Mkuu wa wilaya ya Kyela Bi.Margretha Malenga akila kiapo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro.(Picha kutoka Maktaba)
Na Solomoni Mwansele.
MKUU wa wilaya ya Kyela, Magreth Malenga, amesema kazi
waliyopewa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya uongozi wa Rais
Jakaya Kikwete, ya kuwaletea maendeleo wananchi inafanyika kwa kasi.
Imeelezwa barabara nyingi, zikiwemo zile za kiwango cha lami
na ujenzi wa madaraja likiwemo la Lusungo, zinaendelea vizuri.
Magreth aliyasema hayo jana wakati akielezea utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa wananchi waliohudhuria maadhimisho ya miaka 36 ya
CCM, zilizofanyika kiwilaya katika
viwanja vya siasa, Kyela mjini.
“Ahadi ya Rais Kikwete ya ujenzi wa barabara ya Kikusya
kwenda Matema, kwa kiwango cha lami, imeanza kutekelezwa.Vile vile upembuzi
yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Lusungo tayari umekamilika na mara
baada ya msimu huu wa mvua kumalizika litaanza kujengwa” alisema na
kushangiliwa.
Mkuu wa wilaya aliongeza wakulima wilayani humo, hivi sasa
wanaendesha kilimo chenye tija ambacho ndiyo mkombozi wa mkulima, huku ujenzi
wa shule za sekondari sambamba na mabweni umekuwa ukiendelea vizuri.
Magreth alisema hivyo ni jukumu la wananchi kumalizia ujenzi
wa sekondari hizo pamoja na mabweni, ili serikali nayo iweze kutimiza jukumu
lake la kumalizia ujenzi huo na hivyo kuziwezesha kuchukua wanafunzi.
Kwa upande wa sekta ya afya, alisema serikali imekuwa
ikifanya kila jitihada kuhakikisha sekta hiyo inaimarishwa na kuboreshwa zaidi
ili wananchi waweze kupata tiba stahili na kwa wakati.
Magreth alisema:”Lakini moja ya changamoto iliyopo ni uzembe
unaofanywa na baadhi ya watendaji katika hospitali yetu ya wilaya…hili
tunaendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha tunaipatia ufumbuzi kero hii ili
hospitali hii iwe kimbilio la wananchi wengi”.
0 comments:
Post a Comment