Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Viongozi
wa Chama cha Waendesha Pikipiki (BODABODA) Jiji la Mbeya wamelazimika kuachia
ngazi baada ya kutuhumiwa kufuja fedha za Chama hicho Shilingi Milioni
15(15,000,000/=) zilizokuwa zikikusanywa na viongozi hao kwa kipindi cha miaka
minne.
Hayo yalibainishwa juzi katika Mkutano
uliofanyika kwenye ukumbi wa Tumaini ulioko Ilomba Jijini Mbeya ambao
uliwakutanisha Viongozi wa Vituo vya Bodaboda vya Uyole, Kabwe, Soweto,
Mafiati, Mwanjelwa, Ilomba, Sai na Stendi kuu.
Wakizungumza
katika kikao hicho viongozi wa Mpito wa Chama hicho chini ya Mwenyekiti Jackson
Nusurupia aliwaambia wajumbe wa Mkutano huo kuwa fedha zilizofujwa ni pamoja na
viingilio vya wanachama Shilingi Milion Sita, Fedha za Ushirika Shilingi
855,000/=, Vitambulisho Shilingi 545,000/=, Fedha za tozo na adhabu kwa
waendesha bodaboda wanaobeba abiria zaidi ya Mmoja(mishikaki) Shilingi Milion
7.1/= pamoja na Fedha zilizotolewa na Naibu Waziri wa Elimu Philipo Mulugo
Shilingi Laki tano na kufanya jumla ya Milion 15.
Mwenyekiti
huyo alisema kufuatia tuhuma hizo viongozi hao walijiuzulu wao wenyewe ili
kupisha uchunguzi, ambapo Uongozi wa muda ulichaguliwa ili kuendelea kuendesha
chama hicho hadi Mei 20, Mwaka huu uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Alisema
baada ya kujiuzulu kwa uongozi huo Wanachama waliwachagua viongozi wa Muda
ambao ni Jackson Nusurupia (Mwenyekiti), Eliudi Clemens (Makamu Mwenyekiti),
Msumba Mdesa( katibu) pamoja na wajumbe watano ambao ni Mishael Mwashilindi,
Elly Bariki, Wilson Bukuku, Noah John na Ayubu Mwaisakila.
Aliwataja
watuhumiwa wa kesi hiyo kuwa ni Vicent
Mwashoma aliyekuwa Mwenyekiti, Fred Mwambene (makamu Mwenyekiti), Yonah
Mwaipungu(katibu) na John Bosco aliyekuwa Mtunza hazina wa Chama hicho.
Nusurupia
alisema Viongozi hao hawakuwahi kutoa taarifa ya mapato na matumizi tangu
kuanzishwa kwa Chama chao Mwaka 2009 na kuongeza kuwa baada ya kutuhumiwa
walitakiwa kukabidhi nyaraka zote za Chama pamoja na kuhudhuria Mkutano lakini
hawajafanya hivyo jambo linaloashiria kuhusika na Ubadhilifu huo.
Kwa
upande wake Viongozi wanaotuhumiwa walijitetea kuwa habari za kuliwa Fedha si
za kweli kwa sababu Chama kina Jumla ya Shilingi 589,000/= na kwamba fedha
zilizotolewa na Naibu Waziri zimetumika na kubakia Shilingi 185,000/=na
kusisitiza kuwa taarifa zote zipo na zitatolewa kwenye mkutano mkuu.
Mwenyekiti
aliyejiuzulu wadhifa wake huo alisema Fedha za viingilio za wanachama
hazijawahi kukusanywa kwa kile alichodai kuwa Wanachama walikuwa wabishi wa
kuchangia, na kuongeza kuwa fedha za adhabu zilirudishwa kwenye vituo vya Bodaboda
kwa Wenyeviti huku zingine zikiwa zimelipiwa faini Polisi kwa wenye makosa.
Mkutano
huo uliosimamiwa na Walezi wa Chama hicho ambao ni Jeremia Magacha na Isack
Jackson Lema ambao ni Maofisa wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, walisema
hawapingani na maamuzi ya viongozi ambapo waliwasihi wanachama kuwa watulivu
katika kipindi cha mpito wakati wakisubiri taarifa za uchunguzi na kuongeza
kuwa baada ya kubainika Sheria itachukua mkondo wake ambapo Mkutano
uliahirishwa hadi Mei 20, Mwaka huu utakapofanyika Mkutano mkuu.
0 comments:
Post a Comment