ofisa wa
Upelelezi Mbozi akionyesha sehemu ya Mbolea mbovu ambayo imefumbiwa macho na
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania na kuitakatisha kama haina matatizo wala
madhara kwa wakulima
Katika hali inayoonyesha kuna mchezo mchafu wa kuendelea
kuwamaliza wakulima wilayani Mbozi, shehena ya Mbolea mbovu iliyozuiwa
kuuzwa mwaka jana hatimaye “upepo umepita” na kuruhusu iendelee kuuzwa kwamba
ipo juu kiviwango!
Katika hali hiyo wakulima wamekuja juu jana wakati wakishuhudia
ufunguzi wa duka la STACCO ambalo miezi kadhaa lilishuhudiwa likiwa limepigwa
makufuli na kwa mbwembwe nyingi ikiwemo msururu wa vyombo vya habari, lakini
kwa jana ilikuwa kimya kimya kufuli la kwanza likafunguliwa, likafuata la pili
na hatimaye la tatu!
Wakati wananchi kwa macho yao meupe wakishuhudia mifuko
iliyoganda ya Mbolea za UREA, DAP, CAN na SA taarifa iliyotolewa kuruhusu
kufunguliwa kwa duka hilo inatoa maelezo kuwa ni Mbolea ya SA peke yake
ndiyo iliyobainika kuwa na ubora hafifu! ambayo ni mifuko 11 tu.
Hata hivyo afisa anayesimamia ubora wa Mbolea katika halmashauri
ya wilaya ya Mbozi Bi Shonyela amesema licha ya maelekezo kutoka juu mengine
hayatatekelezeka kwani kufanya hivyo itakuwa ni kuwamaliza wakuliwa wa wilaya
yake kwakuzingatia kuwa Mbolea iliyoganda kuto kufaa tena mashambani.
“nimeandikiwa Mbolea aina ya SA pekee ndiyo isafirishwe chini ya
usimamizi wa polisi kwenda Dar es Salaam lakini ni mifuko 11tu! Wakati kuna
mbolea aina nyingine ambazo ni zaidi ya mifuko 50 hazina viwango vya ubora na
taarifa imekuwa kimya” alifafanua
Uchunguzi wa haraka kwenye duka hilo unaonyesha kuwa mifuko16 ya
DAP ilikuwa imeganda wakati wa kufunga duka hilo mwezi September mwaka jana,
UREA mifuko 16, CAN 11 na SA 11.
Ingawa katika maelezo ya mkurugenzi wa Mamlaka ya udhibiti wa
Mbolea Tanzania TFRA ilionyesha kuwa wangeshirikiana bega kwa bega na TBS
katika kuhakikisha viwango vya bidhaa hiyo vinasimamiwa, maamuzi ya kuruhusu
uuzwaji wa mbolea aina ya DAP, CAN na UREA iliyoharibika kwenye ghala la STACO
wilayani Mbozi yanajenga mawimbi na mashaka kwa wananchi kuwa mamlaka
imelainishwa na ama wamefumbishwa macho!
Tanzania hutegemea maabara yake ya Mbolea iliyopo Mlingano
mkoani Tanga kuthibitisha ubora wa bidhaa hizo hata hivyo kumekuwepo
udanganyifu unaofanywa na baadhi ya maofisa wa serikali na kuwasaliti wakulima
kutokana na makampuni yanayofanya shughuli za usambazaji wa pembejeo na hasa
Mbolea kushika keki kubwa katika mzunguko wa fedha nchini
Wakati pia chuo cha kilimo SUA kimekuwa kikitumika katika tafiti
na uchunguzi wa Mbolea, mwaka jana Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika Dr Adam
Malima alikataa matokeo ya uchunguzi wa mbolea yaliyotolewa na SUA na kuahidi
sampuli za Mbolea iliyokamatwa RUVUMA kupelekwa nchini Afrika kusini
kujiridhisha na uchuguzi wa maabara za huko baada ya kulalamikiwa na wakulima
Aidha naibu waziri alisitisha leseni za makampuni ya STACO na
Mohamed Enterpries mnamo August 07 mwaka jana, ambapo baada ya siku kadhaa
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania Suzana Ikelya alitua Mbozi na
kukamata Mbolea kwenye duka la STACO
“Maamuzi ya mamlaka ya ukaguzi wa ubora wa Mbolea yanawaacha
wananchi wilayani Mbozi wakikosa imani kutokana na namna maamuzi yanavyofikiwa
hata katika mambo ambayo hayahitaji utaalamu kuthibitisha ubora kama suala la
Mbolea iliyoganda” anaeleza bwana Keneth Mwazembe mmoja wa wakulima wakubwa
wilayani Mbozi.
Msimamizi wa duka la STACO bwana Julius Masai licha ya kufurahia
kufunguliwa kwa ofisi yake ya chakula, amesema ni kweli kwamba kuna mbolea
ambayo haimo kwenye barua ya kuruhusu uuzwaji ambayo haifai kwa matumizi lakini
wanatumia busara kuitenga licha ya kutoelezwa kwenye barua hiyo
Ni kweli kuna mifuko kama 37 hivi ya mbolea mchanganyiko ambayo
ni mbovu na tumeitenga pembeni na hatutaiuza” alisema meneja huyo bwana Julius
Masai
Duka hilo limefunguliwa jana chini ya usimamizi wa maofisa
wawili wa idara ya upelelezi ya jeshi la polisi na ofisa anayesimamia ubora wa
MBOLEA wilaya ya Mbozi, na shughuli hiyo imefanyika kimya kimya tofauti na
mbwembwe zilizofanyika wakati wa kufunga duka hilo ambapo wananchi waliokuwa
wakipita barabarani waliitwa kushuhudia namna wanavyotendwa!
Kwahisani ya Indaba Africa
|
0 comments:
Post a Comment