Pages


Home » » TAKUKURU WAMPIGA NA KUMJERUHI MWANAMKE - MBARALI MKOANI MBEYA.

TAKUKURU WAMPIGA NA KUMJERUHI MWANAMKE - MBARALI MKOANI MBEYA.

Kamanga na Matukio | 03:05 | 0 comments
Na Ezekiel Kamanga,Mbarali
Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (TAKUKURU)wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya inatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili  wake mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Udindilwa kata ya Ruiwa Bi Sarah Paulosi (32)baada ya kukataa kusaini hati ya wito ya mumewe .

Hati hiyo ya wito ilitoka ofisi ya TAKUKURU ikimtaka mume wa  mama huyo Bw. Kassimu Watson ambaye piqa ni mwenyekiti wa kijiji cha Udindilwa kufika haraka katika ofisi hizo bila maelezo zaidi ya kumtaka afike haraka.

Akizungumza na gazeti hili jana Bi.Paulosi alisema kuwa tukio hilo lilitokea agosti 14 mwaka huu majira ya saa 7 mchana akiwa nyumbani kwake ndipo walipotokea maafisa hao wakiwa na gari yao.

“Nikiwa nyumbani kwangu niliona gari ikiwa na watu wanne ambapo kati ya hao wawaili walishuka katika gari  hilo na kuanza kuniuliza kuwa mume wangu yupo wapi nikawajibu kuwa mume wangu hayupo toka jana,kwani ana wake wawili na siku hiyo alikuwa kwa mke mwingine lakini hawakuridhika na maelezo yangu ndipo walipoanza kunipiga kwa mateke na ngumi wakiniamuru kusaini hati ya wito wa mume wangu  kwa
lazima”alisema.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruiwa Bw. Jordan Masweve alisema kuwa hakuwa na taarifa za ujio wa maafisa hao wa TAKUKURU kutoka wilayani .

Hata hivyo Diwani wa Kata hiyo Bw. Alex Mdimilaje alisema amesikitishwa na zoezi hilo kwa kwa kutotoa taarifa ofisi za kata kwani wao hufanya kazi kwa ushirikiano na ofisi zote zinatoa taarifa katika kata na hutoa ulinzi kuhakikisha wanafanya kazi kwa usalama bila kubugudhiwa.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye alitafutwa na maafisa hao bila mafanikio alisema kwamba siku walipokuja maafisa hao alikuwa safarini .

“Baada ya kurudi tu nyumbani kwangu nilikuta  hati ya wito  ambayo ilikuwa imetoka ofisi za TAKUKURU ikinitaka kufika ofisini na kumkuta mke wangu amejeruhiwa kwa kipigo na kulazimika kutoa taarifa ofisi za kata  na kupewa barua ya kwenda polisi wilayani ambako mke wangu alipewa barua ya kwenda kutibiwa hospitali ya wilaya ambapo alirudi na kufungua jarada lenye namba RUJ/IR/1058/2012”alisema.

Kwa upande wake Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Mbarali Bw. Ramadhani Ndwata alisema hakuna tukio lolote lililotokea na mara nyingi wamekuwa wakifanya ziara hizo  vijijini pindi inapolazimu ili kupata vielelezo kuhusiana na hoja mbali mbali zinazoletwa katika ofisi hizo kwa uchunguzi.
Share this article :

0 comments:

 
Support : Creating Website | Greyson Salufu Template | Chimbuko Letu Inc
Copyright © 2011. Kamanga na Matukio - All Rights Reserved
Template Modify by Chimbuko Letu Inc
Proudly powered by Blogger