Pages


Home » » WANANCHI WAKATAA KUKATWA SHILINGI 200/= KWA AJILI YA HISA

WANANCHI WAKATAA KUKATWA SHILINGI 200/= KWA AJILI YA HISA

Kamanga na Matukio | 04:36 | 0 comments
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Wananchi wa Tarafa  ya Itaka inayojumuisha kata ya Bala, Halungu, Itaka na Nambizo, wilayani Mbozi wamekataa kukatwa shilingi 200 toka kwenye mauzo yao ya kahawa kwa ajili ya kuchangia hisa ya uanzishwaji wa benki ya wananchi wa wilaya humo.

Katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika wilayani hapo uliazimia kila mkulima kukatwa shilingi 200 toka katika mauzo yao ya kahawa ambapo madiwani hao baadhi yao walionekena kutofautiana na kauli ya Charles Chenza, ambaye ni mwaandaji wa rasimu ya uanzishwaji wa benki ya wananchi wilaya ya Mbozi ambapo alisema kuwa kila mkulima wa zao hilo atakatwa kiasi hicho cha fedha ili kuchangia hisa ya benki hiyo.

Kufuatia kauli hiyo ya Chenza, wananchi tarafa hiyo waliamua kuitisha mkutano wa ndani agosti 18 mwaka huu katika kata ya Halungu ukihusisha madiwani toka kata zote za tarafa hiyo, na vikundi 24 vinavyohusika na ununuzi wa kahawa ambapo kwa pamoja walipinga kauli hiyo.

Wananchi hao walisema walifikia uamuzi huo wa kupinga kwa madai yakuwa hawakuwashirikishwa  katika kikao chochote na kukubaliana na maamuzi hayo kwani suala la ununuzi wa  hisa ni hiari ya mtu na kwamba walisema kuwa wao hawapingi kuanzishwa kwa benki hiyo.

Eribariki Msukwa, mkazi wa Nambizo, alisema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wamekuwa wakionewa mara kwa mara kwa kukatwa fedha zao za mazao hususani zao la kahawa na fedha hizo kutokuwa na maelezo ya kutosha huku serikali ikishindwa kuwasaidia.

Alisema kuwa baada ya kikao hicho waliazimia kuunda kamati itakayokwenda kumuona mkuu wa wilaya hiyo Dr. Michael Kadeghe, mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro na hatimaye kwenda Bodi ya Kahawa(TCB) Moshi ili kupinga kwa ukatwaji wa fedha hizo.

Aidha, walisema kuwa endapo itashindikana kupata msaada toka kwa viongozi hao wanaokusudia kuwafuata basi wataamua kwenda moja kwa moja mahakamani ili kudai haki yao.

Hata hivyo madiwani wa kata hizo kwa pamoja walionekana kupingana na kauli iliyotolewa na mwandaaji wa rasimu ya uanzishwaji wa benki hiyo,Charles Chenza ndani ya kikao hicho ambapo hata baada ya hapo madiwani hao waliweza kukaa na wanachi wao ili kuwapa taarifa na ambapo waliamua kwa pamoja kupinga suala hilo.

Madiwani hao ni pamoja na  Wiston Songa,toka kata ya Bara, Alan Mgula toka kata ya Itaka, Samson Simkoko toka kata ya Halungu,Bernad Mweniyonde wa kata ya Nambizo, na Salome Kibweja diwani viti maalum.

 Katika kamati hiyo walioteuliwa ni Eribariki Msukwa toka kata ya Nambizo, Cairo Msyete wa kata ya Bara, Taji Mwashambwa wa kata ya Itaka na Lewadi Sikaponda wa kata ya Halungu.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger