Pages


Home » » MAKALA YA MBEGU FEKI

MAKALA YA MBEGU FEKI

Kamanga na Matukio | 02:32 | 0 comments
Na Esther Macha,
SERIKALI ya Tanzania ilitangaza sera ya Kilimo Kwanza kama njia maalumu ya kitaifa ya kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini na kuinua pato la wakulima Kwanza inajumuisha mikakati inayolenga katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili kilimo chetu na kutumia fursa lukuki tulizonazo kujiondolea umaskini wa kipato.

Azima ya Kilimo Kwanza ilibuniwa chini ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambalo ni mfumo wa mashauriano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenyekiti wa Baraza hilo.

Licha ya nchi yetu kuwa na hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo, ni asilimia 23 tu ndiyo inayotumika. Kuna hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na maji ya kutosha yapo lakini ni asilimia moja tu iliyo chini ya umwagiliaji.

Aidha, licha ya Tanzania kuwa na maziwa na mito yenye maji ya eneo la kilomita za mraba 62,000, ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilomita 1,424 na kilomita za mraba 223,000 za ukanda maalumu wa kiuchumi baharini (Exclusive Economic Zone), lakini maji hayo mchango wake kwa pato la taifa na la mtu mmoja mmoja bado ni hafifu .

Kilimo kinachangia asilimia 95 ya chakula kinachotumika nchini, asilimia 30 ya mauzo nje na asilimia 65 ya malighafi zinazotumika katika viwanda vyetu vya ndani.

Kujitosheleza kwa chakula ni muhimu kwa usalama na utulivu wa nchi yetu, pia itasaidia kupunguza mfumuko wa bei kwani chakula huchangia kiasi cha asilimia 55.9 katika kupima kiwango cha mfumuko wa bei.

Kilimo ni kiungo muhimu cha sekta mbalimbali katika kuchangia kutimiza malengo ya kukuza uchumi wa taifa. Ni dhahiri kwamba hatuwezi kufuta umaskini bila kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo. Kwa jumla ili Tanzania iweze kufikia malengo yake ya maendeleo sekta ya kilimo inatakiwa ikue kutoka asilimia nne hivi sasa na kufikia angalau asilimia 10.

Kwa kutambua umuhimu wa kilimo katika nchi yetu, kwa nyakati mbalimbali, zimefanyika jitihada maalumu za kuendeleza kilimo.

Mafanikio ya kilimo kwa kiasi fulani yamepatikana lakini bado hakijapata nafasi ya kumwondolea Mtanzania umaskini wa kipato, bado yuko taabani kimaisha.

Kutokana na umuhimu wa kilimo katika maendeleo yetu, ilitakiwa kipewe kipaumbele mkubwa ili kuinua maisha ya watu ambayo yanategeme kilimo cha mvua, ambayo si ya uhakika.

Hivyo, ni wajibu wa serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kuhakikisha kwamba sera ya Kilimo Kwanza inamkwamua kiuhalisia mkulima, hasa mdogo, kwa kumuwezesha kulima kisasa.

Kwa kuzingatia hilo hivi karibuni mwandishi wa makala alitembelea katika kijiji cha Ichesa Kata ya Myovisi ,Wilaya ya Mbozi Mkoani  Mbeya kufuatilia malamiko ya wakulima  kuumwa matumbo baada ya kula ugali unaodaiwa kutokana na mbegu feki ya  mahindi ya njano inayodaiwa kusambazwa na wakala mmoja kijijini hapo.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wakulima hao Bi.Joliga Ndwina anasema kutokana na adha hiyo wakulima hao wameziomba mamlaka husika na watafiti kulifuatilia kwa kina suala la ununuzi wa vocha za mbolea ya ruzuku kutoka kwa wakulima kumuuzia wakala kwa bei ya kati ya sh.2,000 hadi Sh.4,000 unaodaiwa kufanywa na wakala mmoja jina limehifadhiwa.

“Sawa tunaweza kulaumu wakala kwa haraka lakini mtu ambaye anatakiwa kulaumiwa hapa ni Kampuni ya PANNAR kwani wao ndo walimpa wakala wao kusambaza mbegu hizo,mahindi haya hayana soko kabisa pili  matumbo yanauma sana tukila ugali wake tunaomba serikali itusaidie katika hili  hali mbaya kwakweli nah ii kampuni ichungwe kuhusu mbegu hizi haiwezekani sisi tuumie wakati wengine wanapata raha”anasema mama huyo.

 “Hili suala ni la muda mrefu sana hapa kijijini lakini wataalamu mbali mbali wamekuwa wakifika lakini hatuna huyu wakala kuchukuliwa hatua zozote zaidi ya kuona tu mtaalamu huyu anakuja na Yule lakini kinachofanyika”anasema.

Wakizungumza na  gazeti hili baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ichesa (majina tunayo)walisema kuna hatari kubwa kwa mwaka huu waananchi wa Kijiji hicho kukumbwa na baa LA njaa na hali ya uchumi

kushuka kutokana na kusambaziwa mbegu inayotoa unga wa njano inayodaiwa ya kampuni ya pannar na hivyo kukosa kabisa soko.

Bw.Nasibu Mwashilindi anasema kuwa  wamejitahidi kwenda kuuza mahindi hayo kwa sh. debe sh.2,000 katika soko la mazao Mlowo licha ya bei ya mahindi kwa debe kupanda hadi kufikia sh.6,000 lakini hayanunuliwi na kurudi nayo majumbani.

"Hali ni mbaya ndugu zangu haya mahindi ni shida kwani hakuna anayenunua kutokana na ugali wake kuwa mchungu mdomoni na hata upande wa soko bado ni tatizo sana sisi wananchi wa kijiji cha Ichesa tuna
wakati mgumu sana kwani uchumu wetu wa maisha ni mgumu kufuatia hali hii kwani hatujui haya mahindi tutayapeleka wapi mpaka sasa"anasema mwananchi huyo.

Bw.Mwashilindi anasema kibaya zaidi mahindi hayo hayaliki kutokana na uchungu wa ugali wake hasa ukipoa na wengine wanalalamika watoto wao kuumwa matumbo wanapokula jambo ambalo wamehofia kuwa linaweza kuleta athari kiafya.

Hata hivyo baadhi ya wakulima hao wamesema  kuwa mbegu hizo zilizokuwa rangi ya njano wameuziwa na wakala huyo ambapo mfuko umeonesha zimetoka katika kampuni ya Pannar lakini katika jambo la kushangaza hata kibunzi ni chekundu na imefikia hatua wananyanyapaliwa katika mashine za kusaga
kama watu wenye kimela cha kutengenezea pombe.

"Tunapokwenda kusaga mashine wanatuambia tusubiri hadi wamalize kusaga wenye mahindi meupe na sisi ndiyo tunakuwa wa mwisho hata kama tumewahi,sababu ni kwamba nikitangulia mimi mwenye mahindi ya njano na wote watakaofuatia hata wakiwa na mahindi meupe yanabadilika kuwa
njano,"walisema.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ichesa,Bw.Paul Mwasenga anasema walipokea vocha za ruzuku za pembejeo 600 za mbolea aina ya Urea ya kukuzia mwezi februari,2012 na kwamba kweli vocha za mbolea ya kupandia aina ya CAN hazikufika kabisa.

Aidha Bw.Mwasenga alikanusha kusikia taarifa ya wakala kununua vocha za ruzuku kwa Sh.2,000 amekanusha vikali na kudai hizo ni njama za kuchafuana kisiasa na hakuna kitu kama hicho ingawa alifafanua.

Mtendaji huyo amekiri kupata malalamiko ya kuwepo mbegu feki ya mahindi ambayo imekuja kubainika baada ya mahindi kukomaa na kwamba wakulima walinunua mbegu hiyo katika maeneo tofauti ikiwemo kwa wakala Ntandala wa Kijiji cha Ichesa ambaye ndiye alikuwa akisambaza Kata ya
Myovisi.
Mjumbe wa kamati ya ugawaji wa vocha ya Kijiji cha Ichesa,Bw.Mashaka Mwashambwa anasema  hajawahi kusikia madai hayo na kazi wanayoifanya kamati ni kubwa kwani kabla ya kugawa wanatoa elimu kuhusu thamani ya vocha na punguzo lililotolewa na serikali baada ya kuitisha mkutano wa
hadhara na baadaye walitembelea mashamba na kugawa vocha kwa wahusika.

Hata hivyo wajumbe wengine watano kati ya sita akiwemo Mwenyekiti na Katibu wa Kamati ya Vocha ya kijiji cha Ichesa hawakuweza kupatikana kuelezea sakata hilo.

Ofisa kilimo Kata ya Myovisi Bw.Danfod  Mandali   amethibitisha kupokea malalamiko ya mbegu feki  na hivyo alichukuwa hatua ya kuwasiliana na Ofisa wa kilimo Wilaya ya Mbozi ambaye alifika na timu
ya wataalamu waliwahoji wakulima na kuchukua sample.

Bw.Mandali anasema  suala la madai ya baadhji ya wakulima kuuza vocha kwa wakala halijamfikia rasm,i ila kuna tetesi mitaani wakulima wakiwataja wenzao wanaolalamika kuuza kwa bei ya chini vocha hizo baada ya kuziona hazina kazi tena kutokana na mazao yao kukomaa.

"Wakulima ni kama asilimia 40 walioathirika na mbegu hiyo na kuhusu kuuza vocha  nimewahi kuwasikia wakulima wakiwataja wenzao waliouza kwa wakala huyo  lakini wanaficha ficha kuhofia kukosa kupata katika msimu unaokuja  kwa sababu kisheria ni makosa...huku ilikuja UREA tena kwa kuchelewa mwezi Machi,mbegu na mbolea ya kupandia walisema imehifadhiwa mkoani watapewa mwezi septemba, kwa ajili ya msimu wa 2012 na 2013,"alisema.

Wakala aliyedaiwa kugawa mbegu na kununua vocha katika kijiji cha Ichesa, Bw.Japhet Ntandala alipohojiwa kuhusiana na tuhuma hizo alikanusha na kulaani vikali kwamba wanataka kumchafua mbele ya wananchi wake na kwamba yupo tayari kununua mahindi yote kwa wale aliowauzia mbegu ili wananchi wake wasife na njaa.

Wakala huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kijiji hicho anasema  hajawahi kununua vocha na angependa mtu aliyedai amemuuzia ajitokeze ili azungumze ukweli na yupo tayari kufika naye mahakamani ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.

Ofisa Kilimo Mkoa wa Mbeya ,Dkt.Philipo Mwaisoba alishukuru kupata taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia huku akidai ni hatari kubwa endapo vocha za ruzuku zimeuzwa tena kwa wakala kwani ni makosa  sheria na kwamba atafuatilia kujuwa mbegu hizo zinazodaiwa feki na kutolea majibu.

Hata hivyo Gazeti hili lilimtafuta Mwakilishi wa Kampuni ya Pannar  inayodaiwa kusambaza mbegu hizo feki Bw.Tulio  ambaye baada kuulizwa na gazeti hili alisema kuwa   hakuna mbegu feki katika kampuni yake na kusema kuwa watafika katika kijiji hicho kuangalia ni nani aliyesambaza mbegu hizo.

“Hawa najua ni watu au makampuni yanayotupiga vita kuhusiana na utoaji wa mbegu  zetu ,sisi mbegu zetu ni bora.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kuna taarifa ya kusambazwa kwa mbegu hizo feki karibu maeneo mengi ya Wilaya ya Mbozi na kuna hofu ya wananchi walio wengi kupata madhara ya kiafya na hali ngumu ya maisha kutokana na mahindi hayo kukataliwa na wanunuzi wa mazao.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger