kulitafutia ufumbuzi ingawa alikiri madhaifu ya Wizara ambayo ni pamoja na kutokuwa na vitengo vya Ukaguzi katika ngazi ya Wilaya na Mkoa.
 
Alivitaja baadhi ya Vyuo ambavyo vimewahi kuleta ugumu wa kutatua matatizo kama hayo licha ya Serikali kufanikiwa kuvifunga kabisa kuwa ni kilichokuwa Chuo cha Uuguzi Inyara, Ilemi na Chuo cha Uuguzi Chimala ambacho kilifungwa baada ya Hatua kuchelewa na kusababisha wanafunzi kufanya vurugu.
 
Katika kuonesha Uongozi wa Chuo hicho haujali kabisa matatizo ya wanafunzi pamoja na michango ya Wazazi umekuwa ukitumia baadhi yaVyombo vya habari (siyo gazeti hili) kwa gharama kubwa ili kuuraghai umma kwa kukanusha kutokuwepo kwa matatizo yoyoteChuoni na kwamba wanafunzi hawana madai yoyote.
 
Baadhi ya Vichwa vya habari kutoka katika Vyombo hivyo vinavyotumika kuupotosha ukweli na kusababisha wanafunzi kuendelea kuishi chuoni hapo bila kujua hatma yao ili hali Viongozi wakifarijiwa na Vyombo ambavyo havifuati weledi na taaluma za habari kwa kuandika habari zenye pande moja tena kwa kusafisha na kupotosha ukweli na hali halisi inayoonekana hata kwa wapiti njia.
 
Vichwa vya habari vya vyombo hivyo ambavyo vilitoka katika nyakati tofauti viliandikwa hivi“ Uhaba wa wauguzi Tanzania kumalizwa na Chuo cha Uuguzi St. Aggrey na katika Toleo lingine liliandikwa St. Aggrey kupunguza adha ya wataalam wa afya nchini” Jambo linaloniumizi na kujiuliza  kichwani ni kwamba Uhaba na adha ya wauguzi itamalizwa kwa wanafunzi wepi ambapo wanaosoma katika Chuo hicho hawana uhakika wa ajira kutokana na kutokuwa na Sifa za kufanya mitihani.
 
Kutokana na kuandikwa kwa Stori zenye lengo na nia ya kuficha ukweli ni kwamba tunatengeneza madaktari na wauguzi wasiokuwa na sifa hali ambayo itasababisha wagonjwa kutibiwa katika hali isiyokuwa na uhakika endapo wanachuo hao wataruhusiwa kuingia mitaani na kufanya kazi kama wauguzi wa afya.
 
Hata hivyo kutokana na vyombo hivyo kuripoti habari hizo wanachuo hao wamejenga fitina na wanahabari ambapo wamekuwa wakiwazomea pindi wanapowaona Waandishi wanapofuatilia mgogoro wa Chuo hicho kwa kile wanachodai kuwa habari zinazoandikwa hazina ukweli kabisa na zinaripoti tofauti kabisa na hali  ilivyo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kupokea malalamiko ya Wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi St. Aggrey na kukiri kuwa kuna udhaifu na dharau kutoka katika Uongozi wa Chuo hicho kwa kushindwa kutoa ushirikiano mara baada ya Jeshi hilo kufika Chuoni hapo na kusuluhisha migogoro inayotokea.
 
Ameongeza kuwa dharau nyingine wanayoonesha viongozi hao ni kushindwa kupokea Simu zao za Viganjani wanapopigiwa na Maofisa wa Jeshi la Polisi kwa nia ya Kupata maelezo juu ya mustakabali wa Wanafunzi zaidi ya 120 wa Mwaka wa Pili wa Chuo hicho.
 
Aidha Kamanda Diwani amewahakikishia wanachuo hao kulitafutia ufumbuzi haraka sana suala lao ikiwa ni pamoja na Wanafunzi haokutakiwa kufungua kesi ili Jeshi hilo lipate malalamiko yao ya  kimaandishi ili hatua za kiuchunguzi zianze kufanyika mapema iwezekanavyo.
 
Hata hivyo juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya ziligonga ukuta baada ya Simu ya Mezani ya Mkurugenzi huyo kupokelewa na Sekretari ambaye aligoma kutoa namba ya Simu ya kiganjani na kuongeza kuwa Dr. Mwamasage yuko safarini Dodoma hivyo angetafutwa Msemaji wa Wizara ambaye hata hivyo ilishindikana kupatikana.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger