Pages


Home » » MAKALA JUU YA VITAMBULISHO VYA TAIFA

MAKALA JUU YA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Kamanga na Matukio | 05:47 | 0 comments
Makala na Ester Macha.
UDANGANYIFU  wa vitambulisho vya Taifa  wenye lengo la utambuzi wa watu Nchini umeingia dosari baada ya watendaji wa mitaa na  kata katika maeneo yao kugeuza zoezi hilo kuwa mradi wao binafsi na kusahau dhamana waliyopewa na serikali ya  kuwatumikia wananchi.

Kutokana na Unyeti wa zoezi hili kuna umuhimu wahusika wakuu waweze kuchukuliwa hatua mapema kwani Jiji Dar Es Salaam  ndo limeanza ndo wamekuwa wa kwanza kuanza mchakato huo sasa endapo mamlaka ya

vitambulisho ikifanya mzaha kuna hatari maeneo mengine yakashindwa kufikia malengo  vizuri kama ilivyotarajiwa zoezi hili.

Tunafahamu kuwa zoezi kama hili ni nyeti kwa Taifa lakini kinachokuja kushangaza ni kuona baadhi ya watendaji ambao si waaminifu wanataka kufanya mchezo kuhusu suala la vitambulisho ambalo ni muhimu ambalo linatakiwa kupewa kipaumbale.


Ni dhahili kuwa katika maeneo mengine ya Jijini Dar Es Salaam hayataweza kufanikisha zoezi hili  na wananchi walio wengi hawataweza kupata vitambulisho vya Taifa kutokana na urasimu uliopo na rushwa

iliyokithiri miongoni mwa watendaji ambao si waaminifu .

Nionavyo katika zoezi hili kumekuwa na changamoto  mapema kabla ya hata zoezi hilo halijakamilika mapema  hivyo kuna wajibu kwa serikali kufanya kila linalowezekana  kutoa elimu kwa wananchi kupitia

wenyeviti wake wa serikali kuhusu vitambulisho vya Taifa kuwa vinatolewa bure.

Hata hivyo katika zoezi hilo watendaji watatu wa mitaa walikamatwa kuhusiana na kuchukua rushwa kwa wananchi kati y ash.1000 mpaka 3000 kwa lengo la kuwaandikia barua ambazo zinaonyesha kuwa ni wakazi wa maeneo yao.


Pia maeneo ambayo yamekubwa na adha hiyo ni Yombo Vituko,Mwabe Pande na Bunju ambapo wananchi wake walidaiwa fedha na watendaji wa mitaa ili waweze kukamilishiwa zoezi la kupata vitambulisho hivyo.


Nionavyo serikali isipokuwa makini kuna hatari vijana na wazee waliopo Mijini na Vijijini kukosa vitambulisho vya Taifa hasa vijijini ambako watadanganywa sana na watendaji hawa ambao huko vijijini hujifanya miungu watu na kuwanyanyasa wananchi.


Katika hili Mamlaka inayohusika na vitambulisho lazima iwe makini na zoezi hili hasa vijijini kwani vitambulisho hivi vinaonekana kuwa dili kubwa  kwa watendaji wa mitaa hata wa kata kwani hawa jambo lao

ni moja.

Ili kukomesha tabia hii ninachofikiri ni kwa Halmashauri zinazohusika na utoaji wa ajira kusitisha ajira zao kwani kama hili limefanyika Dar Es Salaam je kwa mikoani itakuwaje ambako ndo kuna watu wengi ambao

hata hawaelewi chochote kile ,kufanyike utaratibu mzuri ambao utaweza kupelekea kila mmoja aweze kupata kitambulisho cha Taifa.

Ushauri wangu kuhusu  zoezi hili kwa Mamlaka ya  ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)kufanya kazi hii kwa undani zaidi kwani inawezakana kuwa kukawa na maeneo mengine  ambako kuna tatizo la upatikanaji wa

vitambulisho ,hivyo ni muhimu wakajaribu kupitia maeneo mtaa kwa mtaa ili kuweza kubaini tatizo na kulifanyia ufumbuzi  ili Mikoa na wilaya ambazo zinatarajia kufanya zoezi hili isitokee dosari.

Katika hili tayari baadhi ya wananchi wameanza kukatishwa tamaa kutokana na mchezo mchafu uliongia wa kutoa rushwa kwa viongozi wa mitaa il waweze kupatiwa huduma hiyo.


Lakini pia ikumbukwe kuwa wakati mpango wa uchangishaji fedha hizo kwa wananchi awali Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) inasisitiza kuwa uandikishaji huo ni bure na kuwa mwananchi yeyote hapaswi kutozwa fedha au gharama nyingine zozote lakini watendaji hawa wamekuwa wakienda tofauti na matakwa  na NIDA.


Dhuluma hii imekuwa ikifanyika kwa watu ambao hawana vitambulisho,kama vile kadi ya mpigakura, cheti cha kuzaliwa, ubatizo au hati ya kusafiria na ndipo maofisa waandikishaji huwaelekeza kwenda kwa watendaji wa mitaa na kata ili waweze kupata uthibitisho kuwa ni raia.


Nionavyo serikali isipokuwa makini kuna hatari zoezi hili lisiweze kukamilika vizuri kama ilivyotarajiwa endapo wahusika wanaohusika  na utozaji wa fedha hawatachukuliwa  hatua na pia kuwepo  na ufuataliaji

makini katika vituo vyote.

Lakini hivi karibuni Msemaji wa Nida,Bi. Rose Mdami alisema kuwa mwananchi yeyote hapaswi kutoa fedha yoyote ili kufanikisha mkakati wa kuandikishwa, hivyo akawaonya maofisa waandikishaji na wale wa serikali za mitaa kuacha tabia hiyo mara moja.


Mimi nadhani onyo hilo pekee halitoshi kinachotakiwa  kwa mamlaka ya vitambulisho ni kuwachukulia hatua kali wale wote waliohusika na utozaji wa fedha wakati zoezi hilo lilipoanza mapema mwezi wa saba mwaka huu.


Mamlaka ya vitambulisho Taifa ikumbuke kuwa zoezi hilo ni nyeti ambalo linatakiwa lifanywe  kwa umakini na hao wahusika waliokamatwa wachukuliwe hatua isiishie kukamatwa na polisi tu, zoezi hili bado linatakiwa kufanyika katika mikoa mingine sasa endapo wahusika wakikamatwa  na kuwekwa ndani na kutolewa  na kuishia mitaani bila ya kuchukuliwa hatua zozote za kinidhamu kuna hatari mikoa mingine ambako zoezi  hili linatarajiwa kuendeshwa  kutofanikiwa hasa maeneo ya vijijini.


Nionavyo  hawa watendaji wa mitaa na kata wanaweza kuitia serikali katika matatizo kwani kwa mtindo huu  uraia unaweza kutolewa kiolela kwa wageni na watanzania kubaki wakiwa hawana uraia katika serikali 
lazima iwe macho na watendaji wake,kwasababu wamezoea kila mpango unaoletwa na serikali kwao wanaona ni sehemu ya kujipatia fedha.

Ifike wakati watendaji waweke kipaumbele kazi waliyopewa  na serikali badala ya kuweka maslahi mbele  kuliko dhamana waliyopewa na serikali ya kuwatumikia wananchi.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger