Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mtikisiko mkubwa umeukumba Mkoa wa Mbeya kutokana na vitendo vya ujambazi vilivyotokea hivi karibuni, likiwemo la Askari wa Jeshi la Polisi kuawa katika Wilaya ya Chunya mkoani humo.
Mbali na askari polisi kuuawa pia majambazi walimuua kwa kumpiga risasi Mzee Cosmas Kunzugala mkazi wa Airpot, Jijini Mbeya, akiwa nyumbani kwake baada ya kugongewa mlango na watu wasiofahamika.
Tukio jingine limetokea Mafinga ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Festo Kyando(47), akiwa na msaidizi wake katika gari waliuawa kisha kuzikwa katika msitu wa Mafinga, kabla ya Jeshi la polisi mikoa ya Iringa na Mbeya kugundua na kuifukua Februari 18 na kuisafirisha hadi Mbeya Februari 19 mwaka huu na miili hiyo kuzikwa upya.
Akiongea na mtandao huu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Diwani Athuman amesikitishwa na vitendo hivyo na kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivyo vinavyofanya wananchi kuishi kwa hofu pia kuwafanya watu wanaotaka kuwekeza mkoani hapa kuogopa na kuufanya mkoa kudumaa kiuchumi.
aidha Kamanda huyo wa polisi amesema Jeshi lake linafanya kila jitihada ili kubaini wale wote waliohusika na vitendo hivyo ambavyo vinatia doa Mkoa wa Mbeya.
Katika tukio la dereva na tingo wake kuuawa mali ya zaidi ya shilingi milioni 800 iliporwa na majambazi hayo kisha gari kutelekezwa Makambako.
0 comments:
Post a Comment