NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Kyela kimesema viongozi
wa CHADEMA wanataka kutumia fursa ya uwepo wa mafuta katika tarafa ya Ntebela, kuwachochea
wananchi kufanya fujo.
Kufuatia hilo,kiimewatoa
hofu wananchi kipo makini, na kitahakikisha kinatoa elimu sahihi kwa wananchi
juu ya utafiti wa mafuta uliofanyika hivi karibuni, na kubaini uwepo wa mafuta
katika baadhi ya kata za tarafa hiyo.
Kaimu Katibu wa CCM wilayani humo, Richard Kilumbo,
aliyasema hayo mbele ya Mjumbe wa halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM,
Sambwee Shitambala, kwenye maadhimisho ya miaka 36 ya CCM.
Kilumbo alisema:”Juzi na jana wenzetu wa CHADEMA wamekuwa
wakiwashawishi wananchi ili tuingie kwenye vurugu kama
ilivyotokea hivi karibuni mkoani Mtwara, baada ya kuonekana wilaya yetu inayo
mafuta na utafiti umefanyika bado taarifa rasmi kutolewa”.
Aliongeza hivyo CHADEMA wanataka kutumia fursa hiyo ya
kuwepo mafuta wilayani Kyela, kuwahamasisha wananchi kufanya vurugu ili
machafuko yatokee wilayani humo kitendo ambacho Chama hakiwezi kukubali.
Kaimu Katibu wa CCM wilaya, aliwataka wananchi kuondoa hofu
juu ya hilo, kwani mwananchi yeyote ambaye eneo lake analolimiliki
likionekana kuwa mkondo huo wa mafuta atalipwa fidia stahili.
Kilumbo alisema wananchi waondoe dhana potofu
inayopandikizwa na viongozi wa CHADEMA, kwani CCM itahakikisha hakuna mwananchi
anayestahili haki yake halafu akadhurumiwa.
Aliongeza Chama kipo tayari kupambana na CHADEMA na vyama
vingine vya upinzani wilayani humo, ambavyo vinajiandaa kufanya kama yale
yaliyotokea mkoani Mtwara wananchi kugomea gesi isisafrishwe kwenda Dar es Salaam.
Kilumbo alisema:”Chama kitapita kata zote ambazo mkondo huo
wa mafuta umeonekana na kutoa elimu sahihi juu ya uwepo wa mafuta wilayani
kwetu…walifanikiwa kuwachochea wananchi wa Mtwara, lakini kwa wilaya ya Kyela
wasahau kwani hilo
halitawezekana kamwe”.
0 comments:
Post a Comment