Habari na Ezekiel Kamanga, Chunya.
Wakazi wawili wa Kijiji cha Iyovyo,
Kata ya Totowe, Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wamejeruhiwa kwa risasi
kufuatia vurugu kuzuka kijijini hapo mnamo Oktoba 7 mwaka huu majira ya
saa 12 jioni.
Diwani wa Kata ya Totowe mheshimiwa
Godian Wangala, amewataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Bi, Asha
Juma(31) na Bwana Yasin Damisiano Nambuyu(44) ambalo walijeruhiwa vibaya
na Askali waliokuwa na silaha kwa lengo la kumkamata mhalifu Zunzu
Sengeka(38), anayetuhumiwa kubaka na kulisha mifugo katika mashamba
kadhaa katika Kitongoji cha Maleza hivi karibuni.
Mtuhumiwa huyo na wenzake 9 walimbaka
mke wa mkulima kijijini hapo baada ya kumfungia mumewe katika nyumba
yake na kumjeruhi vibaya na kutokomea kusikojulikana, lakini baada ya
ukatili huo kutendeka mwanamke alikimbizwa katika Zahanati ya Mkwajuni
na taarifa kutolewa Kituo cha Polisi cha Galula wilaya hiyohiyo.
Aidha, baada ya taarifa hizo Jeshi la
polisi wakiwa na pikipiki walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Bwana
Sengeka ndani ya kijiji hicho hicho na kisha kumfunga pingu na kumpakia
katika pikipiki hiyo na walipojaribu kuondoka mtuhumiwa alifanya vurugu
na kusababisha pikipiki kuanguka ndipo kundi la wafugaji wakiwa na
silaha mbalimbali za jadi na fimbo walianza kuwashambulia askari hao.
Hali hiyo iliwalazimu Askari kufyatua
risasi kwa ajili ya kuwatawanya wananchi hao ndipo ziliwajeruhi Bi Asha
na Bwana Nambuyu miguuni na kukimbizwa Kituo cha Afya cha Mkwajuni
ambapo hali zao kwa sasa wanaendelea vema baada ya kufika kituoni hapo
kutokana na juhudi kubwa za Diwani kwa kutumia pikipiki mbili majira ya
saa saba usiku Oktoba 8 mwaka huu.
Hata hivyo Kamanda wa Jeshi la Polisi
Mkoani Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kutoa onyo kwa wananchi kutojichukulia sheria mikononi na kuahidi kuwa
wale wote waluiohusika na tukio hilo watashughulikiwa kwa mujibu wa
sheria. Mgogoro wa wakulima na wafugaji umedumu kwa muda mrefu bila
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
0 comments:
Post a Comment