Pages


Home » » Wananchi Mkoani Mbeya wameaswa kuacha na shughuli za kiuhalifu...

Wananchi Mkoani Mbeya wameaswa kuacha na shughuli za kiuhalifu...

Kamanga na Matukio | 02:34 | 0 comments
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani akiongea na waandishi wa habari
Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Wananchi Mkoani Mbeya wameaswa kuacha na shughuli za kiuhalifu badala yake wafanye shughuli halali ili kupata maendeleo kutokana na fursa  zinazowazunguka.
 
Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa kuhakikisha mtandao wa ujambazi unasambaratishwa na kukamatwa wahusika.
 
Diwani alisema ni vema wakazi wa Mkoa wa Mbeya wakatafuta kazi ambazo ni halali na siyo kujiingiza katika ujambazi kwa lengo la kujipatia mali kwa njia zisizofaa ambazo husababisha ukosefu wa amani katika jamii.
 
Aidha Kamanda Diwani  amewatahadharisha watu wote wanaojihusisha na ujambazi kujisalimisha wenyewe katika Jeshi la Polisi au kuacha kabisa ikiwa ni pamoja na kuondoka katika Mkoa wa Mbeya kwa kile alichodai kuwa Jeshi lake limejipanga kuhakikisha uhalifu unaisha.
 
Amewata wananchi wenye taarifa zinazohusu mtandao wa ujambazi kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na siyo kuwakumbatia mitaani na wengine kushirikiana nao.
 
Alisema Jeshi lake limejipanga kikamilifu kuhakikisha ana usambaratisha mtandao wa Ujambazi na uhalifu uliokuwa umekithiri Mkoani Mbeya hali iliyosababisha wageni kuogopa kuja kuwekeza katika mkoa humo wenye fursa za kutosha.
 
“ Nitahakikisha majambazi wote wanakamatwa la sivyo watafute shughuli zingine za kufanya, naogopa siku nikifa nitajibu nini kwa Mwenyezi Mungu atakapo niuliza nilipokuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ulifanya nini?” alisema Kamanda Diwani.
 
Hata hivyo aliwasihi Wananchi kuacha tabia ya kuchukua sheria mkononi katika matatizo yanayowakabili  badala yake watafute ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na utaratibu unaokubalika kisheria kupitia mamlaka husika yakiwemo matatizo ya kijamii.
 
Wakati huo huo Wadau wa Amani Mkoani Mbeya wamelipongeza Jeshi la Polisi mkoani hapa kutokana na juhudi za kupambana na uhalifu hususani kudhibiti mtandao wa majambazi sugu.
 
Wadau hao walisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani ndiye anayepaswa kupongezwa kutokana na juhudi alizozionesha za kufichua mtandao wa majambazi ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwauwa wengine.
 
Akizungumza kwa niaba ya wadau hao Nwaka Mwakisu ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia Umoja wa Vijana Mkoa wa Mbeya katika mkutano wa waandishi wa Habari uliofanyika katika ofisi za Umoja wa Vijana CCM Mkoa wa Mbeya.
 
Mwakisu alisema historia ya Mkoa wa Mbeya ilikuwa mbaya ambapo ilikuwa ikisifika kwa matukio mabaya kama ya upigaji nondo, ubakaji, ushirikina na ujambazi ambavyo vimeanza kutoweka kutokana na juhudi zilizooneshwa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi.
 
" Kutokana na hali ilivyo sioni sababu ya kutompongeza RPC Diwani kutokana na kupambana na uhalifu Mkoani Mbeya " alisema Mwakisu.
 
Alisema kutokana na hali halisi ya amani ya Mkoa wa Mbeya wawekezaji watajitokeza kwa wingi kufanya uwekezaji tofauti na ilivyokuwa ambapo wawekezaji walikuwa wakikimbia Mkoa wa Mbeya kutokana na vurugu zilizokuwepo.
 
Aliongoza kuwa kutokana na juhudi za Jeshi la Polisi za kupambana na uhalifu alisema ni vema kila mwananchi akatambua mchango huo na kusaidia katika kuhakikisha kuwa amani inaongezeka Mkoani Mbeya.
 
Mwakisu alisema pamoja na kutokomeza uhalifu mkoani hapa pia suala la kuwatumikisha vijana katika mambo yasiyokuwa na msingi wowote hususani kwenye vurugu ndiyo sababu ya kuongezeka kwa uhalifu.
 
Alisema taifa lolote duniani linalindwa na kuendelezwa na vijana hivyo alitoa wito kwa wanasiasa kuacha kuwatumia vijana vibaya ambapo aliongeza kuwa vijana wenyewe wanatakiwa kujitambua na kujiunga kwenye vikundi mbali mbali ilikuepuka kutumika kwa maslahi ya watu wengine.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger