Na.Angelica Sullusi.
HALMASHAURI
ya Jiji la Mbeya imewaondoa hofu wakazi wake wanaoishi na virusi vya
Ukimwi (VVU) kuwa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi ARVs
zilizosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini hazikuingia Mkoani Mbeya.
Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, DK. SAMWEL
RAZARO ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha
Halmashauri ya Jiji la Mbeya kilichoketi hivi karibuni mjini hapa.
Razaro alikuwa akijibu swali la Diwani wa
kata ya Isyesye, SANKE SESO ambaye alitaka kujua kama kuna madhara
yaliyowapata wakazi wa Jiji la Mbeya baada ya kubainika kuwa zipo dawa
za ARVs ambazo ni bandia.
DK.RAZARO amesema kuwa
baada ya kubainika kuwa kuna dawa za bandia zimeingizwa sokoni, Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa kushirikiana na Wakala wa usambazaji dawa
nchini (MSD) walifanya ukaguzi kwa kupitia dawa zote na kugundua kuwa
dawa hizo hazikuingia katika mikoa ya Mbeya na Rukwa.
Akizungumza
na BOMBA FM baada ya kumalizika kwa kikao hicho, DK. RAZARO amesema
kuwa taarifa za kuwepo kwa dawa za bandia za kupunguza makali ya virusi
vya Ukimwi zilionyesha kuwatia hofu kidogo watumiaji ingawa hazikuathiri
mahudurio ya watumiaji kwenye vituo vya kutolea dawa hizo.
Sakata
la uwepo wa dawa za bandia sokoni tayari limeshasababisha baadhi ya
maofisa wa MSD kuwajibishwa ambapo Mkuu wa MSD na viongozi wengine
wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa suala hilo.
0 comments:
Post a Comment