Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mh, Philipo Mulugo.
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Wamiliki wa Shule na Vyuo
visivyokuwa vya Serikali nchini wametakiwa kujikita na kuanzisha Shule na
Vyuo vya Ufundi Stadi ili kukidhi haja ya ongezeko la wanafunzi wanaomaliza
Kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano.
Aidha wametakiwa kuendana na mipango ya baadaye ambapo Shule na Vyuo vingi vimejikita katika Michepua ya
Sanaa na kusahau Michepuo ya Sayansi kutokana na Nchi kuwa na uhitaji wa Walimu
na wataalamu wa Sayansi ambapo pia ameongeza kuwa Serikali itawakopesha
Wanafunzi watakaosoma Sayansi.
Mwito huo ulitolewa jana na
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo alipokuwa akifunga Mkutano wa Mwaka wa Wamiliki,
Mameneja na Wakuu wa Shule na Vyuo visivyokuwa vya Kiserikali (TAMONGSCO)
uliofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkapa uliopo Sokomatola Jijini
Mbeya.
Alisema Wamiliki wa Vyuo
wanaouwezo wa kujenga Shule na Vyuo vingine hivyo wajikite katika Michepuo ya
Sayansi ili kuisaidia Serikali katika Kuziba pengo la upungufu wa Wataalamu wa
Sayansi ambapo pia aliongeza kuwa Serikali imewapa kipaumbele cha Mikopo
wanaochukua michepuo hiyo.
Naibu Waziri aliongeza kuwa ili
kuondoa migogoro baina ya Serikali na Shule binafsi ni vema kila anayetaka
kuanzisha Shule au Chuo pamoja na Vyuo
vilivyopo ambavyo havijajiunga na Umoja wao kufanya hivyo mara moja, lakini
ambaye hatajiunga na umoja huo hataweza kupata ufafanuzi wa maswala yoyote
anayoyahitaji kutoka Serikalini.
Mulugo alisema Wenye mashule na
vyuo binafsi wengi hawana uelewa juu ya Wizara ya Elimu, Tamisemi na ngazi zinazohusika na Elimu hivyo njia
rahisi ya kuwaelimisha ni kupitia umoja wao ambapo aliongeza kuwa katika
kulisisitiza Hilo atahakikisha anamwagiza Kamishna wa Elimu na Nekta
kuwasisitiza umuhimu wa kujiunga na umoja.
Awali akimkaribisha Naibu
Waziri kufunga Mkutano huo Mwenyekiti wa TAMONGSCO Taifa Mahamoud Mlingo
alisema umoja wao unakabiliwa na
Changamoto nyingi kutoka Serikalini ambazo zinatishia baadhi ya Shule binafsi
kuendelea kujiendesha.
Alizitaja baadhi ya Changamoto
hizo kuwa ni kutolewa kwa Nyaraka nyingi zinazofikia 20 ambazo zinaeleza namna
ya kuongoza Elimu hususani Shule za Taasisi Binafsi ambapo baadhi ya Vipengele
ndani ya Nyaraka hizo zinapingana na Haki ya Mtanzania ya kupata Elimu Bora kwa
njia ya Mchujo.
Aliongeza kuwa Mfumo mzima wa
kuangalia Viwango vya Ufaulu tangu Mwanzo bila kuwashirikisha Wakuu wa Vyuo na
Shule binafsi ndiyo unaochangia Elimu kuendelea kudorora kutokana na Serikali
kutothamini mchango unaotolewa na Sekta Binafsi hususani kwenye Elimu ili hali
Sekta zingine binafsi zinashirikishwa kutokana na Sera ya PPP.
Pia aliongeza kuwa Kushirikiana
na Serikali namna ya ya kushirikiana katika Matumizi ya Vyumba vya
Madarasa 500 ambavyo viko tupu nchi
nzima kutokana na upungufu wa Wanafunzi katika Shule binafsi.
Mwenyekiti huyo alisema
Changamoto nyingine inayoikabili Sekta binafsi katika Suala la Elimu ni gharama
kubwa za uendeshaji kutokana na kuchangia michango mingi Serikalini kama
Zimamoto na Osha pamoja na Kodi za kawaida ili hali huduma ya Elimu ni huduma
ya Jamii ambayo haipaswi kuwa na michango mingi.
Aliitaja Changamoto nyingine
kuwa ni Serikali kupokonya Wanafunzi wote kutokana na ujenzi wa Shule za Kata
ambapo Shule binafsi hukosa wanafunzi hivyo kupelekea Shule hizo kushindwa
kujiendesha kutokana na kuwa na wanafunzi wachache.
Akijibu baadhi ya Changamoto
hizo Naibu Waziri Mulugo alisema ni vema wakaandika madai yao yote ili yakaye
kwenye maandishi ili Serikali ianze kuyafanyia kazi moja baada ya jingine ambapo alisema pia kuna kamati maalumu
imeundwa ili kuyafanyia kazi madai ya baadhi ya Vyuo n Shule binafsi kutoza ada
kubwa inayowaumiza wazazi.
Pia aliongeza kuwa Serikali
imeanza kuyafanyia kazi baadhi ya mambo ikiwemo Maswala ya Sheria ambazo
zilitungwa muda mrefu na haziendani na mfumo wa sasa wa uendeshaji wa Elimu.
0 comments:
Post a Comment