Serikali Mkoani Mbeya imetajwa
kuwa nyuma katika kuhamasisha wananchi kupenda zaidi kuutangaza na kuuweka Mkoa
huo kuwa ni Mkoa wa Kiutalii licha ya kuwa na vivutio vingi vya utalii huku
ukiabinishwa kujikita zaidi katika biashara.
Hayo yamebainishwa katika
kikao cha Kamati ya Utalii Mkoa wa Mbeya kilichoketi katika ukumbi wa
hospitali ya Mkoa wa Mbeya, ambapo mbali na hilo kamati hiyo imejiwekea
mikakati ya kuhakikisha inawashawishi wakazi wa Mkoa huu kuwavutia ili kuupenda
na kuutangaza utalii wa ndani.
Wakichangia hoja mbalimbali
wajumbe wa kamati hiyo ya utalii, walisema kuwa Mkoa wa Mbeya licha ya kuwa na
vivutio vingi vya kiutalii ambavyo vikiboreshwa na kupendwa na wakazi wa Mkoa
huo wanaweza kupata fedha nyingi kutoka kwa watalii, lakini wakazi wa Mbeya
pamoja Serikali yake imejikita zaidi katika masuala ya Kibiashara.
Mjumbe wa kamati hiyo
ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Rosemary Senyamle, alisema kuwa
Mkoa wa Mbeya unakosa fursa ya kujitangaza kupitia utalii uliopo kutokana
na wakazi wengi kuelekeza zaidi mawazo yao katika biashara huku akibainisha
kwamba Mkoa umejitangaza na umefanikiwa kuwa ni moja ya mikoa ya kibiashara.
“Mbeya imejiweka zaidi kibiashara
kuliko utalii na hili nadhani linachangiwa na Serikali ya Mkoa kutoweka
kipaumbele zaidi kuutangaza Mkoa katika sekta ya utalii licha ya kuwa na
utajiri mwingi wa vivutio vya kiutalii ambavyo tukiungana kwa pamoja
tunaweza kusonga mbele zaidi ya hapa tulipo kwa kuwa na wageni wengi wanaokuja
kwa kibiashara na kiutalii pia,” alisema Mjumbe huyo.
Aidha, wajumbe hao walisema
pamoja na kuwa Mkoa wa Mbeya kuwa na sura ya kibiashara kwa kipindi
kirefu, wakazi wa Mbeya na Viongozi wao wanawajibu wa kuubadili na kuwa sura ya
Kiutalii zaidi ili kuendelea kuwavutia wageni wengi kuja ndani ya Mkoa wa
Mbeya.
Hata hivyo, kamati hiyo
inakusudia kukuza utalii wa ndani kwa kuwapa watu wa Mbeya habari
sahihi kwa vipeperushi na matangazo yatakayohusiana na
utalii ili waelewe na kuanza kufanya shughuli za kiutalii sehemu
mbalimbali zenye vivutio.
|
0 comments:
Post a Comment