Pages


Home » » Imebainika kuwa Wanawake wengi kushindwa kusimama na kutetea haki zao kumetokana na kutojua Sheria za ndoa,

Imebainika kuwa Wanawake wengi kushindwa kusimama na kutetea haki zao kumetokana na kutojua Sheria za ndoa,

Kamanga na Matukio | 02:57 | 0 comments
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Imebainika kuwa Wanawake wengi kushindwa kusimama na kutetea haki zao kumetokana na kutojua Sheria za ndoa, Mirathi na uandikaji wa Wosia baada ya kufiwa na Waume zao.
Hayo yalibainishwa jana na Mratibu wa Kitengo cha  Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (MBEPAU) Jane Lawa wakati wa Semina iliyotolewa na Shirika hilo kwa Vijana, Wajane, Wagane, Viongozi wa Kimila na Dini iliyofanyika katika ukumbi wa Coffee Garden Mkoani hapa kwa ufadhili wa Asasi ya The Faundation for Civil Society.
Lawa alisema lengo la Semina hiyo ni kuiwezesha jamii kujua sheria ya ndoa, mirathi na uandikaji wa wosia baada ya kugundulika kuwa watu wengi wanashindwa kusimama mahakamani na kutetea haki zao kama talaka na mirathi  hususani wanawake.
 
Aidha alisema Semina hiyo ni ya mwisho kufanyika kutokana na ufadhili wa Asasi ya The Faundation baada ya kufanya kwa awamu nne kwa kata zote za Jiji la Mbeya ambapo alizitaja kata zilizomalizia kuwa ni pamoja na Ilemi, Iyela, Nonde, Tembela na Mwasanga.
 
Alisema MBEPAU walianza kutoa elimu katika jamii kwa lengo la kuijengea uwezo wa kutambua haki zao baada ya kuona jamii ina uelewa mdogo wa kisheria na haki zao.
 
Hatua hiyo inakuja baada ya wanawake wengi na watoto maeneo ya vijijini kudhurumiwa haki zao kutokana na kuto tambua haki zao za msingi zikiwemo haki ya kumiliki Ardhi na mali,haki za watoto na elimu ya ndoa.
 
Lawa alisema kutokana na kutambua uwepo wa tatizo hilo, wameshatoa mafunzo hayo kwa washiriki  ambao kati yao ni Maafisa watendaji wa kata,wenyeviti na Makatibu wa mabaraza ya usuruhishi kwa wilaya ya Mbeya mjini.
 
Alisema tangu kuanza kwa mpango huo unaofadhiliwa na Tasisi ya The foundation for civil Society(FCS) umeweza kutoa elimu kwa washiriki hao kutoka kata zote za Jiji la Mbeya wakiwemo  wajane,Walemavu, Wazee wa Mila na vijana.
 
Lawa alisema wanawake wengi wamekuwa wakipata manyanyaso mengi baada ya kufiwa na waume zao kutokana na kutojua haki zao kutokana na kukandamizwa na sheria za kimila za makabila yao.
Kwa upande wake baadhi ya Washiriki wa semina hiyo walisema Serikali inatakiwa kuunga mkono juhudi za asasi binafsi zinazotoa mafunzo na elimu kwa jamii zilizosahaulika kama walemavu.
“ Mara nyingi walemavu husaulika katika mafunzo kama haya lakini Serikali inatakiwa iwe inatoa elimu kama hizi vijijini pia nawasihi walemavu wenzangu kutojificha majumbani kwa sababu wanakosa mambo mengi” alisema Elizabeth Mwanjala makazi wa kata ya Ilemi mshiriki wa semina ambaye pia ni mlemavu.
 
Kiongozi wa Mila Nicholaus Sinjinga(85) aliyehudhuria  mafunzo hayo alisema mafunzo kama hayo yawe yanatolewa mara kwa mara ili jamii iachane na mila zilizopitwa na wakati badala yake wafuate sheria zinavyotaka.
Naye Imelda Mbwilo(25) mkazi wa Tembela aliyewakilisha kundi la vijana alisema watu muhimu wa kupewa mafunzo kama hayo ni vijana ambao wanatakiwa baada ya kupewa elimu kwenda kutoa kwa wengine ili kujenga kizazi kitakachokuwa kinajua umuhimu wa sheria hiyo.
 
Aliitaja Sheria ya Mwaka 1971 kifungu cha 39 kinachosema ndoa ni maamuzi ya hiari kati ya mume na mke kukubaliana kuishi pamoja hivyo suala la ndugu kuingilia masuala ya mirathi hususani kwa wanawake wanaofiwa na waume zao kuwa yanapingana na sheria hiyo.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger